UJENZI wa mradi wa kuzalisha umeme kwa nishati ya jua Kishapu mkoani Shinyanga umekamilika. Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO), Lazaro Twange amesema kukamilika kwa mradi huo ni ushahidi wa dhamira ya Serikali ya Awamu ya Sita kuimarisha upatikanaji wa huduma ya umeme ya uhakika kwa Watanzania.
“Hii ni historia mpya imeandikwa kwa nchi yetu.Tangu tupate uhuru hatujawahi kuwa na mradi mkubwa wa aina hii wa umeme wa jua. Serikali kupitia Wizara ya Nishati na Tanesco imeandika historia na leo (juzi) mmeshuhudia hapa umeme ukizalishwa,” alisema.
Amesema Machi Mosi mwaka huu megawati 50 zitakuwa zimeunganishwa kwenye Gridi ya Taifa. Twange amemshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuwezesha upatikanaji wa Sh bilioni 118.6 kwa ushirikiano na Benki ya Maendeleo ya Ufaransa (AFD), fedha zilizowezesha utekelezaji wa awamu ya kwanza ya mradi huo. Mkuu wa Wilaya ya Kishapu, Peter Masindi alisema mradi huo ni kichocheo cha ukuaji wa uchumi wa eneo hilo hasa kwa vijana wanaojishughulisha na uchimbaji wa madini na shughuli za kilimo.
“Mradi huu umeleta ajira kwa wananchi wetu na umefungua ukurasa mpya wa maendeleo. Umeme wa uhakika utaongeza tija katika sekta za madini na kilimo na kuchochea shughuli za kiuchumi na kijamii kwa wakazi wa Kishapu,” alisema Masindi. SOMA: Visiwa Ziwa Victoria vitakavyofaidi ushirikiano nishati safi
Kaimu Meneja wa Kituo cha Kuzalisha Umeme Kishapu, Mariana Mrosso amesema kituo hicho kitaimarisha uthabiti wa Gridi ya Taifa na kuboresha ubora wa upatikanaji wa umeme hususani kwa wateja wa maeneo ya mikoa ya Kanda ya Ziwa. “Umeme unaozalishwa hapa utaongeza uwezo wa uzalishaji kwenye Gridi ya Taifa na kuboresha ufanisi wa huduma kwa wateja wetu hasa katika mikoa ya Kanda ya Ziwa,” alisema Mrosso.

Wakati huohuo Tanesco ipo katika hatua za mwisho za kumpata mkandarasi kwa ajili ya utekelezaji wa awamu ya pili ya mradi huo itakayozalisha megawati 100 kwa gharama ya Sh bilioni 200.4. Mradi wa umeme wa jua Kishapu unatajwa kuwa alama ya mabadiliko na hatua muhimu katika mwelekeo wa Tanzania kutumia nishati jadidifu katika uzalishaji wa umeme.
Taarifa ya Wizara ya Nishati inaeleza mradi wa umeme jua unaotekelezwa wilayani Kishapu mkoani Shinyanga utazalisha megawati 150 za umeme baada ya kukamilika. Taarifa ya Tanesco inaeleza hadi Februari 2026 uwezo wa mitambo ya kufua umeme kwenye Gridi ya Taifa ulifikia jumla ya megawati 3,975.5 wakati mahitaji ya juu kabisa ya umeme kwenye Gridi ya Umeme ya Taifa yalikuwa megawati 2,071.3.
Awali, katika bajeti ya Wizara ya Nishati kwa mwaka wa fedha 2025/2026, serikali ililieleza Bunge kuwa uwezo wa mitambo ya kufua umeme iliyounganishwa katika mfumo wa Gridi ya Taifa ulikuwa umeongezeka na kufikia megawati 4,031.71 Aprili mwaka jana sawa na ongezeko la asilimia 86.6 ikilinganishwa na megawati 2,138 zilizokuwepo Machi 10, 2024.
Bunge lilielezwa kwamba katika kiasi hicho, megawati 2,716.27 (asilimia 67.4) ulikuwa umeme uliotokana na maji, megawati 1,198.82 (asilimia 29.7) gesi asilia, megawati 101.12 (asilimia 2.5) mafuta, megawati tano (asilimia 0.1) jua na megawati 10.5 (asilimia 0.3) tungamotaka.