Maswali mengi yamekuwa yakigota kwenye utajiri wa mtuhumiwa wa uhalifu wa ngono kwa watoto wadogo, Jeffrey Epstein. Je, ilikuwaje mwalimu aliyefukuzwa kazi kwa kubainika alidanganya wasifu wake wa kielimu, akawa mfanyakazi wa benki, ndani ya miaka michache akaibuka kuwa bilionea?

Utata huo wa utajiri wa Epstein, ndiyo ulisababisha wajumbe wa Baraza la Wawakilishi Marekani, wajifungie na bilionea Leslie “Les” Wexner, na kumtwisha mzigo wa maswali. Mkutano huo ulifanyika nyumbani kwa Wexner, Ohio, Jumatano (Februari 18, 2026).

Bilionea Wexner ndiye alikuwa chemchemi ya utajiri wa Epstein. Angalau hili linatosheleza. Swali kuhusu kwa nini Wexner alimpa nafasi Epstein ya kutajirika kwa kiasi kikubwa? Hilo halijapata majibu. Wexner hafafanui, zaidi ya kujuta kumfahamu Epstein.

Wajumbe watano wa Kamati ya Baraza la Wawakilishi ya Usimamizi na Marekebisho ya Serikali, walimweka kikaangoni Wexner, baada ya jina lake kutokeza mara nyingi, katika nyaraka zenye kurasa milioni tatu kutoka kwenye Mafaili ya Epstein, zilizoachiwa na Wizara ya Haki Marekani (DOJ), Januari 30, 2026.

Katika nyaraka zilizohaririwa na ambazo hazijahaririwa kutoka kwenye Mafaili ya Epstein, bilionea Wexner, emepamba kurasa nyingi kila upande. Dhahiri, kwa kila hatua ambayo Epstein aliipiga na kuifikia kimaisha, utajiri na nguvu kubwa ya ushawishi kijamii, ngazi yake kuu ilikuwa Wexner.

Baada ya Epstein kuaminiwa na Wexner, na kufanywa msimamizi wa mali za bilionea huyo, ikiwemo kuwa mjumbe wa bodi ya wadhamini wa Taasisi ya Wexner, mhalifu huyo alijiweka karibu na watu mashuhuri ulimwenguni, hasa matajiri wakubwa na wanasiasa. Hadhi aliyopewa na Wexner ilimfanya aaminike.

Wexner alikutana vipi na Epstein? Jibu la swali hilo ni benki ya Bear Stearns. Epstein akiwa anafundisha Shule ya Dalton, iliyopo Manhattan, New York, alijenga ukaribu na baadhi ya wazazi wa wanafunzi aliowafundisha. Mmoja wa wazazi ni Alan “Ace” Greenberg aliyekuwa Mkurugenzi Mtendaji wa Bears and Stearns.

Sifa moja ya Epstein ni uwezo wake wa kujenga uhusiano na watu kwa haraka na kuaminika. Sifa nyingine ya Epstein ilikuwa uwezo wake wa kucheza na namba. Alikuwa na umahiri mkubwa katika somo la hisabati. Alikuwa hivyo tangu anasoma, wanafunzi wenzake walimtegemea awafundishe katika muda wa ziada. Aliendelea hivyo akiwa mwalimu, wanafunzi walimpenda na kumtumainia.

Sifa za Epstein zilipomfikia Greenberg, kisha wakafahamiana, ukafuata urafiki. Epstein alipofukuzwa kazi Shule ya Dalton, Greenberg alimpa ajira kama ofisa wa chini, benki ya Bears and Stearns. Haraka sana, Epstein alianza kupanda ngazi haraka. Uwezo wake uliwavutia viongozi. Hatimaye, Epstein alikabidhiwa kitengo cha kushughulika na akaunti za matajiri wakubwa, na zile taasisi zenye ukwasi.

Nafasi hii ya kushughulika na akaunti za matajiri wakubwa, Epstein hakuichezea. Aliitumia ipasavyo kutimiza malengo yake ya kifedha kwa kujenga ukaribu na matajiri, hasa mabilionea. Alijinasibu na kuaminika kama mshauri wa fedha na kodi. Alijitengeneza na kukubalika kama mlinda usalama wa mali ili kutoibiwa, kutopotea, au kutofilisika.

Mwaka 1986, Epsteine alikutana na Wexner. Miaka mitano baadaye, bilionea huyo wa biashara za rejareja alisaini kiapo kumpa mamlaka Epstein, ya usimamizi wa mali zake. Yalikuwa mamlaka ya kushangza kwa mmiliki kumpa mtu mwingine. Tena mtu baki. Nguvu ya kisheria ambayo Epstein alipewa na Wexner kwenye mali zake, yalimruhusu kusaini hundi, kuajiri na kufukuza wafanyakazi, kukopa fedha, kununua au kuuza mali yoyote, kwa niaba ya Wexner.

Nguvu hizo ambazo Epstein alikuwa nazo kufanya chochote alichotaka kwenye mali za Wexner, ndizo zinatafutiwa maelezo. Wexner hafunguki, zaidi ya utetezi ambao ameshautoa, akidai alikuwa mjinga, mpumbavu, na rahisi kudanganyika, ndiyo maana alimwamini Epstein, hadi kumpa nguvu kubwa ya usimamizi wa mali zake.

“Epstein alikuwa tapeli. Alinitapeli,” ndivyo Wexner anavyojitetea. “Na kipindi chote nilichokuwa natapeliwa, sikuwahi kutenda kosa lolote. Mimi ni mwathirika wa utapeli wa Epstein. Ukweli unasimama hivyo, na sina kitu cha kuficha. Alitoa fedha nyingi bila idhini kwenye akaunti yangu, na alifanya hivyo hivyo katika akaunti ya familia yangu.”

Utetezi huo wa Wexner ni kujaribu kujitenga na nadharia ndani ya mapendekezo ya kijamii kuwa alimpa nguvu ya kisheria Epstein kwenye mali zake, baada ya mhalifu huyo wa ngono kwa watoto wadogo, kumtegea msichana mdogo (au wasichana kadhaa), kisha akamrekodi, baada ya hapo alimgeuza mateka na kumwendesha alivyotaka.

Sehemu ya nyaraka za Mafaili ya Epstein, iliyotolewa Januari 30, 2026, imeonyesha rekodi za makubaliano ya ununuzi na uuzaji, pamoja na hati ya kisheria ya ahadi ya malipo na dhamana, vilevile maelezo wa uhamishaji wa mali baina ya Epstein na Wexner. Nyaraka zimeonyesha pia uhamishaji tata wa hatimiliki ya jumba la Wexner, lililopo Manhattan, kwenda kwa Epstein.

Mwamala wa ununuzi wa jengo hilo, unasoma Dola za Marekani 10 milioni. Kiasi hicho cha fedha kinaweza kuongeza kwa kupima hali ya mfumuko wa bei. Kwa mujibu wa Benki ya Kuu ya Marekani (The Fed), kwa viashiria vya mfumuko wa bei, dola 10 milioni ya mwaka 1998, inaweza kununua bidhaa za dola 19.88 milioni (Sh51.7 bilioni) mwaka 2026.

Jumba hilo siyo tu likawa ngome kuu ya Epstein, New York, bali pia alama ya ukuaji wa mhalifu huyo. Ghafla, Epstein akawa anaonekana mwenye hadhi kubwa, na alizidi kuaminiwa na matajiri, maana naye alionekana mwenye nazo. Mtu wa maisha ya kubangaiza asingeweza kumiliki jumba hilo lililopo Mtaa wa 9 East 71st.

Taasisi ya Wexner hutoa misaada ya kijamii. Nafasi ya Epstein kuwa mdhamini kwenye Taasisi ya Wexner, vilevile akiwa na nafasi ya kufanya uamuzi wa kibiashara, kwa pamoja vilimpa hadhi kubwa. Viongozi wengi mashuhuri waliuingia mtego. Walijikuta wakijenga ukaribu na mhalifu huyo, ambaye naye hakufanya ajizi katika kuwatumia ili kukuza mtandao wake.

Katika kujijenga zaidi, Epstein alianza kujiita “mfadhili”. Akitumia nguvu aliyonayo kwenye Taasisi ya Wexner, Epstein aliweza kutoa misaada ya kijamii na kujinasibu ilitoka kwake, wakati kila kitu kilitoka kwa Wexner. Jina la Epstein na namba zake za mawasiliano pamoja na barua pepe, vilikuwa kwenye kitabu cha kumbukumbu cha kila tajiri Marekani, vilevile wanasiasa wa ndani na nje ya Marekani.

Mmoja wa viongozi wakubwa waliongia kwenye 18 za Epstein ni Ehud Barak, ambaye alikuwa Waziri Mkuu wa Israel, kati ya mwaka 1999 na 2001. Barak alitambulishwa kwa Epstein na Rais wa zamani wa Israel, Shimon Perez, katika hafla moja kubwa iliyofanyika Washington DC, Marekani, mwaka 2003.

Mpaka unaona kuwa Epstein alikuwa na nguvu kiasi gani. Rais mstaafu ndiye alimtambulisha Epstein kwa Barak (Waziri Mkuu mstaafu). Kisha, kati ya mwaka 2004 na 2006, Barak alipokea Dola 2.3 milioni (Sh6 bilioni), kutoka Taasisi ya Wexner. Maana yake, nguvu ambayo Wexner alimpa Epstein, ilimfanya mhalafu huyo ajipambanue kama mtu mwafaka kufuatwa kwa aliyehitaji msaada kutoka Taasisi ya Wexner.

Inaendelea kesho.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *