Miaka 27 imepita tangu Profesa Hubert Clemence Kairuki, mwasisi wa Hospitali ya Kairuki, alipofariki dunia. Hata hivyo, maono yake makubwa na mchango wake wa kipekee katika sekta za afya, elimu na viwanda bado vinaendelea kuishi, kukua na kuleta matokeo chanya kwa jamii ya Watanzania na vizazi vijavyo.

Leo hii, tunapokumbuka maisha na kazi za Profesa Kairuki, tunasherehekea urithi wa fikra na dhamira aliyoiacha urithi unaoendelea kuwa nguzo ya matumaini kwa Watanzania wengi wanaotamani kupata huduma bora za afya na elimu.

Hospitali ya Kairuki, iliyoanzishwa mwaka 1987, ilikuwa hatua ya kihistoria katika maendeleo ya huduma za afya binafsi nchini Tanzania. Wakati huo, Profesa Kairuki alitambua changamoto kubwa ya msongamano wa wagonjwa katika hospitali za umma na upungufu wa huduma bora za matibabu.

Hali hiyo ilimchochea kuanzisha hospitali binafsi yenye lengo la kutoa huduma za afya zenye ubora wa hali ya juu, kwa ufanisi na kwa kuzingatia mahitaji ya Watanzania wa makundi yote ya kijamii na kiuchumi.

Kupitia uongozi wake mahiri, maadili ya kazi, na usimamizi uliojikita katika ubora na weledi, Hospitali ya Kairuki ilikua kwa kasi na kujijengea heshima kama mojawapo ya vituo bora vya huduma za afya nchini. Huduma zake zilizingatia uharaka, usalama wa mgonjwa, na utekelezaji wa miongozo ya kitaifa ya Wizara ya Afya.

Pamoja na mafanikio haya, Profesa Kairuki alielewa wazi kuwa uendelevu wa sekta ya afya hauwezi kupatikana bila kuwa na rasilimali watu ya kutosha na yenye ujuzi wa hali ya juu.

Kwa msingi huo, mwaka 1997 alianzisha chuo kikuu cha mafunzo ya afya kilichojulikana awali kama Mikocheni International University. Baada ya kifo chake, chuo hicho kilibadilishwa jina na kuitwa Hubert Kairuki Memorial University (HKMU) kama ishara ya kumuenzi.

Mwaka 2024, chuo kikuu hicho kilipata jina jipya la Kairuki University (KU) ili kulinganisha utambulisho wake na taasisi nyingine zilizo chini ya mwamvuli wa Kairuki Health and Education Network (KHEN).

Chuo hiki kimeendelea kutoa elimu ya kiwango cha kitaifa na kimataifa katika fani za udaktari, uuguzi na taaluma nyingine za afya, kikizalisha maelfu ya wataalamu wanaohudumu ndani na nje ya nchi.

Profesa Kairuki aliamini katika elimu ya vitendo, matumizi ya teknolojia ya kisasa na ubunifu katika tiba. Mtazamo huu umeendelea kuonekana katika uwekezaji wa teknolojia za kisasa za matibabu, ikiwemo huduma ya kuondoa uvimbe mwilini bila upasuaji kwa kutumia teknolojia ya HIFU (High-Intensity Focused Ultrasound), mojawapo ya tiba za kisasa zinazopatikana leo nchini.

Akifahamu mchango mkubwa wa wauguzi katika mfumo wa huduma za afya, Profesa Kairuki pia alianzisha Shule ya Uuguzi ya Kairuki, yenye lengo la kutoa mafunzo ya kina, ya kitaaluma na ya kimaadili.

Hadi leo, shule hiyo imeendelea kuzalisha wauguzi mahiri wanaotoa huduma kwa weledi mkubwa katika taasisi mbalimbali za afya nchini na nje ya mipaka ya Tanzania. Maono ya Profesa Kairuki hayakuishia katika hospitali na elimu pekee. Alitambua pia umuhimu wa huduma za kisasa za uzazi katika jamii.

Kwa msingi huo, muanzilishi mwenza Mama Kokushubira Kairuki, kwa kushirikiana na Bodi ya Wakurugenzi, waliendeleza maono haya kwa kuanzisha Kituo cha Uzazi Pandikizi (IVF) kituo kinachotoa huduma za kisasa na tumaini jipya kwa wanandoa wanaokabiliwa na changamoto ya kupata watoto kwa njia ya kawaida.

Kituo hiki kimeleta mageuzi makubwa katika huduma za uzazi nchini, kikiwa miongoni mwa vituo vinavyoongoza katika utoaji wa tiba za uzazi kwa viwango vya kimataifa, na kimekuwa msaada mkubwa kwa familia nyingi kutoka ndani na nje ya nchi.

Zaidi ya hayo, Profesa Kairuki aliona umuhimu wa uwepo wa viwanda vya ndani vya dawa ili kuhakikisha upatikanaji wa dawa bora, salama na kwa gharama nafuu. Katika kuendeleza maono hayo, Kairuki Pharmaceuticals Industry Limited (KPIL) ilianzishwa kama sehemu ya mkakati wa kuimarisha uzalishaji wa dawa nchini.

Kiwanda hiki kimechangia kwa kiasi kikubwa kupunguza utegemezi wa dawa kutoka nje ya nchi na kuimarisha sekta ya viwanda vya dawa nchini.

Zaidi ya nafasi yake ya kiuongozi, Profesa Kairuki alikuwa mtu aliyethamini ushirikishwaji, mshikamano na jitihada za pamoja. Aliamini kuwa maendeleo ya kweli hayawezi kupatikana kwa juhudi za mtu mmoja, bali kwa ushirikiano wa jamii nzima inayoshirikiana kwa lengo la pamoja.

Kwa hakika, urithi wa Profesa Hubert Clemence Kairuki unaendelea kuishi si tu katika majengo na taasisi alizoanzisha, bali katika maisha ya watu wengi walioguswa na huduma, elimu na maono yake. Huu ni urithi wa kudumu, unaoendelea kuleta mabadiliko chanya katika taifa letu.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *