Akizungumza mbele ya viongozi wa Afrika akiwemo ais João Lourenço wa Msumbiji na na Rais Évariste Ndayishimiye wa Burundi, ametoa shukrani zake za dhati kwa msaada “thabiti na wa maamuzi wa Muungano wa Afrika katika kipindi chote cha uongozi wake.

“Katika dunia iliyojaa mgawanyiko na kutoaminiana, Muungano wa Afrika ni kinara wa ushirikiano wa kimataifa,” amesema Guterres. “Kila mara maamuzi kuhusu Afrika na dunia yanapojadiliwa, Afrika lazima iwe mezani.”

António Guterres, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, ameketi kwenye meza ya mkutano akiwa na kipaza sauti na bendera ya Umoja wa Mataifa nyuma.

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres akizungumza na waandishi wa habari mjini Addis Ababa Ethiopia katika mkutano wa AU

Mageuzi Baraza la Usalama

Katibu Mkuu amesema kukosekana kwa uwakilishi wa kudumu wa Afrika katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa “ni jambo isilokubalika,” akisisitiza haja ya mageuzi ya haraka ya mfumo wa utawala wa kimataifa.

“Huu ni mwaka 2026 sio 1946,” amesisitiza, akimaanisha kuwa taasisi za kimataifa lazima ziakisi uhalisia wa sasa wa kisiasa na kiuchumi.

Katibu Mkuu amepongeza mchango wa Afrika katika kuunda Mkataba wa Zama Zijazo na kuimarisha ushirikiano kati ya Umoja wa Mataifa na Muungano wa Afrika, ikiwemo kupitishwa kwa Azimio namba 2719 la Baraza la Usalama, lililoweka njia ya ufadhili wa uhakika kwa operesheni za kulinda amani zinazoongozwa na AU.

Wito wa dharura wa amani barani Afrika

Amani imekuwa kipaumbele cha kwanza katika ajenda yake. Kuhusu Sudan, Guterres amezitaka pande zinazohasimiana kukubali “kusitisha mapigano mara moja na kurejea katika mazungumzo ya kufanikisha mchakato wa kisiasa unaomilikiwa na kuongozwa na Wasudan wenyewe”.

Pia amesisitiza umuhimu wa kuzuia kurejea kwa mzozo Sudan Kusini, kuimarisha mafanikio katika Jamhuri ya Afrika ya Kati CAR, na kusukuma mbele mchakato wa kisiasa unaoongozwa na Walibya kwa msaada wa Umoja wa Mataifa.

Nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo DRC, ametaka ahadi zilizotolewa ziheshimiwe “kuanza na kusitisha mapigano mara moja, huku akisisitiza haja ya juhudi za pamoja kukomesha mizunguko ya vurugu na ugaidi katika eneo la Afrika Magharibi na Sahel.”

Kuhusu Somalia, ameeleza masikitiko yake kwa kukosekana kwa muafaka katika Baraza la Usalama kuhusu ufadhili wa kudumu kwa ujumbe wa Muungano wa Afrika wa msaada na uthabiti.

“Kama ujumbe huu haukustahili msaada wa kimataifa, basi ni upi unastahili?” amehoji.

media:entermedia_image:2e0ac094-66c0-42e7-aaaf-933430481980

UNECA/Daniel Getachew

Makao Makuu ya Muungano wa Africa jijini Addis Ababa Ethiopia

Hatua za kiuchumi na haki ya kifedha

Eneo la pili la kipaumbele limekuwa hatua za kiuchumi. Guterres ameonya kuwa nchi zinazoendelea zinakabiliwa na pengo la dola trilioni 4 kila mwaka ili kufanikisha Malengo ya Maendeleo Endelevu (SDGs), huku Afrika ikipoteza fedha nyingi zaidi katika ulipaji wa madeni na mtiririko haramu wa fedha kuliko inavyopokea katika misaada.

“Lazima tuongeze mara tatu uwezo wa kukopesha wa benki za maendeleo za kimataifa,” amesema. “Tupunguze gharama na hatari za ukopaji, na tufanye mageuzi ya mfumo wa kifedha wa kimataifa ili kuhakikisha nchi zinazoendelea zinakuwa na sauti ya maana katika maamuzi.”

Pia ametaka jumuiya ya kimataifa kuchukua wajibu kamili katika kupambana na utakatishaji fedha, ukwepaji kodi na mtiririko haramu wa fedha.

Mabadiliko ya tabianchi

Kuhusu tabianchi, Katibu Mkuu amesema licha ya Afrika kuwa na asilimia 60 ya uwezo bora wa nishati ya jua duniani, inapokea asilimia mbili tu ya uwekezaji wa nishati safi duniani. Wakati huo huo, bara hilo linakabiliwa na ongezeko la joto kwa kasi zaidi kuliko wastani wa dunia licha ya kuchangia kidogo katika uzalishaji wa hewa chafuzi.

“Sayansi iko wazi dunia itazidi kiwango cha nyuzi joto 1.5 C,” amesema. “Jukumu letu la pamoja ni kuhakikisha kuzidi huko kunakuwa kidogo, kwa muda mfupi na kwa usalama.”

Ametoa wito wa kuongezwa mara tatu kwa fedha za kukabiliana na athari za tabianchi, kukusanya dola trilioni 1.3 kwa mwaka ifikapo 2035 kwa ajili ya nchi zinazoendelea, kuimarisha Mfuko wa Hasara na Uharibifu, na kuhakikisha minyororo ya thamani ya madini muhimu inakuwa ya haki na endelevu.

Amesema “Hakuna tena uporaji. Hakuna tena unyonyaji. Watu wa Afrika lazima wanufaike na rasilimali za Afrika.”

media:entermedia_image:e811f7b7-d700-435a-83fc-b7c2b5a01995

Katibu Mkuu wa UN Antonio Guterres akihutubia mkutano wa Muungano wa Afrika AU mjini Addis Ababa Ethiopia

Ushirikiano kwa mustakabali

Guterres amesisitiza kuwa uongozi na mshikamano wa Afrika umeunda dhamira yake kama Katibu Mkuu katika kila hatua.

Ameahidi kuendeleza ushirikiano uliojengwa juu ya heshima, mazungumzo endelevu na mshikamano usiotetereka.

“Tusonge mbele,” almehimiza, “kuimarisha ushirikiano wetu kwa ajili ya amani, maendeleo endelevu na haki za binadamu kwa Afrika na dunia yetu.”

Hii si kwaheri.

Wakati António Guterres anakaribia kumaliza muda wake wa uongozi mwishoni mwa mwaka huu, amehitimisha hotuba yake katika Mkutano wa Muungano wa Afrika kwa ujumbe ulio wazi

“Wapo wanaoeleza kuwa uwepo wangu hapa leo ni wa kuaga, lakini si kweli. Nawahakikishia kwamba, hadi dakika ya mwisho ya mamlaka yangu, Afrika itaendelea kuwa kipaumbele cha kwanza cha Umoja wa Mataifa katika shughuli zangu zote.”

Ameongeza kuwa ushirikiano kati ya Muungano wa Afrika na Umoja wa Mataifa utakuwa ushirikiano wetu wa kimkakati wa kina zaidi. 

“Baada ya tarehe 31 Desemba, nawathibitishia kwamba Afrika itaendelea kuwa moyoni mwa fikra zangu na mshikamano wangu wa dhati popote nitakapokuwa na popote nitakapofanya kazi.”

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *