Dar es Salaam. Waziri Mkuu, Dk Mwigulu Nchemba amekumbushia magumu waliyopitia wananchi wa Longido mkoani Arusha kutokana na changamoto ya maji, akisema familia nyingine zilitumbukia kwenye umaskini.

Dk Mwigulu amekumbushia hali hiyo leo Februari 23, 2026 baada ya kukagua mradi wa maji Sinya uliopo Longido mkoani Arusha, uliotajwa kuwa tiba ya changamoto ya maji safi kwa wananchi wa wilaya hiyo.

Waziri Mkuu amesema mradi huo wa maji ulikuwa hitaji la lazima kwa ajili ya wananchi wa wilaya hiyo, kutokana na shughuli wanazofanya.

“Ni kwa vile hatutangazi hasara za kukosa maji katika wilaya hii, kitendo cha Rais Samia Suluhu Hassan kusema kwa gharama yeyote mradi huu uletewe, mimi naendelea kusema amejua gharama ya hasara ambayo wananchi wa Longido mnapata ni kubwa sana,” amesema na kuongeza.

“Zipo familia zilizokuwa na hali nzuri kiuchumi lakini zikarudi kwenye umaskini kutokana na mifugo kukosa maji, kuna familia moja naikumbuka kwenye zizi moja walikufa ng’ombe 60 hadi 70 ndama ndio usiseme, nimpongeze Rais Samia kwa kuleta suluhisho kwenye jambo ambalo lilikuwa gumu la kilio kwa wananchi wa hapa.”

Awali, akitoa taarifa ya Shule ya Sekondari Sinya kabla ya kuzinduliwa kwake, Mwalimu Mkuu wa shule hiyo aliyejitambulisha kwa jina moja Emmanuel, ameeleza shule hiyo ina jumla ya walimu 12 na wanafunzi 387.

Mwalimu huyo amemuomba Waziri Mkuu kujengwa uzio kwenye shule hiyo kutokana na mazingira yake kuzungukwa na wanyama wakali, wakiwemo tembo, simba na chui.

“Tunaomba pia tujengewe nyumba za walimu, tuna walimu 12 lakini tuna nyumba moja, tunahitaji pia mabweni kwa ajili ya wanafunzi wa shule yetu,”amesema.

Akizindua Shule ya Sekondari ya Sinya, Waziri Mkuu amesema taarifa aliyopewa kuhusu ujenzi wa shule hiyo imezingatia ubora na fedha zilizotolewa na Serikali.

Dk Mwigulu amesema suala la uzio ni jambo muhimu na litazingatiwa akimuelekeza mkurugenzi kuangalia tatizo hilo kupitia bajeti ya halmashauri na kama kutakuwa na ziada ya fedha inayohitajika awasiliane na Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi).

Kwa upande wa Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), anayeshughulikia afya, Dk Jafar Seif, akizungumzia miundombinu ya Shule ya Sinya amemuelekeza Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Longido kuangalia kiwango cha fedha kwa ajili ya ujenzi wa uzio na nyumba za walimu.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *