Kilio kikubwa tangu nchi yetu iingie katika mfumo wa Vyama Vingi vya Siasa ni Katiba mpya, lakini kwa hali ya mgawanyiko tulionao kama taifa, hata kama Serikali itaanzisha mchakato huo, bado tunaweza tukwame kama mwaka 2014.

Kwanini tulikwama?, ni kwa sababu tuliingia katika Bunge Maalum la Katiba (BMK) tukiwa hatuna maridhiano ya kitaifa hivyo hata kama Katiba Inayopendekezwa ingeenda hatua ya kupigiwa kura, kura za Hapana pengine zingekuwa nyingi.

Awali alipounda Tume ya Mabadiliko ya Katiba chini ya Jaji Joseph Sinde Warioba, Rais wa awamu ya nne, Jakaya Kikwete alijiwekea ahadi ya kuwaachia watanzania kumbukumbu inayoishi (legacy), lakini ndoto yake iliyeyuka mithili ya barafu.

Tume ya Jaji Warioba ilifanya kazi nzuri sana na ya kutukuka, ikazunguka nchi zima kupata maoni ya watanzania ya nini kiwemo katika Katiba mpya na nini kisiwemo, lakini sote ni mashahidi, namna BMK lilivyogawanyika kwa maslahi ya kisiasa.

Ni kutokana na wajumbe waliotokana na Chama cha Mapinduzi (CCM) ambao walikuwa ndio wengi,kuyakataa na kuondoa maoni ya wananchi walio wengi katika Katiba ya Jaji Warioba, mchakato ule haukuwa tena na maridhiano.

Katika Katiba ya Jaji Warioba, wananchi walipendekeza kupunguzwa kwa madaraka makubwa ya Rais hasa ya uteuzi wa viongozi na watendaji yapunguzwe na ziundwe Taasisi za kikatiba za kumshauri Rais kabla hajafanya teuzi.

Pia wananchi walitaka Katiba inayotendanisha Mamlaka ya Mihimili ya Dola na walipendekeza Bunge liwe na uhuru zaidi katika kuisimamia, kuiwajibisha na kuishauri Serikali na kuitenganisha serikali na Bunge, hali ambayo iko sasa.

Rasimu hiyo ilizuia Waziri, Naibu Waziri, Mbunge au mtu mwenye madaraka ya aina nyingine yoyote yatakayotajwa na sheria za nchi, hataweza kuchaguliwa kuwa Spika na ililenga kulifanya Bunge kuwa huru zaidi na lisiwe sehemu ya Serikali.

Lakini rasimu ya Katiba ya Jaji Warioba, iliwapa wapiga kura uwezo wa kuwawajibisha Wabunge kwa kupiga kura ya kutokuwa na imani nao wakati wowote (Recall Powers) kama wakienda kinyume na maslahi ya wananchi hao.

Rasimu hiyo iliweka sifa ya mtu kuchaguliwa kuwa mbunge kuwa ni pamoja na mtu huyo kujua kusoma na kuandika lugha ya Kiswahili au Kiingereza na ana elimu isiyopungua kidato cha nne tofauti na sifa ya kujua kusoma na kuandika.

Kubwa zaidi iliweka muundo wa Serikali tatu, ambao kwa maoni ya watanzania muundo huo ndio ungejibu changamoto nyingi za muundo wa sasa na hili pengine lingeondoa mtizamo hasi Mzanzibar anapoteuliwa katika Serikali ya Bara.

Hayo ni machache kati ya mengi mazuri yaliyokuwepo katika rasimu ya Jaji Warioba, lakini yaliondolewa kutokana na kutokuwepo kwa maridhiano ya kitaifa, na CCM kuweka mbele zaidi maslahi yake ya kisiasa katika kushika dola.

Katiba hii ingezaa Tume Huru ya Uchaguzi kwa sifa na muundo wake, lakini maoni hayo yalipigwa chini na ukidodosa sana utakugundua kuwa hilo lilifanyika kwa hofu tu kuwa ujio wa Katiba mpya ungeiondoa CCM katika sanduku la kura.

Kwa hiyo hofu hiyo na mchanganyiko wa mgawanyiko wa wananchi kati ya wale waliotaka Rasimu ya Jaji Warioba na wale waliotaka Katiba Inayopendekezwa, ni dhahiri na hata serikali inajua, Katiba inayopendekezwa isingepata kura nyingi.

Sasa mazingira yaliyofanya Katiba Inayopendekezwa isiende kupigiwa kura, ndio hayo hayo tutakutana nayo wakati Serikali ya CCM itakaporejesha mchakato wa Katiba mpya kutokana na mazingira ya chuki, uhasama na visasi yaliyopo sasa.

Wala tusitafute mchawi nini kimetufikisha hapa kwani kilio cha Katiba mpya kimedumu zaidi ya miaka 30 sasa, utendaji usioridhisha wa Jeshi la Polisi, utekaji, kupotea kwa watu na wengine kuuawa, ndio kiini cha chuki hizi zilizopo.

Lakini hakuna ambaye atasema mazingira ya siasa za upinzani Tanzania yanafanyika kwa mujibu wa Katiba na Sheria za Nchi, yeyote utakayemuuliza atakuambia baadhi ya vyama vya upinzani na viongozi wake hawatendewi haki.

Kubwa zaidi ni yale yaliyotokea Oktoba 29,2025 na siku zilizofuata ambapo ghasia zimesababisha vifo, majeruhi na kuharibiwa kwa mali na wengine hadi leo hawajapata miili ya ndugu zao, katika mazingira haya tutavukaje hapo?

Ninaipongeza na kuishukuru Serikali ya awamu ya sita chini ya Rais Samia Suluhu Hassan na chama chake cha CCM kwa dhamira yake ya kuleta maridhiano.

Tusiridhiane kinafiki huku tumeficha mapanga nyuma, maridhiano yawe na sifa na vigezo vyote kwamba ukweli usemwe, pale ambako Serikali na vyombo vyake iliteleza iombe radhi, tulipe fidia na wa kuwajibishwa, wawajibishwe. Baada ya kufanya hivyo, ndiyo twende kwenye mchakato wa Katiba mpya.

Daniel Mjema ni mwandishi wa habari na mwanafunzi wa Shahada ya Uzamivu (PhD) katika Mawasiliano ya Umma, Chuo Kikuu Huria cha Tanzania. 0656600900

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *