
Waziri wa Fedha wa Marekani Scott Kenneth Homer Bessent amekiri kuwa, Washington ilisababisha uhaba wa sarafu ya dola ya nchi hiyo ndani ya Iran, hatua ambayo ilisababisha kushuka kwa kasi kwa thamani ya sarafu ya Iran ya riali na kuibua mashinikizo ya kiuchumi yaliyochochea machafuko ya Desemba mwaka jana.
Katika kikao cha Baraza la Seneti la Marekani kilichofanyika siku ya Ijumaa, Seneta Katie Elizabeth Boyd Britt alimhoji Scott Bessent kuhusu hatua zilizochukuliwa na serikali ya rais wa Marekani Donald Trump ili kushadidisha utekelezaji wa kile kinachoitwa sera ya “mashinikizo ya juu kabiosa” dhidi ya Iran.
Akijibu suali hilo, waziri huyo wa fedha wa Marekani alisema: “tulichofanya ni kusababisha uhaba wa dola ndani ya nchi … Ulitokea haraka, na niseme kwamba, ulifikia kwenye kilele mnamo mwezi Desemba, wakati moja ya benki kubwa zaidi nchini Iran ilipoanguka”.
Bessent ameendelea kueleza: “benki kuu ililazimika kuchapisha pesa, sarafu ya Iran ilishuka bila kizuizi, mfumuko wa bei ukaripuka”.
Mbali na kusababisha uhaba wa fedha za kigeni za dola, Washington ilisukuma na kushusha pia mauzo ya mafuta ya Iran hadi kiwango cha “chini cha sifuri” ikiwa ni sehemu ya kampeni hiyo hiyo ya utoaji mashinikizo, ikishadidisha pia vikwazo vya kiuchumi kwa raia wa kawaida wa Iran huku ikifuatilia waziwazi mpango wa kuvuruga uthabiti wa kifedha.
Mnamo Januari 20, waziri huyo wa fedha wa Marekani alisema katika mahojiano kwamba vikwazo vya nchi hiyo vilibuniwa ili kuidhoofisha sarafu ya fedha ya Iran.
“Huu ni ustadi wa kiuchumi, hakuna risasi zilizofyatuliwa,” alitamka bila aibu Bessent kumaanisha utumiaji wa makusudi vya vita vya kiuchumi dhidi ya Iran…/