Dar es Salaam. Wafanyabiashara wa Tanzania wamehamasishwa kuwekeza katika Jimbo la Maniema lililopo Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) kutokana na uwepo wa fursa nyingi za kibiashara, mahitaji makubwa ya bidhaa na ardhi ya kutosha kwa uwekezaji.
Wito huo umetolewa Februari 24, 2026 jijini Dar es Salaam na Gavana wa Maniema, Mussa Kabwankubi, alipokutana na wafanyabiashara wa Shirikisho la Sekta Binafsi Tanzania (TPSF). Amesema Maniema, mojawapo ya majimbo 26 ya DRC, lina ardhi kubwa ya kilimo na utajiri wa madini mbalimbali, yakiwemo yanayotumika kutengeneza simu.
Kabwankubi ameeleza kuwa jimbo hilo lina ukubwa wa zaidi ya ekari 132,000 na lina fursa nyingi za uwekezaji ambazo hazitawakatisha tamaa wawekezaji. Kuhusu usalama, amesema mapigano yanayoripotiwa yapo katika majimbo ya Kivu Kaskazini na Kivu Kusini, huku Maniema likiwa halijaguswa na hali hiyo.
Balozi wa Tanzania nchini DRC, Said Mshana, akizungumza na waandishi wa habari kwenye mkutano uliowakutanisha gavana wa Jimbo la Maniema lililopo nchi ya Jamhuri ya Demokrasia Congo (DRC), Mussa Kabwankubi, na wafanyabishara waliopo kwenye Shirikisho la Taasisi ya Sekta Binafsi(TPSF),jijini Dar es Salaam
Kwa upande wake, Balozi wa Tanzania nchini DRC, Said Mshana, amesema kuna soko kubwa la bidhaa katika jimbo hilo. Amebainisha kuwa mfuko wa saruji huuzwa zaidi ya Sh120,000 na mafuta ya nishati kufikia Sh5,000 kwa lita, hali inayoonyesha fursa ya faida kwa wafanyabiashara.
Rais wa Ushoroba wa Kati, Florio Kanju, amesema taasisi hiyo itaendelea kurahisisha usafirishaji wa mizigo kwenda nchi zisizo na bandari na kuzigeuza changamoto zilizopo kuwa fursa, ikiwemo kuhamasisha ushiriki wa sekta binafsi katika ujenzi wa miundombinu ya barabara.
Kwa upande wa wafanyabiashara, Ngomile Ngwenya kutoka kampuni ya Bravo amesema wamepata ufafanuzi kuhusu taratibu na wapi pa kufuata wanapokumbana na changamoto. Hata hivyo, ametaja changamoto kubwa katika usafirishaji kwenda DRC kuwa ni usalama wa magari na madereva kutokana na matukio ya uvamizi au utekaji yanayoripotiwa mara kwa mara.
Gavana wa Jimbo la Maniema lililopo nchi ya Jamhuri ya Demokrasia Congo (DRC), Mussa Kabwankubi, akizungumza na wafanyabishara waliopo kwenye Shirikisho la Taasisi ya Sekta Binafsi(TPSF),jijini Dar es Salaam
Aidha, ameeleza kuwa ucheleweshaji wa ukaguzi wa nyaraka mipakani ni tatizo linalosababisha safari kuchukua hadi miezi miwili, badala ya wiki tatu kama wanavyopendekeza.
Naye David Barongo wa kampuni ya Magic Builder amesema Watanzania wana nafasi kubwa ya kuwekeza Maniema, hasa ikizingatiwa kuwa bidhaa nyingi zinazoingia DRC hupitia Bandari ya Dar es Salaam. Amesema kwa kujipanga vizuri, wafanyabiashara wa ndani wanaweza kuongeza mauzo ya bidhaa za Tanzania DRC na pia kuingiza bidhaa kutoka huko, hatua itakayochangia kukuza uchumi wa nchi.