Kwa wakazi wengi wa jiji la Dar es Salaam, usafiri wa kila siku umeendelea kuwa chanzo cha malalamiko, kuanzia gharama zisizotabirika, upatikanaji wa madereva katika nyakati muhimu, hadi malalamiko ya makato kwa madereva wa majukwaa ya usafiri wa mtandaoni. 

Wakati mahitaji ya huduma hizo yakiongezeka, maswali yamekuwa mengi zaidi kuhusu nani ananufaika na mfumo uliopo.

Ni katika mazingira hayo ambapo huduma mpya ya usafiri wa kidijitali, Bantu Ride, imeingia sokoni, ikilenga kujipenyeza katika sekta inayokua kwa kasi lakini inayokabiliwa na changamoto za kijamii na kiuchumi.

Akizungumza wakati wa uzinduzi wa huduma hiyo, February 4, Mkurugenzi Mtendaji wa Bantu Ride, Peter Msanga, alisema kuwa kuanzishwa kwa jukwaa hilo ni sehemu ya juhudi za kutumia teknolojia kutatua changamoto halisi za usafiri zinazowakabili Watanzania kila siku.

“Leo tunazindua rasmi Bantu Ride, huduma ya usafiri wa kidijitali iliyojengwa kwa ajili ya Watanzania. Ni jukwaa la ndani linaloelewa mazingira yetu, changamoto zetu na mahitaji ya wasafiri wa kila siku,” alisema.

Mr Msanga, aliongeza kwa kusema kwamba lengo kuu la Bantu Ride si tu kurahisisha upatikanaji wa usafiri kwa abiria, bali pia kuhakikisha madereva wanapata kipato cha haki bila mzigo mkubwa wa gharama.

“Tunalenga kutoa usafiri unaoaminika, salama na wa bei nafuu kwa abiria, huku tukiwawezesha madereva wetu kupata kipato cha haki kupitia matumizi ya teknolojia ya kisasa,” aliongeza.

Kwa upande wake, Marketing and Consultant Advisory wa Bantu Ride, Ellinipendo, alisema huduma hiyo imezingatia zaidi mahitaji ya makundi mawili makuu yanayoendesha sekta ya usafiri wa mtandaoni abiria na madereva.

Alieleza kuwa kwa abiria, changamoto kubwa imekuwa gharama na upatikanaji wa usafiri, huku kwa madereva, malalamiko mengi yamekuwa yakihusu makato makubwa na ukosefu wa uhakika wa kipato.

“Tumejaribu kusikiliza pande zote mbili. Lengo ni kuhakikisha abiria anapata usafiri wa bei nafuu na salama, huku dereva akipata kipato cha haki kinachomsaidia katika maisha ya kila siku,” alisema.

Kwa mujibu wa kampuni hiyo, Bantu Ride inapatikana kupitia App Store na Play Store, na inafanya kazi kwa saa 24. Huduma hiyo pia inatajwa kutoa vivutio vya muda mfupi kwa watumiaji wapya, huku ikisisitiza kuwa mkazo mkubwa umewekwa katika urahisi wa matumizi na upatikanaji wa huduma.

Ellinipendo aliongeza kuwa jukwaa hilo si tu suluhisho la usafiri, bali ni sehemu ya juhudi za kutumia teknolojia ya kisasa kuboresha maisha ya watu wa kawaida, hasa wale wanaotegemea usafiri wa mtandao kwa shughuli zao za kila siku.

Wakati huduma za usafiri wa kidijitali zikiendelea kushika kasi nchini, wadau wa sekta hiyo wanaendelea kufuatilia kwa karibu namna majukwaa mapya kama Bantu Ride yatakavyoweza kujibu changamoto zilizojitokeza katika mifumo iliyopo, ikiwemo masuala ya gharama, usalama na maslahi ya madereva.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *