
MSHAMBULIAJI wa maafande wa JKT Tanzania, Paul Peter Kasunda, ameichezea timu hiyo dakika 1326 za mashindano yote hadi sasa, huku akiwa na rekodi bora, ikiwa ni msimu wa kwanza tu na kikosi hicho tangu ajiunge nacho akitokea Dodoma Jiji.
Katika dakika 1326 hizo, dakika 1253 ni za Ligi Kuu ambazo amecheza mechi 16 na kati ya hizo nyota huyo amechangia mabao saba, baada ya kufunga matano na kuasisti mawili, huku akichaguliwa mchezaji bora wa mechi mara tatu kwa msimu huu.
Kwa dakika 73, zilizobakia ambazo kwa ujumla zinakuwa 1326, ni za Kombe la Shirikisho, alizocheza mechi moja tu ya hatua ya 64 bora, huku nyota huyo akiendeleza kiwango bora, baada ya kufunga mabao manne katika ushindi wa timu hiyo wa 7-0.
Mshambuliaji huyo alifungia mabao manne wakati kikosi hicho cha maafande kiliposhinda mabao 7-0, dhidi ya mabingwa wa Ligi Kuu Bara mwaka 1982, Pan Africans, huku Edward Songo akifunga mawili na jingine moja likifungwa na Karimu Mfaume.
Paul Peter aliyeanzia timu ya vijana ya Azam chini ya miaka 20, hadi kupandishwa kuchezea ya wakubwa, amekuwa ni muhimili mkubwa kwa kikosi hicho cha maafande msimu huu, akishirikiana na nyota, Valentino Mashaka na Salehe Karabaka.
Mshambuliaji huyo aliyepandishwa kuichezea Azam na aliyekuwa kocha wa kikosi hicho, Mromania Aristica Cioaba, amechezea pia timu mbalimbali zikiwamo za Mugabe FC, KMC FC, maafande wa Tanzania Prisons na msimu uliopita alikuwa Dodoma Jiji.
Nyota huyo alijiunga na JKT Tanzania Julai 9, 2025, akitokea Dodoma Jiji, baada ya msimu wa 2024-2025, kufunga mabao manane ya Ligi Kuu Tanzania Bara, akiwa nafasi ya pili kwa wachezaji wazawa waliofunga mabao mengi, nyuma ya Clement Mzize wa Yanga aliyefunga 14.