Lindi. Takwimu zinaonesha kuwa takribani asilimia 11 ya watoto wanaozaliwa Tanzania huzaliwa kabla ya wakati (njiti) na zaidi ya asilimia 30 ya vifo vya watoto wachanga vinahusishwa moja kwa moja na matatizo ya kuzaliwa kabla ya wakati.

Akizungumza mara baada ya kukabidhiwa mashine hizo leo Jumatatu Februari 9,2026  Mkuu wa idara ya watoto hospitali ya Rufaa ya mkoa wa Lindi Sokoine, Dk Abdallah  Mwinyihija amesema kuwa, kwa mwaka 2025  mkoa wa Lindi kati ya watoto 600 waliozaliwa 200 walikuwa njiti, huku wastani kwa mwezi ni watoto njiti 20.

Dk Mwinyihija amesema   zaidi ya asilimia 60 ya watoto wachanga hupata ugonjwa wa manjano (jaundice) katika siku za mwanzo za maisha bila matibabu ya mapema inaweza kusababisha uharibifu wa ubongo, ulemavu wa kudumu au hata kifo.

“Mashine hizi zitakwenda kuboresha utoaji wa tiba salama pamoja na kusaidia kupunguza vifo vitokanavyo na watoto njiti.

Hata hivyo Mkurugenzi mkuu wa Taasisi ya kuzuia na kupambana na rushwa (Takukuru) Chrispin Chalamila amesema kuwa malengo yao ni kufikia hospitali zote 28 zilizopo Tanzania bara ili kuweza kupunguza au kuondoa kabisa vifo vitokanavyo na watoto njiti.

Amesema kuwa mashine hizo zinatolewa kwa kujitoa wao wenyewe Takukuru ili kuweza kusaidia jamii pamoja na watoto wanaozaliwa kabla ya wakati.

“Malengo yetu kama Takukuru ni kuhakikisha kuwa tunazifikia hospitali zote za rufaa  28 ili kuweza kuboresha huduma ya afya pamoja na kusaidia kupunguza vifo vitokanavyo na watoto njiti,” amesema Chalamila.

Hata hivyo Mganga Mkuu wa hospitali ya Rufaa  Sokoine Dk Kheri Kagya ameziomba taasisi nyingine kujitokeza kusaidia kama walivyofanya Takukuru, ili kuweza kuwasaidia watoto wanaozaliwa kabla ya wakati.

Dk Kagya pia ameahidi kuzitunza mashine hizo ilikuweza kuboresha utoaji wa huduma katika hospitali hiyo, na kusema kuwa mashine hizo zitakwenda kuwa mkombozi katika utoaji wa huduma .

 “Tunaahidi kuwa mashine hizi tutazitunza ipasavyo kwani zitakwenda kuwa mkombozi katika boresha huduma katika hospitali hii ya mkoa,” amesema Dk Kagya.

Naye Fatuma Selemani anayeuguza mtoto mwenye matatizo ya manjano ameishukuru Takukuru kwa msaada wa mashine hizo kwani zitasaidia katika kuondoa changamoto kwa watoto njiti na wenye manjano.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *