Kagame aliyasema haya wakati ambapo shinikizo linazidi huko Marekani kwa taifa hilo kuwekewa vikwazo zaidi kutokana na kuhusika kwake katika Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo.

Akizungumza katika hafla moja katika Mji Mkuu wa RwandaKigali, Kagame alionekana kuzungumza kwa kusisitiza kujitegemea kwa nchi yake.

Kukerwa na jamii ya kimataifa

Amesema kuwa Rwanda imedhamiria kujitegemea ili uwepowake usitegemee bahati au nia ya wengine wanaoweza kuchagua kuwasaidia sasa na kusitisha usaidizi siku zijazo.

Rais Paul Kagame wa Rwanda na Felix Tshisekedi
Rais Paul Kagame wa Rwanda (kushoto) na Felix Tshisekedi (kulia)Picha: Virginia Mayo/AP/picture alliance

“Kiasi cha vitisho tunavyopata kila siku, oh tutafawafanyia hivi musipofanya hivi, tutawafanyia vile musipofanya hivi…unajua wakati mwengine nahisi kukerwa sana na maneno kama haya…ila badala ya kukerwa na yote haya, nitakerwa kwa kukataa na kuwaambia, kwendeni huko,” alisema Kagame.

Rwanda inasisitiza kuwa kuhusika kwake mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo ni kusaidia dhidi ya kundi la wanamgambo lililoundwa kutokana na wale waliofanya mauaji ya kimbari ya mwaka 1994 nchini Rwanda.

Kagame amekanusha kuhusika kijeshi kwa Rwanda moja kwa moja nchini humo licha ya ushahidi wa wazi kutoka kwa waangalizi wa Umoja wa Mataifa na wengine.

“Unajua hawa Wakongo wana bahati sana, huyu Tshisekedi ambaye anasimama na kutusi watu na kuwatishia kisha mwishowe, jamii hiyo hiyo ya kimataifa inakuja kwangu na kusema, ndio ndio, unastahili kufanya hivi na hivi…mimi nasema, nini? Na nawaambia….hamuoni kwa kufanya hivyo munamfurisha kichwa huyu bwana asitafute suluhu la matatizo yao?” alisema Kagame.

Balozi wa Rwanda nchini Marekani Mathilde Mukantabana kwa mara ya kwanza mnamo Januari 22 wakati wa kikao cha kamati ya bunge la Marekani kuhusu masuala ya kigeni, alikiri kuhusika kwa Rwanda katika operesheni ya moja kwa moja ya usalama na waasi wa M23 na tawi lake la kisiasa la AFC.

Kuzuia uvamizi unaotishia uwepo wa Rwanda

Mukantabana alisema Rwanda imechukua hatua hiyo ili kuzuia uvamizi mwengine wa mpakani kama ule uliofanyika katika miaka 1990, ambao unaweza kutishia uwepo wa Rwanda.

Rais Trump wa Marekani akisaini mkataba wa amani kati ya Marais Kagame wa Rwanda na Tshiskedi wa Kongo
Rais Trump wa Marekani akisaini mkataba wa amani kati ya Marais Kagame wa Rwanda na Tshiskedi wa KongoPicha: Chip Somodevilla/Getty Images/AFP

Kamati hiyo ya mambo ya kigeni ya bunge la Rwanda iliunga mkono Rwanda kuwekewa vikwazo.

Nchi hiyo ndogo iliyo katika ukanda wa Maziwa Makuu imejikuta katika shinikizo la kimataifa linalozidi kuongezeka kufuatia ushirikiano wake na waasi wa M23, kundi ambalo mwaka jana liliteka eneo kubwa la mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo.

Mkataba wa amani kati ya Rwanda na Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo uliosimamiwa na Rais wa Marekani Donald Trump, ulisainiwa Washington kuelekea mwishoni mwa mwaka jana ila siku chache baadae, waasi wa M23 wakauteka mji wa Uvira.

Chanzo: AFP

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *