Dar es Salaam. Waziri wa Ujenzi, Abdallah Ulega, ametangaza kutoa Sh10 milioni kwa wanafunzi watatu bora wa uhandisi na ukadiriaji majenzi kutoka vyuo vikuu vyote nchini watakaoandika miradi ya ubunifu itakayosaidia kutatua changamoto zinazoikabili Tanzania.

Amezitaja baadhi ya changamoto hizo kuwa ni foleni katika majiji, gharama kubwa na zinazojirudia za matengenezo ya barabara kila mwaka pamoja na upatikanaji wa makazi bora. Amesema wanafunzi watakaoandika maandiko bora yenye suluhu ya changamoto hizo watashinda sehemu ya fedha hizo.

Kwa mwaka wa fedha 2024/25, Serikali ilitenga Sh594 bilioni kwa ajili ya matengenezo ya barabara kuu na za mikoa, na Sh255 bilioni kwa barabara za wilaya. Aidha, katika hotuba ya mwaka 2021, Rais Samia Suluhu Hassan alisema msongamano wa magari jijini Dar es Salaam unasababisha hasara ya takriban Sh4 bilioni kwa siku, sawa na Sh1.44 trilioni kwa mwaka.

Waziri wa Ujenzi, Abdallah Ulega, akizungumza na Jumuiya ya Wanafunzi wa Ndaki ya Uhandisi katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) leo Jumatatu, Februari 23, 2026. 

Ulega ameyasema hayo leo, Jumatatu Februari 23, 2026, alipokutana na Jumuiya ya Wanafunzi wa Fani za Uhandisi katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM). Amesema wizara yake inalenga kuchochea ubunifu miongoni mwa wanafunzi wa uhandisi ili wawe sehemu ya suluhu ya changamoto za Taifa.

“Dunia nzima wahandisi ni chachu ya maendeleo. Changamoto za nchi yetu kwenu zinapaswa kuwa fursa,” amesema.

Amesema aliwahi kuulizwa na Rais Samia ni ubunifu gani unaweza kupunguza gharama za matengenezo ya barabara zinazoharibika kila mwaka, akisisitiza kuwa ni lazima kupatikane suluhu ya kudumu.

“Katika kipindi chote nitakapokuwa Waziri wa Ujenzi, vijana watakaoleta suluhu inayokubalika kitaalamu, nimetenga Sh10 milioni kwa watatu bora,” amesema.

Waziri wa Ujenzi, Abdallah Ulega, akizungumza na Jumuiya ya Wanafunzi wa Ndaki ya Uhandisi katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM)

Mbali na fedha hizo, washindi watasaidiwa kusajiliwa katika bodi za kitaaluma, kufungua kampuni na kupewa mkataba wa Serikali kutekeleza wazo lao.

“Fedha ni kichocheo tu. Ukiwa na usajili, kampuni na kazi, utaajiri wengine na ubunifu wako unaweza kuingiza Taifa fedha za kigeni,”amesema.

Ameongeza kuwa fedha hizo zitatolewa kila mwaka na yuko tayari kuwakaribisha wadau wengine kuunga mkono mpango huo. Amesema hatua hiyo inalenga kumuunga mkono Rais Samia ambaye hivi karibuni alitoa Sh200 bilioni kwa ajili ya kuwawezesha vijana na wanawake.

Ulega amesema matarajio yake ni kuona wahandisi wanaofikiria miradi itakayoboresha maisha ya Watanzania. Ametolea mfano nchi kama China na Vietnam, ambako vijana wamechangia ubunifu katika miradi ya barabara za mijini kurahisisha usafiri kwenda shule, hospitali na masokoni.

Aidha, amesema fani ya uhandisi inabadilika kwa kasi na ni muhimu kuendana na teknolojia, hasa Akili Mnemba (AI).

“AI haikwepeki. Kazi yetu ni kujikinga na athari zake hasi. Haikuja kuchukua ajira za wahandisi bali kusaidia kuboresha kazi zao,” amesema.

Asimulia maisha yake

Ulega amesema alisoma UDSM kati ya mwaka 2002 na 2005, na sasa ni takriban miaka 21 tangu amalize masomo. Akiwa mwanafunzi, alikumbana na changamoto za kifedha na usafiri.

Amesema wakati mwingine walitembea kwa miguu kupitia njia za mkato kwa kukosa nauli, na mara kadhaa alibakiwa na Sh5 akilazimika kuchagua kati ya kula au kupanda daladala.

“Nilikula mihogo, nilitembea kwa miguu na wakati mwingine nilirudi nyumbani bila chakula. Lakini leo hii mimi ni waziri. Tanzania ni nchi ya fursa,” amesema.

Amesema simulizi hiyo inalenga kuwahamasisha vijana kuwa changamoto za leo haziwezi kuwazuia kufikia mafanikio.

Awali, Mkuu wa Ndaki ya Uhandisi na Teknolojia (CoET) ya UDSM, Dk Innocent Macha, amesema ndaki hiyo inatoa programu 10 za shahada katika sekta ya ujenzi, ambayo ni mhimili wa uchumi jumuishi na shindani.

Amesema UDSM imeboresha mitaala ili wahitimu wawe na ujuzi unaoendana na soko la ajira, ujasiriamali na utatuzi wa changamoto za karne ya 21.

Kwa sasa, amesema CoET inatoa ushauri wa kitaalamu katika miradi 40 inayoendelea, huku wahandisi wake wakiwa na uwezo wa kusanifu na kusimamia miradi ya barabara kwa ufanisi, ingawa bado hawajatumika ipasavyo katika baadhi ya miradi mikubwa.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *