Zanzibar: Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, kupitia Wizara ya Utalii na Mambo ya Kale pamoja na Wizara ya Kazi na Uwekezaji, imesaini makubaliano ya Ushirikiano kati ya Sekta ya Umma na Sekta Binafsi (PPP) na Infinity Developments kwa lengo la kurejesha na kuhuisha baadhi ya maeneo muhimu ya kihistoria na urithi wa Zanzibar.
Makubaliano haya yanaashiria mwanzo mpya wa maendeleo ya kiutamaduni na kiuchumi Zanzibar, yakiiweka hifadhi ya urithi kuwa nguzo kuu ya kukuza utalii endelevu.
Mpango wa marejesho utazingatia maeneo muhimu yaliyopo ndani ya Tovuti ya Urithi wa Dunia ya UNESCO ya Mji Mkongwe (Stone Town), ikiwemo: Ngome Kongwe (Old Fort), Makumbusho ya Mahakama Kuu (High Court Museum) na Hamam za Hamamni.
Maeneo mengine ni pamoja na Hamam za Forodhani, Hamam za Kidichi na Hamam za Kizimbani.

Kupitia Mpango wake wa Infinity Culture Program, Infinity Developments imejitolea kuwekeza takribani Dola za Kimarekani milioni 12 kwa awamu ya kwanza ya marejesho, uboreshaji wa miundombinu, kazi za uhifadhi pamoja na kuboresha uzoefu wa wageni.
Akizungumza katika hafla ya utiaji saini, Dk Aboud Suleiman Jumbe, Katibu Mkuu wa Wizara ya Utalii na Mambo ya Kale, alieleza kuwa ushirikiano huo ni hatua muhimu katika mustakabali wa urithi wa Zanzibar.
“Ushirikiano huu unaonesha nguvu ya sekta ya umma na sekta binafsi katika kulinda utambulisho wetu wa kiutamaduni huku tukitekeleza dira ya Mheshimiwa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Hussein Ali Mwinyi, ya kuharakisha mageuzi ya sekta ya utalii na urithi wa mambo ya kale kwa ajili ya ukuaji wa uchumi na maendeleo ya kijamii,” alisema.
SOMA: Mapinduzi sekta makazi mradi wa dola mil 250 ukizinduliwa Zanzibar
Naye Bw. Khamis Suleiman Mwalimu, Katibu Mkuu wa Wizara ya Kazi na Uwekezaji, alisisitiza kuwa makubaliano hayo yanaakisi dhamira ya Zanzibar ya kuweka mazingira ya wazi na yenye usawa kwa wawekezaji wa sekta binafsi, na hivyo kufungua fursa mpya za ajira, ujasiriamali na ukuaji wa uchumi endelevu.
Kwa upande wake, Nduhu Samuel Saba, Mkurugenzi Mtendaji na Mwenyekiti wa Infinity Developments, alisema:
“Zanzibar ina historia ya kipekee na ya kuvutia katika ukanda huu. Tunajivunia kushirikiana na Serikali katika kulinda na kuinua maeneo haya ya kihistoria. Uwekezaji huu sio tu wa kurejesha majengo, bali ni wa kuunda maeneo hai ya kitamaduni yatakayochochea elimu, utalii na fahari ya jamii kwa vizazi vijavyo.”
Mpango huu ni miongoni mwa uwekezaji mkubwa zaidi wa aina ya PPP katika sekta ya urithi katika historia ya karibuni ya Zanzibar, na unaimarisha nafasi ya uhifadhi wa urithi kama nguzo kuu ya mkakati wa utalii na maendeleo ya muda mrefu ya Zanzibar.