
“Afrika inapitia baadhi ya changamoto ngumu zaidi duniani na inafanya hivyo kwa dhamira, ubunifu na mnepo,” amewaambia wanahabari. Katika mazingira ya kimataifa yaliyojaa mgawanyiko na misukosuko kuliko wakati wowote tangu kumalizika kwa Vita Baridi, amesisitiza kuwa maendeleo barani Afrika hayahusu “miujiza, bali ni kazi thabiti na ya vitendo ya kutatua matatizo halisi.”
Amani, usalama na mageuzi ya Baraza la Usalama
Akizungumzia masuala ya amani, Guterres ameeleza kuwa maeneo mengi ya Afrika yanakabiliwa na migogoro tata, ikiwemo Sudan, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo DRC, Sahel na Pembe ya Afrika.
Amesema taasisi za Afrika zinazojitahidi “kunyamazisha mtutu wa bunduki mara nyingi zimeelemewa na kukosa rasilimali za kutosha”.
Amelitaja Azimio 2719 la Baraza la Usalama kuwa “la kihistoria,” akieleza kuwa kwa mara ya kwanza linaweka utaratibu wazi wa operesheni za msaada wa amani zinazoongozwa na Muungano wa Afrika na kuidhinishwa na Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, zikifadhiliwa kupitia michango ya lazima ya nchi wanachama. “Hii ni hatua halisi kuelekea uwajibikaji wa pamoja kwa migogoro yenye athari za kimataifa,” amesema. Hata hivyo, ameeleza “masikitiko makubwa kwa kushindwa kufikiwa kwa makubaliano kuhusu ufadhili wa operesheni ya msaada na utulivu ya Muungano wa Afrika nchini Somalia”.
Amesisitiza pia umuhimu wa mageuzi ya Baraza la Usalama: “Ni wakati wa kuimarisha Baraza la Usalama kwa karne ya 2. Hii inamaanisha, hatimaye, viti viwili vya kudumu vya Afrika.”
Wito wa haki ya kifedha
Kuhusu uchumi, Katibu Mkuu ameelezea mfumo wa fedha wa kimataifa kuwa umepitwa na wakati na usio wa haki. “Mfumo wa kifedha wa kimataifa uliundwa kwa ajili ya dunia ambayo haipo tena na umekuwa ukishindwa kwa nchi nyingi zinazoendelea leo,” amesema, akiongeza kuwa uliundwa na nchi tajiri kwa kuzingatia maslahi yao wenyewe.
Licha ya Afrika kuwa na baadhi ya uchumi unaokua kwa kasi zaidi duniani, nchi nyingi zinakabiliwa na mzigo wa madeni, gharama kubwa za mikopo na ukosefu wa fedha za muda mrefu kwa ajili ya maendeleo.
“Haikubaliki kabisa kwamba Afrika, baada ya madhara ya ukoloni, bado inakabiliwa na mfumo wa kiuchumi na kifedha isio ya haki kabisa,” amesisitiza. Ametoa wito wa kuongeza mara tatu uwezo wa mikopo wa benki za maendeleo za kimataifa na kuhakikisha nchi zinazoendelea zinapata “sauti halisi na ushiriki wenye maana katika taasisi za kifedha za kimataifa”.
Haki ya tabianchi na fursa kwa Afrika
Katika suala la mabadiliko ya tabianchi, Guterres amezungumza kwa msisitizo, “Watu wa Afrika hawakusababisha mgogoro wa tabianchi. Hata hivyo, wanalipa gharama kubwa zaidi.” Ametaja ukame, mafuriko, njaa na joto kali kama mifano ya athari hizo, akisema hali hiyo ni “ukosefu wa haki wa tabianchi ulio wazi na dhahiri.”
Amezitaka nchi zilizoendelea kuongeza mara tatu fedha za kukabiliana na athari za tabianchi, kukusanya dola trilioni 1.3 kila mwaka ifikapo 2035, na kuongeza michango katika Mfuko wa Hasara na Uharibifu. Kwa msaada sahihi, amesema, Afrika inaweza kuwa “nguvu kubwa ya nishati jadidifu, na kutumia madini yake muhimu kuunda viwanda na ajira ndani ya bara hilo. Unyonyaji na uporaji wa rasilimali za Afrika lazima ukome,” amesisitiza.
Afrika Daima
Akijibu madai kuwa huenda ziara yake ni ya kuaga, Guterres amekanusha vikali. “Baadhi ya watu wanasema uwepo wangu hapa ni wa kuaga. Sio kweli,” amesema. Alihakikisha kuwa hadi tarehe 31 Desemba, Umoja wa Mataifa utaendelea kuichukulia Afrika kama “kipaumbele chake cha kwanza” katika shughuli zake zote, na kwamba ushirikiano kati ya Umoja wa Mataifa na Muungano wa Afrika unabaki kuwa “ushirikiano muhimu zaidi wa kimkakati.” Hata baada ya kumalizika kwa muhula wake, ameahidi kuwa mshikamano wake utaendelea.
“Katikati ya wasiwasi wangu na mshikamano wangu wa vitendo, daima itakuwa Afrika,” amehitimisha, akiongeza kwa Kireno: “Africa sempre. Akimaanisha Afrika daima”