
Dar es Salaam. Raia wa China, Xiuzhu Yan amewasilisha maombi kortini (Habeas Corpus) dhidi ya Inspekta Jenerali wa Polisi (IGP) na Mkurugenzi wa Mashitaka Nchini (DPP), kupinga kushikiliwa mahabusu kwa siku 82 tangu Novemba 2025.
Katika maombi hayo namba 000002421 ya 2026, Yan anayewakilishwa na wakili Michael Lugina, amemuunganisha Mkurugenzi wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) na Kamanda wa Polisi (RPC) Kanda Maalum ya Dar es Salaam.
Wajibu maombi wengine katika maombi hayo ambayo yamewasilishwa chini ya ombi la usikilizwaji wa haraka (extreme urgency), ni pamoja na Mkuu wa Polisi wa wilaya (OCD) na Mkuu wa Kituo (OCS) katika mahabusu anakoshikiliwa.
Maombi hayo yamefunguliwa Februari 4,2026 katika Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Dar es Salaam na yamepangwa kutajwa Februari 10,2026 saa 4:00 asubuhi mbele ya Jaji Salma Maghimbi wa Mahakama hiyo jijini Dar es Salaam.
“Nikiwa nimepewa maelekezo kamili kuleta maombi haya kwa maoni kwamba maombi haya yana dharura na kuzuiliwa kwa mwombaji ni kinyume cha sheria na kunaathiri sana haki zake za kikatiba,” amesema wakili Lugina.
Kupitia kiapo chake, wakili Lugina ameeleza hali hiyo inasababisha uvunjaji wa utawala wa sheria na sheria zote za nchi zinazosimamia kuzuiliwa kwa mtu au ‘detention of a person’.
“Pia nilifahamisha kuwa wajibu maombi wanakataa kuwaruhusu ndugu na marafiki wa karibu wa mwombaji kupata nafasi ya kumwona tangu Novemba 14, 2025, hajawahi kupata fursa ya kukutana na mawakili wala ndugu zake,” amesema.
Tangu Novemba 14, 2025 hadi maombi hayo yanafunguliwa Februari 4, 2026, raia huyo alikuwa amefikisha siku 82 akiwa mahabusu kwa tuhuma ambazo hazikuelezwa katika kiapo cha wakili Lugina, kilichoambatanishwa na maombi.
“Hali hiyo inataka Mahakama hii kuingilia kwa uharaka ili kuokoa haki za kikatiba za mwombaji,” amesema wakili Lugina na kuiomba Mahakama itoe wito wa mahakama (summons) ili Yan aweze kufikishwa mbele ya mahakama hiyo.
Katika usikilizwaji wa maombi hayo, wakili huyo amesema wataweka mbele ya mahakama maombi 4, mojawapo ni kwa mahakama kutoa amri ya kuachiwa huru kwa muombaji, kutoka katika mahabusu za wajibu maombi anakoshikiliwa.
Pia wataiomba mahakama itoe amri ya kuwataka wajibu maombi wote kufika mbele ya mahakama na kuieleza ni kwa nini raia huyo wa China ambaye wanamshikilia kinyume cha sheria, hapaswi kuachiliwa mara moja.
Mbali na ombi hilo, pia wanaiomba mahakama itoe amri ya kuwazuia wajibu maombi kuendelea kumshikilia raia huyo wa China kinyume cha sheria za Tanzania, na mahakama itoe nafuu nyingine inayoona inafaa.
Habeus corpus huwasilishwa chini ya kifungu cha 390 (1), (a), na (b) na 191 cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai Sura ya 20 [R.E.2023] ikisomwa pamoja na Kanuni ya 2 na 12 ya Kanuni za Habeas Corpus GN 150 ya mwaka 1930.