
Dar es Salaam. Katika hatua inayolenga kuongeza imani kwa wawekezaji na kulinda masilahi ya wafanyabiashara, Tume ya Ushindani (FCC), imesema itaanza kutekeleza uamuzi wake dhidi ya kampuni hata pale mlalamikaji atakapokata rufaa katika Baraza la Ushindani (FCT).
Mamlaka hiyo inatokana na marekebisho ya Sheria ya Ushindani ya Mwaka 2024, yaliyolenga kuziba mianya iliyokuwa ikiruhusu baadhi ya kampuni kuchelewesha utekelezaji wa uamuzi ya tume.
Meneja wa Huduma za Sheria wa FCC, Josephat Mkizungo amesema awali, mlalamikaji alipowasilisha rufaa, utekelezaji wa uamuzi wa tume ulikuwa unasimamishwa, hali iliyotumiwa na baadhi ya wafanyabiashara kuchelewesha utekelezaji.
“Sheria mpya inatupa nguvu ya kuhakikisha maamuzi yanatekelezwa wakati rufaa ikiendelea kusikilizwa,” amesema Mkizungo leo Jumatatu Februari 23, 2026 katika semina iliyoandaliwa na FCC kwa wahariri wa vyombo vya habari kuwajulisha kuhusu marekebisho hayo ya kisheria.
Amesisitiza kuwa, walalamikaji bado wana haki ya kupeleka shauri lao katika Mahakama Kuu iwapo hawataridhishwa na uamuzi wa FCT.
Ulinzi kwa mlaji waimarishwa
Amesema sheria hiyo pia imeimarisha ulinzi kwa watumiaji wa bidhaa.
Awali, FCC haikuwa na mamlaka ya kuchukua hatua dhidi ya wafanyabiashara waliokuwa wakiwapotosha wateja kwa kuuza bidhaa zisizokidhi viwango vilivyotangazwa.
“Kumekuwa na matukio, mteja ananunua bidhaa, kama jokofu likitangazwa kufanya kazi kwa namna fulani, lakini linapofikishwa halifanyi kazi hiyo. Sasa tuna mamlaka ya kufuatilia na kuhakikisha haki inapatikana. Mlalamikaji anapaswa kuwa na uthibitisho wa manunuzi kama risiti, jambo ambalo Watanzania wengi hawalifahamu. Tuko tayari kuwasaidia,” amesema.
Ameongeza kuwa, kupitia sheria hiyo, Watanzania hususan wa kipato cha chini wanaweza kunufaika zaidi, kwa kuwa wamekuwa wakikumbwa na changamoto kwa muda mrefu.
Hivi sasa, mamlaka zinaandaa utaratibu wa kuwafikia wananchi na kupokea malalamiko yao pindi wanapouziwa bidhaa tofauti na walizokubaliana.
Adhabu kali kwa ukiukwaji
Marekebisho hayo pia yameweka bayana kuwa kampuni zenye nguvu kubwa sokoni haziwezi kutumia nafasi hiyo kuondoa ushindani au kunyanyasa biashara ndogo. Ukiukwaji unaweza kutozwa faini ya kati ya asilimia tano hadi 10 ya mapato ghafi ya mwaka.
Aidha, kampuni zinazokusudia kuungana au kununua nyingine zenye mapato ya Sh3.5 bilioni au zaidi kwa mwaka zitalazimika kutoa taarifa kwa FCC kabla ya kukamilisha mchakato huo, ili Tume iweze kupitia mabadiliko makubwa ya soko.
Mkizungo amesema ushindani wa haki ni nguzo muhimu ya ukuaji wa uchumi. “Wananchi wanapowasilisha malalamiko yenye ushahidi, wanalinda haki zao na kusaidia kudumisha soko lenye usawa linaloimarisha uchumi wa taifa,” amesema.
Akifungua semina hiyo, Mkuu wa Wilaya ya Ilala, Edward Mpogolo amesisitiza umuhimu wa kuongeza uelewa wa umma kuhusu haki za mlaji na umuhimu wa ushindani.
“Semina kama hizi zinawaelimisha wananchi kuhusu haki zao. Mfano, mteja anaweza kuuziwa bidhaa yenye jina linalofanana na chapa maarufu kwa bei ya chini, lakini ikaharibika muda mfupi baadaye. Uelewa unawalinda wananchi,” amesema.
Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa FCC, Khadija Ngasongwa amesema semina kama hiyo zitafanyika kwa makundi mbalimbali nchini ili kuwaelimisha wananchi kuhusu sheria mpya na namna ya kunufaika nayo.
Ameongeza kuwa, marekebisho hayo yanahusu pia vitendo vilivyopigwa marufuku vinavyokiuka ushindani na yamelenga kuunda soko lenye haki kwa biashara zote.
“Kwa kutekeleza hatua hizo, mapato ya Serikali yataongezeka na imani ya wawekezaji itaimarika,” amesema