Uhusiano baina ya mhalifu wa ngono kwa mabinti wadogo, Jeffrey Epstein na Waziri Mkuu wa zamani wa Israel, Ehud Barak, hauishii kwenye misaada.

Lipo jambo lingine ambalo limeibuliwa kwenye nyaraka zilizopo kwenye Mafaili ya Epstein, kama yalivyoachiwa Januari 30, 2026, na Wizara ya Haki Marekani (DOJ).

Barak alikuwa Waziri Mkuu wa Israel kati ya mwaka 1999 na 2001. Kipindi akiwa Waziri Mkuu, alikuwa pia Waziri wa Ulinzi.

Mwaka 2007 hadi 2013, Barak aliwahi kufanya kazi kama Waziri wa Ulinzi chini ya mawaziri wakuu wawili, Ehud Olmert na Benjamin Netanyahu. Novemba 22, 1995 hadi Juni 18, 1996, Barak alikuwa Waziri wa Mambo ya Nje, chini ya Waziri Mkuu, Shimon Perez.

Barak, alishakuwa Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi ya Israel (Tzahal). Pamoja na unyeti wa nafasi alizowahi kushika, nyaraka zimeonyesha kuwa Barak alianguka dhambini, na aliingia moja kwa moja kwenye mnyororo wa waliopokea zawadi ya mapenzi kutoka kwa mabinti wadogo, ambayo alipewa na Epstein.

Taarifa za ushahidi wa mahakamani, ambazo zimetolewa na DOJ, kutoka kwenye Mafaili ya Epstein, zimeonyesha malalamiko ya mwanamke, Virginia Giuffre, akilalamika mahakamani kwamba Barak ni mmoja wa watu mashuhuri, ambao alisafirishwa na kupewa maagizo ya kwenda kuwahudumia masaji na kutenda nao ngono.

Virginia, alikuwa binti mwenye umri wa miaka 16, alipochukuliwa kwa ajili ya kutoa huduma ya masaji na ngono kwenye makasri ya Epstein. Baadaye aliacha kazi na kuolewa alipopelekwa Thailand kusomea zaidi taaluma ya masaji. Alikwenda kuishi Australia na mume wake ili kukwepa kutekwa na Epstein au hata kuua.

Idara ya Upelelezi Marekani (FBI), ndiyo waliomtafuta Virginia na kumfikia ili asaidie kupatikana kwa ushahidi wa kumtia hatiani Epstein na washirika wake. Virginia alikubali kujitoa na kugeuka mtetezi wa waathirika wengine wa uhalifu wa Epstein na genge lake.

Hata hivyo, Aprili 25, 2025, Virginia alikutwa amefariki dunia nyumbani kwake, Neergabby, Jimbo la Western Australia, nchini Australia.

Ripoti ya madaktari ilieleza kuwa Virginia alijiua. Familia, hasa baba mzazi wa Virginia, alipingana na taarifa hiyo, akieleza kuwa mwanaye hakuwa na sababu yoyote ya kujiua.

Nadharia kubwa ya kifo cha Giuffre ni kwamba aliuawa na watu wenye nguvu ili asitoe siri zao, za ushirika wao na Epstein.

Katika mahojiano aliyoyafanya na mwandishi Pierse Morgan, Mei mosi, 2025, baba wa Virginia, Sky Roberts, alisema anaamini kuna mtu amemuua mwanaye.

Aliongeza kuwa kitu pekee ambacho kitasaidia ukweli ujulikane ni uchunguzi wa kina, akabainisha kwamba kwa imani yake, muda utaweka kila kitu bayana kuhusu kifo cha binti yake.

Mazingira ya kifo cha Virginia, na siri kubwa ambayo alikuwa akitembea nayo, jumlisha vifo vya wengine ambavyo navyo bado vimeacha mashaka, hasa kifo cha  Jean-Luc Brunel, ambaye naye ilielezwa amejiua, kama ilivyo kwa Epstein mwenyewe.

Brunel, ndiye alikuwa akiwaandaa na kuwatengeneza watoto wa kike ili wawe tayari kutoa huduma ya ngono kwa watu mashuhuri, hasa matajiri.

Sasa, nyaraka zimeonyesha kuwa Barak, alihusika moja kwa moja na mabinti wadogo kutoka kwa Epstein. Hata hivyo, Februari (mwezi huu), Barak alifanya mahojiano na televisheni ya Israel, Channel 12, na kueleza kwamba hakuwahi kufahamu uhalifu wa Eptein, na kwamba anajuta kukutana naye na kujenga naye mawasiliano.

Kila ambaye anatajwa kwenye Mafaili ya Epstein, hapingi kufahamiana naye, isipokuwa utetezi wake unajielekeza kwenye kutofahamu uhalifu aliokuwa anautenda.

Kama Barak, ndivyo hata bilionea Leslie Wexner, ambaye ushahidi wote umedhihirisha kuwa nguvu kubwa ya Epstein kutajirika na kuwa mtu mwenye ushawishi ulimwenguni, ilitoka kwake.

Hata Wexner naye alisema anajuta kumwamini Epstein, kisha akamwita tapeli. Ukirejea nyaraka za Mafaili ya Epstein, unakutana na hari ya mahakamani, ambayo ina maelezo ya Virginia akisimulia alivyopelekwa na Epstein kwa Wexner, kwa ajili ya kumhudumia masaji bilionea huyo na kufanya naye ngono. Bahati mbaya, Virginia hayupo duniani.

Barak naye alisema hakuwa akifahamu uhalifu wa Epstein. Hata hivyo, Juni 30, 2008, Epstein alihukumiwa kwenda jela miezi 18, baada ya kukiri makosa ya uhalifu wa kingono kwa mabinti.

Hukumu hiyo ilikuwa habari ya dunia kwa sababu makosa yake yalistahili kifungo cha maisha, lakini akapewa “dili”, ambalo wengi waliona lilijaa upendeleo.

Nyaraka za kwenye Mafaili ya Epstein, zimeonyesha kuwa Oktoba 2014, yaani miaka sita na miezi minne tangu Epstein alipokutwa na hatia ya uhalifu wa kingono kwa mabinti wadogo, mke wa Barak, Nili Priel Barak, alimwandikia baruapepe Epstein, kumjulisha kuhusu mipango ya safari ya New York.

Nili, alimweleza Epstein tarehe ambayo Barak angekuwepo New York, na kumuuliza kama angepata muda wa kuonana naye. Wawili hao (Nili na Epstein), waliendelea kuwasiliana kwa barua pepe.

Halafu, kuna ujumbe wa sauti wa Barak, akimweleza Epstein kuwa alipokuwa Waziri wa Ulinzi alikutana na Rais wa 44 wa Marekani, Barack Obama, zaidi ya mara moja na walibishana kuhusu suluhu ya nchi moja au mbili Mashariki ya Kati (mgogoro wa Israel na Palestina).

Mwaka 2015, Epstein aliwekeza kwenye kampuni ya kiteknolojia ya Israel, iliyokuwa inaitwa Reporty Homeland Security, siku hizi Carbyne na mwenyekiti wa kampuni hiyo akawa Barak.

Nyaraka pia zinaonesha kuwa kati ya mwaka 2012 na 2014, Epstein alimsaidia Barak kwa kumuunganisha na viongozi wa Kiafrika wenye nguvu.

Kila kitu kipo dhahiri kwamba uhusiano baina ya Epstein na Barak ulikuwa mkubwa hata baada ya mhalifu huyo kukiri kosa makosa na kutiwa hatia.

Utetezi wa Barak kuwa hakujua matendo ya Epstein, yanatafsiriwa na wengine kama asili ya binadamu, kwamba hata abananishwe vipi, atatafuta upenyo wa kujiokoa.

“Nawajibika kwa matendo yangu yote na uamuzi. Kuna chumba cha kuhoji endapo nilitakiwa kufanya uchunguzi zaidi wa kina. Nasikitika sikufanya hivyo,” alijitetea Barak akiwa Channel 12, Februari 2026. Utetezi wake unapingwa na wengi, Marekani na Israel, na presha ni kubwa kutaka ashtakiwe ili haki itendeke.

Oktoba 21, 2025, kitabu cha maisha ya Virginia, “Nobody’s Girl: A Memoir of Surviving Abuse and Fighting for Justice” – “Msichana asiye wa yeyote: Kumbukumbu Binafsi za Kunusurika Ukatili na Kupambana kwa ajili ya Haki.” Kitabu hicho, Virginia alikiandika kwa kushirikiana na mwandishi Amy Wallace. Kilitoka takriban miezi miezi sita baada ya kifo cha Virginia.

Ndani ya kitabu hicho, Virginia anasimulia kuhusu jinsi alivyobakwa na waziri mkuu mashuhuri.

Kutaja waziri mkuu mashuhuri hakumfanyi Barak moja kwa moja kuwa ndiye mlengwa, maana wapo mawaziri wakuu wengine wametajwa kwenye Mafaili ya Epstein.

Waziri Mkuu wa UK (mwaka 2007 – 2010), Gordon Brown na Waziri Mkuu wa Norway (mwaka 1996 – 1997), Thorbjørn Jagland, nao wametajwa.

Je, ni yupi ambaye Virginia amesema ni waziri mkuu mashuhuri aliyembaka? Nyongeza kuhusu Barak ni nyaraka za mahakamani, ambako Virginia amemtaja. Brown bado hajaguswa, licha ya kutajwa kwenye Mafaili ya Epstein. Jagland, ameshafunguliwa mashitaka.

Itaendelea kesho

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *