
FURSA ya bingwa wa Kombe la Shirikisho (FA) kushiriki michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika, imetajwa kuongeza ugumu na ushindani mkali wa hatua ya 32 bora, mechi zinazotarajiwa kuchezwa Machi 6 hadi 8, 2026.
Baada ya upangaji wa droo ya michuano hiyo uliofanyika leo Jumanne jijini Dar es Salaam, Mwanaspoti limezungumza na makocha, wachezaji wa zamani na wa sasa ambao wamekiri hazitakuwa mechi rahisi, kila timu itahitaji kupata nafasi ya kufika mbali zaidi.
Kocha wa JKT Tanzania, Ahmed Ally alisema: “Timu zote zilizofika hatua ya 32 bora ni nzuri, hivyo hatuwezi kuipuza Hausang FC, tunachofanya sisi ni maandalizi ya mechi hiyo.”
Kwa upande wa mshambuliaji wa timu hiyo, Edward Songo aliyefunga mabao mawili katika ushindi wa 7-0 dhidi ya Pan African hatua ya 64 bora, alisema: “Siyo mechi nyepesi, lakini tupo tayari kupambana kusogea hatua ya 16 bora kwani na sisi tunatamani kushiriki michuano ya CAF.”
Kocha wa Geita Gold, Zuberi Katwila alisema: “Droo imepangwa, kazi yetu ni kucheza, kilichobaki ni kujiandaa na mechi dhidi ya Nyika FC, utakuwa mchezo mgumu lakini tupo tayari kwa mapambano.”
Staa wa zamani wa Simba na Yanga, Zamoyoni Mogella, alisema: “Ni nafasi kwa timu zinazoshindwa kunyakua taji la Ligi Kuu Bara, kupambana na iwe fursa kwao kucheza michuano ya CAF.”
Staa mwingine wa zamani aliyecheza Yanga, Edibily Lunyamila, alisema: “Michuano ya FA kwa sasa ni migumu, timu nyingi zimeanza kuona fursa za kucheza michuano ya CAF.”
DROO ILIVYOCHEZESHWA
Katika hatua ya 32 bora, Azam iliyoiondosha Endumenti kwa bao 1-0, inakwenda kucheza dhidi ya Mbeya Kwanza ambayo nayo iliifunga FGA Talents mabao 5-0, huku mabingwa watetezi Yanga waliyoichapa Cosmopolitan mabao 2-0, wamepangwa kucheza dhidi ya Polisi Tanzania iliyofuzu baada ya wapinzani wake THB kushindwa kutokea uwanjani.
Simba ambayo iliifunga Greenland mabao 3-0, itacheza dhidi ya B19 FC iliyoitoa Dhujau kwa mabao 7-0, wakati Singida Black Stars iliyofuzu kwa kuifunga Copco mabao 3-1, imepangwa kukabiliana na Songea United iliyoiondosha Vijana kwa mabao 2-1.
Mechi zingine ni; Geita Gold vs Nyika, JKT Tanzania vs Hausang, Coastal Union vs Stand United, Namungo vs Kagera Sugar, Mbeya City vs Bandari Tanzania, Fountain Gate vs Gunners, TRA United vs Kijiwe Nongwa, Tanzania Prisons vs TMA Stars, Dodoma Jiji vs African Sports, Pamba Jiji vs Transit Camp, Mtibwa Sugar vs Mbuni na Mashujaa vs KenGold.
Katika upangaji wa droo hiyo, pia ilipangwa itakavyokuwa hatua ya 16 bora, ambapo mechi zake zinatarajiwa kuchezwa kuanzia Aprili 9 hadi 11 mwaka huu.
HATUA YA 16 BORA
Itakayoshinda kati ya Singida Black Stars dhidi ya Songea United, itacheza na mshindi baina ya Mbeya City dhidi ya Bandari Tanzania, huku mshindi kati ya Azam dhidi ya Mbeya Kwanza, mpinzani wake ni mshindi baina ya Fountain Gate dhidi ya Gunners.
Mshindi kati ya Yanga dhidi ya Polisi Tanzania, atacheza na Tanzania Prisons au TMA Stars, huku pia mshindi kati ya Simba dhidi ya B19FC, mpinzani wake ni Dodoma Jiji au African Sports.
Zingine zitakuwa hivi; Namungo/Kagera Sugar vs TRA United/Kijiwe Nongwa, Coastal Union/Stand United vs Pamba Jiji/Transit Camp, JKT Tanzania/Hausang vs Mtibwa Sugar/Mbuni na Geita Gold/Nyika vs Mashujaa/Ken Gold.
2015-2016 Yanga
2016-2017 Simba
2017-2018 Mtibwa
2018-2019 Azam
2019-2020 Simba
2020-2021 Simba
2021-2022 Yanga
2022-2023 Yanga
2023-2024 Yanga
2024-2025 Yanga
