GAIRO: Mkuu wa Wilaya ya Gairo, Japhari Kubecha, amefanya ziara ya ukaguzi wa miradi ya madaraja na barabara wilayani humo, akiongozana na wajumbe wa Kamati ya Usalama ya Wilaya pamoja na mwakilishi wa Meneja wa Tanroads Mkoa wa Morogoro.

Katika ziara hiyo, Mkuu wa Wilaya amejionea ukamilifu wa madaraja ya Nguyami na Chakwale, sambamba na mchakato unaoendelea wa uwekaji lami kwenye barabara ya Gairo–Nongwe.

Kubecha amesema ujenzi wa madaraja hayo umeondoa changamoto kubwa zilizokuwa zikiwakabili wananchi, hususan katika kipindi cha mvua, na kurahisisha usafiri pamoja na shughuli za kiuchumi.

Ametumia fursa hiyo kumshukuru Rais DkSamia Suluhu Hassan, kwa kuendelea kuboresha miundombinu ambayo inaleta maendeleo ya moja kwa moja kwa wananchi wa Wilaya ya Gairo.
