
Dar es Salaam. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, anatarajiwa kulizindua rasmi Soko Kuu la Kariakoo Februari 8, 2026.
Taarifa hiyo imetolewa leo Ijumaa, Februari 6, 2026, na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila, alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari kuhusu ziara ya Rais Samia mkoani Dar es Salaam.
Chalamila amesema Rais Samia atawasili mkoani Dar es Salaam Jumapili saa mbili asubuhi kwa ajili ya uzinduzi wa soko hilo.
Amesema mbali ya kuzindua soko, Rais Samia ameupatia heshima Mkoa wa Dar es Salaam ya kufanya ziara ambayo ni heshima kubwa kwa wakazi wa mkoa huo.
“Februari 8, 2026 Rais Samia Suluhu Hassan ametupatia heshima ya kufanya ziara katika mkoa wetu kwa lengo la kuzindua Soko Kuu la Kariakoo. Mtakumbuka soko hili liliungua, na Rais kupitia Ofisi ya Rais–Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa alitoa maelekezo ya haraka kwamba soko lijengwe upya na kurudi katika hali yake ya awali. Leo tuna furaha kuwataarifu Watanzania kuwa kazi hiyo imekamilika, zaidi ya Sh28 bilioni zilitolewa na Serikali kwa ajili ya ujenzi wake,” amesema Chalamila.
Kutokana na uzinduzi huo, mkuu wa mkoa huyo amewataka wafanyabiashara wote waliovamia na kuziba njia za kuingia sokoni hapo kuziachia mara moja kabla ya siku ya uzinduzi, ili kuruhusu miundombinu ya soko kutumika kama ilivyokusudiwa.
Amesema wakati soko hilo likiungua, lilikuwa na wafanyabiashara wengi, na kwamba Shirika la Masoko Kariakoo linaendelea kutekeleza maelekezo ya Rais Samia ya kuhakikisha wafanyabiashara wote waliokuwepo awali wanarejeshwa katika soko hilo.
Kuhusu maboresho yaliyofanyika, Chalamila amesema yameongeza tija ya soko hilo, huku zaidi ya wafanyabiashara 1,500 wanatarajiwa kufanya shughuli zao ndani ya soko hilo jipya, likiwa na maeneo maalumu ya biashara, ikiwamo sehemu za vizimba.
Ameongeza kuwa soko hilo lina uwezo wa kuhudumia zaidi ya magari 400 kwa wakati mmoja, na kuwataka wakazi wa Dar es Salaam kujitokeza kwa wingi kushuhudia uzinduzi huo.
“Nawaomba machinga wa Dar es Salaam, wafanyabiashara wa Kariakoo na wale wa kati wajitokeze kwa wingi ili kumuunga mkono Rais Samia. Pia, niwatangazie rasmi wafanyabiashara ndogondogo walioweka vibanda kwenye njia za kuingia sokoni, huu si wakati wa kutumia nguvu bali ni wakati wa kuziachia barabara ili ziweze kupitika,” amesema.
Chalamila amesema Soko la Kariakoo ni muhimu si kwa Tanzania pekee, bali pia kwa nchi za ukanda wa Kusini na Kati mwa Afrika, akieleza kuwa wafanyabiashara kutoka Zimbabwe, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), Malawi na Zambia wamekuwa wakifanya biashara katika soko hilo, hivyo kulifanya kuwa kituo kikubwa cha biashara na kielelezo cha diplomasia ya kiuchumi.
Amewataka wakazi wa Dar es Salaam kujitokeza kwa wingi kushuhudia uzinduzi huo kwa kuwa soko hilo ni zawadi na kielelezo kikubwa kwa wananchi.
Historia ya Soko la Kariakoo
Soko la Kariakoo liliungua mwaka 2021, Serikali ilitenga Sh28 bilioni kwa ajili ya ujenzi wake upya. Katika kipindi cha ujenzi, wafanyabiashara waliokuwa wakifanya shughuli zao sokoni hapo walihamishiwa katika masoko ya Kisutu, Karume na Machinga Complex.
Baada ya ujenzi kukamilika, Mwenyekiti wa Bodi ya Shirika la Masoko Kariakoo, Hawa Ghasia aliwahi kusema soko hilo lingefunguliwa rasmi Aprili 2025. Alitoa kauli hiyo Aprili 4, 2025, katika hafla ya kumkabidhi ofisi meneja mpya wa shirika hilo, Ashraph Yusuph Abdulkarim, iliyofanyika katika ofisi za shirika hilo Kivukoni, Dar es Salaam.