MAHAKAMA ya Tanzania imemaliza mashauri ya kimkakati yanayohusisha biashara, uchumi, kodi na ardhi yenye thamani ya Sh trilioni 13.1 na fedha hizo zimeingia kwenye mzunguko wa matumizi.
Msajili Mkuu wa Mahakama Tanzania, Eva Nkya amesema mashauri hayo 2,973 yalisikilizwa katika kipindi cha kuanzia Novemba 3 hadi Desemba 15, mwaka jana.
Nkya aliwaeleza waandishi wa habari Dodoma kwamba Oktoba 8, mwaka jana mahakama iliitisha kikao cha wadau wa masuala yanayohusu biashara na uchumi ili kuweka mikakati ya kusikiliza mashauri 2,128 ya kiuchumi yaliyokuwa tayari kwa usikilizaji na yalikuwa katika ngazi mbalimbali za mahakama.
Alisema kwa upande wa Mahakama za Rufani kulikuwa na mashauri 405, Mahakama Kuu mashauri 1,673, Mahakama za Hakimu Mkazi mashauri 17 na mahakama za wilaya mashauri 33.
SOMA: Mahakama itekeleze aliyoagiza Samia kufanikisha Dira 2050
“Mashauri hayo yalikuwa yameshikilia fedha kiasi cha Shilingi trilioni 4.4 za Kitanzania, lakini tulikuwa pia na mashauri ya aina hiyo 4,217 yakihusiana na mambo ya uchumi, biashara, kodi na ardhi,” alifafanua Nkya.
Alisema mashauri hayo yalianza kusikilizwa Novemba 3 mpaka Desemba 15, 2025, na yalisikilizwa kwa njia ya vikao maalumu.
“Pia mashauri yalisikilizwa kwa njia ya kawaida ambayo mahakama huwa inasikiliza kila siku. Wakati wa usikilizaji wa mashauri hayo baadhi ya mashauri yaliisha mapema, kwa hiyo ilitupa fursa ya kuongeza mashauri mengine katika kipindi ambacho walikuwa wamejipanga kwa ajili ya kusikiliza mashauri ya kiuchumi,” alieleza msajili huyo.
“Mashauri 1,068, kati ya hayo mashauri 256 yalikuwa yakihusiana na masuala ya hifadhi ya jamii, jumla yalikuwa mashauri 3,195. Wakati tunamaliza usikilizaji wa mashauri haya Desemba 15, tulipata mafanikio makubwa kwa sababu tuliweza kumaliza mashauri zaidi ya asilimia 93 ya yale mashauri ambayo tuliyojipanga,” alieleza Nkya.
Alibainisha zaidi: “Hapo awali tulikuwa tumepanga mashauri 2,128, lakini kwa sababu mashauri mengine tuliweza kumaliza mapema, basi tuliongeza mashauri kwa hiyo jumla tulikuwa na mashauri 3,196. Tuliweza kumaliza mashauri 2,973, hii ikiwa zaidi ya lile lengo tulilokuwa tumejipangia”.
Pia, alisema wakati wanapanga mikakati, yale mashauri yaliyokuwa mahakamani yalikuwa yameshikilia kiasi cha fedha Sh trilioni 4.4, lakini haya mashauri ambayo yalimalizika yaliweza kushikilia Sh trilioni 13.1.
Alisema kwa upande wa mahakama mashauri 18 yaliisha kwa njia ya usuluhishi, lakini pia mashauri 25 ya wadaawa katika kesi hizo waliomba kufanya usuluhishi nje ya mahakama.
Alisema wanajivunia mafanikio ambayo wameyapata kama mahakama na wadau wote wa masuala ya biashara na uchumi, masuala ya kimadai yameendana na kaulimbiu ya Siku ya Sheria ya mwaka huu ambayo ilikuwa inasema: “Mchango wa Mahakama katika ustawi wa jamii na maendeleo ya nchi”.
“Sisi mahakama kazi yetu ni kwamba tunasikiliza mashauri mapema ipasavyo ili kuwapunguzia wadaawa wanaokuja katika mashauri yao muda na gharama za kuja kusikiliza mashauri mahakamani,” alieleza Nkya.
Alisema kufanyika kwa vikao maalumu kumechangia katika mafanikio ya mahakama katika kipindi cha mwaka uliopita kwa sababu wakati waunamaliza mwaka 2025, mashauri ambayo yalikuwa yamerundikana mahakamani yalikuwa asilimia tano tu ya mashauri walionayo.
“Vilevile tumefanikiwa kupunguza muda wa wastani wa siku, mwaka uliopita wastani ilikuwa siku 96 na mahakama za mwanzo ambazo zinachukua zaidi ya asilimia 70 ya mashauri yote ambayo yako mahakamani, wastani wao ulikuwa siku 30 tu,” alifafanua.
Alisema kikao kilichofanyika jana ni mwenendelezo wa kikao kilichofanyika Oktoba 8, mwaka jana ambacho
walikubaliana kufanya vikao vinne kwa mwaka.
