Dar/Mikoani. Kwa muda wa saa tisa, Ligi Kuu ya NBC leo itakuwa katika hisia za maelfu ya mashabiki wa soka nchini wakati timu nane zitakapokabiliana katika muda, viwanja na miji tofauti, kila moja ikisaka matokeo mazuri ambayo yataiweka pazuri kwenye msimamo wa ligi.

Matokeo ya ushindi yanaweza kuendelea kuziweka baadhi kwenye mbio za ubingwa na kwa nyingine kuziondoa katika nafasi za chini kwenye msimamo wa ligi lakini kupoteza au sare kutaziweka katika mazingira magumu timu ambazo zitapata matokeo hayo huku hapana shaka zikizipa furaha timu pinzani.

Mchezo wa kwanza leo utakuwa katika Uwanja wa Jamhuri Dodoma kuanzia saa 8:00 mchana ukizikutanisha Mtibwa Sugar ambayo itaikaribisha Singida Black Stars.

Mtibwa Sugar iliyopo nafasi ya nne ikiwa na pointi 21, imekuwa na matokeo mazuri tangu ianze kufundishwa na Kocha Yusuf Chipo. Ambapo kabla ya kufungwa mabao 3-1 nyumbani na Mashujaa, ilicheza mechi nane ikishinda nne na sare nne.

Singida Black Stars iliyo nafasi ya 13 na pointi zake 12 ilizokusanya kwenye mechi nane ilizocheza, ina fursa nzuri ya kupanda juu endapo ikishinda leo itafikisha pointi 15 na itapanda hadi nafasi ya kumi.

Baada ya hapo, kuanzia saa 10:15 jioni, KMC itakuwa nyumbani kuikaribisha Azam FC kwenye Uwanja wa KMC Complex.

Ni mechi iliyokaa kimtego kwa Kocha wa KMC, Abdallah Mohamed ‘Bares’ ambaye tangu amekabidhiwa mikoba ya kuiongoza timu hiyo kutoka kwa Marcio Maximo, ameshinda mechi moja pekee kati ya sita, ambapo imepata sare moja na vipigo vinne.

Azam iliyo nafasi ya tisa na pointi 16, ikishinda leo inaweza kupanda hadi nafasi ya saba lakini itatakiwa kuiombea Simba ipoteze mechi yake ya leo.

Kocha Msaidizi wa Azam, Addis Worku, alisema: “Tunakwenda kwa kuheshimu mchezo bila kujali kiwango wala matokeo ya wapinzani wetu. Lazima tuwe na tahadhari kucheza na mpinzani aina ya KMC kulingana na hali yao, kwani wanataka kurudi katika njia nzuri ya ushindi, hivyo lazima tuwe makini.”

Mabingwa watetezi wa Ligi Kuu Bara, Yanga watakuwa Uwanja wa Majaliwa pale Lindi kucheza na wenyeji wao Namungo kuanzia saa 1:00 usiku.

Ni mechi ambayo Yanga inaingia ikiwa na rekodi nzuri dhidi ya mpinzani wake huyo kwani tangu 2020-2021, timu hizo zimekutana mara 12 katika Ligi Kuu ambapo Yanga imeshinda mechi saba mfululizo, sare ni tano na Namungo haijaonja ushindi.

Katika msimamo, Namungo ni ya tano ikiwa na pointi 20 ikicheza mechi 14, imeshinda tano sawa na sare, ikipoteza nne. Ushindi kwao leo utaifanya kufikisha pointi 23 na kuishusha Yanga yenye 22 na mechi nane.

Siku itahitimishwa kwa mechi ya Tanzania Prisons dhidi ya Simba kuanzia saa 3:00 usiku kwenye Uwanja wa Jamhuri, Dodoma.

Tanzania Prisons inajitafuta bado kwani licha ya kushinda mechi mbili mfululizo hivi karibuni dhidi ya Namungo katika Ligi na Kombe la Shirikisho (FA) mbele ya Moro Kids.

Ushindi kwa Simba leo unaweza kuitoa katika nafasi ya saba hadi ya nne kwani itafikisha 22 lakini hilo litatokea iwapo Mtibwa Sugar itaangusha pointi kwa Singida Black Stars.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *