Dar es Salaam. Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi (CDF), Jacob Mkunda, amesema ujenzi wa makao makuu mapya ya Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) jijini Dodoma utagharimu takribani Sh318 bilioni, fedha zinazotolewa na Serikali ya Tanzania.
Akizungumza leo Jumanne, Februari 24, 2026 katika hafla ya uzinduzi wa jengo hilo la kudumu lililopo eneo la Kikombo, jijini Dodoma, lililozinduliwa na Amiri Jeshi Mkuu, Rais Samia Suluhu Hassan.
Jenerali Mkunda amesema kazi zote za usanifu na ujenzi zilitekelezwa na Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) kwa kushirikiana na Jeshi la Kujenga Taifa (JKT).
Amesema jengo hilo kuu linalojumuisha ofisi zote za wizara na jeshi limejengwa kwa viwango vya ubora wa hali ya juu pamoja na miundombinu madhubuti ya kiusalama kwa ajili ya wanajeshi, na watumishi wengine.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Amiri Jeshi Mkuu, Samia Suluhu Hassan akipiga light pistol juu kuashiria uzinduzi wa jengo la Makao Makuu ya Ulinzi wa Taifa (MMUT), Kikombo mkoani Dodoma Februari 24, 2026.
“Haya ni makao makuu ya kwanza ya kudumu kihistoria kwa wizara na jeshi. Tangu mwaka 1964 makao makuu ya jeshi kwa maana ya Ngome na Jeshi la Kujenga Taifa walikuwa wakitumia ya Upanga, Dar es Salaam. Baada ya Serikali kuhamia Dodoma mwaka 2019, tulianza kwa kujenga makao ya muda Msalato kabla ya kuanza ujenzi wa makao haya ya kudumu hapa Kikombo,” amesema.
Ameeleza kwa mara ya kwanza, Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa pamoja na ofisi zote za makao makuu kwa maana ya Ngome watatumia jengo moja la pamoja, hatua itakayorahisisha utendaji kazi, kuimarisha uratibu na kuongeza ufanisi katika masuala ya ulinzi wa nchi.
Jenerali Mkunda ameishukuru Serikali kwa kufadhili mradi huo pamoja na Kamati ya Kudumu ya Bunge kwa maelekezo na ushirikiano uliowezesha kukamilika kwake.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Amiri Jeshi Mkuu, Samia Suluhu Hassan akimkabidhi Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa Rhimo Simeon Nyansaho, funguo mara baada ya kuzindua jengo la Makao Makuu ya Ulinzi wa Taifa (MMUT), Kikombo mkoani Dodoma Februari 24, 2026.
Pia amewashukuru wakuu wa majeshi wastaafu kwa kuweka misingi imara iliyochangia kufanikisha utekelezaji wa mradi huo, akisema miongozo yao imekuwa kiungo muhimu katika kuimarisha ujenzi na usalama wa mipaka ya nchi.
Aidha, amewapongeza wadau mbalimbali waliohusika katika utekelezaji wa mradi huo, wakiwemo kampuni tanzu za jeshi kama Suma JKT na Ngome kwa mchango wao katika kuhakikisha ujenzi unakamilika kwa wakati na kwa viwango vinavyotakiwa.
Naye Katibu Mkuu wa Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa (JKT), Dk Faraji Mnyepe, ameelezea safari ya miaka 48 ya ujenzi wa ‘ngome’ hiyo ya ulinzi, huku akisema gharama za ujenzi wa awamu zote tatu ni Sh318 bilioni.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Amiri Jeshi Mkuu, Samia Suluhu Hassan akipiga light pistol juu kuashiria uzinduzi wa jengo la Makao Makuu ya Ulinzi wa Taifa (MMUT), Kikombo mkoani Dodoma Februari 24, 2026.
Amebainisha awamu ya kwanza ni Sh121 bilioni, awamu ya pili Sh107 bilioni na awamu ya tatu ni Sh90 bilioni.
Amesema wazo la kuunganisha Wizara ya Ulinzi, JKT na Makao Makuu ya Jeshi (Ngome) katika jengo moja lilianza miongo kadhaa iliyopita lakini lilikwama kutokana na changamoto za kiuchumi na vita.
Dk Mnyepe amesema mpango wa awali wa kujenga makao makuu ya kudumu ulianza miaka ya 1970 ukiwa na lengo la kuimarisha uratibu wa taasisi hizo mbili pamoja na Makao Makuu ya Jeshi, maarufu kama Ngome.
Hata hivyo, amesema ujenzi huo haukuweza kukamilika kufuatia kuzuka kwa Vita ya Kagera mwaka 1978 kati ya Tanzania na Uganda, hali iliyosababisha rasilimali nyingi kuelekezwa vitani na baadaye uchumi wa nchi kuyumba.
“Baada ya vita, hali ya uchumi haikuruhusu kuendeleza mradi ule kama ilivyokusudiwa,” amesema.
Amesema wazo hilo lilihuishwa tena mwaka 2014 na Rais wa awamu ya nne, Jakaya Kikwete, ambapo ilipangwa makao makuu ya ulinzi yajengwe katika kambi ya Lugalo jijini Dar es Salaam na jiwe la msingi likawekwa.
Hata hivyo, kwa mara nyingine mradi huo haukuendelea kutokana na sababu za kiuchumi.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Amiri Jeshi Mkuu, Samia Suluhu Hassan akiwa amesimama wakati wimbo wa Taifa ukiimbwa mara baada ya kuwasili katika Makao Makuu ya Ulinzi wa Taifa (MMUT), Kikombo Mkoani Dodoma Februari 24, 2026.
Dk Mnyepe amesema mwaka 2009 iliundwa kamati maalumu ya kufanya utafiti wa eneo linalofaa kwa ujenzi wa makao makuu ya kudumu. Kamati hiyo ilipendekeza eneo la Mbezi Lugalo kutokana na vigezo vya kiusalama na kimkakati.
Mabadiliko makubwa yalikuja mwaka 2015 baada ya Serikali ya awamu ya tano chini ya Rais John Magufuli kuingia madarakani na kuanza kutekeleza rasmi uamuzi wa kuhamishia makao makuu ya Serikali jijini Dodoma.
Kutokana na uamuzi huo, Wizara ya Ulinzi ilijenga makao makuu ya muda Dodoma huku ofisi za muda zikijengwa katika Mji wa Serikali, Mtumba.
Amesema maelekezo yalitolewa ili kurahisisha utendaji kazi kwa kujenga makao makuu ya kudumu yatakayounganisha taasisi zote chini ya jengo moja lenye mifumo madhubuti ya ulinzi.
Novemba 25, 2019, jiwe la msingi la ujenzi wa makao makuu hayo liliwekwa na Rais Magufuli, ambaye katika hotuba yake alisisitiza umuhimu wa jeshi kujenga majengo hayo kwa kutumia wataalamu wake wenyewe, na kuhakikisha katika awamu ya kwanza ofisi zote zinakuwa chini ya paa moja.
Kwa mujibu wa Dk Mnyepe, shughuli za usanifu zilitekelezwa na kamati maalumu iliyoundwa na jeshi, huku ujenzi ukifanywa na kikosi kazi cha jeshi kwa kutumia mfumo wa ‘force account’, unaoruhusu taasisi kutumia wataalamu na rasilimali zake kutekeleza mradi bila kutegemea makandarasi wa nje.
Amebainisha kuwa awamu ya kwanza ni ya ujenzi wa jengo hilo ambayo imeshakamilika imegharimu Sh121 bilioni iliyokamilisha ofisi zote za wizara na jeshi ikiwemo jengo kuu, ununuzi wa samani za ndani, barabara za lami za ndani na majengo ya huduma mbalimbali kuboresha mandhari, umeme na maji.
Amesema awamu ya pili itakayogharimu Sh107 bilioni itahusisha ujenzi wa kikosi cha utawala, majengo ofisi za mahusiano ya nje na makazi ya askari na utaanza baada ya maandalizi kukamilika na awamu ya tatu itagharimu Sh90 bilioni, ikihusisha ujenzi wa makazi ya maofisa jenerali, maofisa mbalimbali na watumishi wa umma.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Amiri Jeshi Mkuu, Samia Suluhu Hassan akiwasili katika Makao Makuu ya Ulinzi wa Taifa (MMUT), Kikombo Mkoani Dodoma Februari 24, 2026.
Amesema kukamilika kwa makao makuu hayo ya kudumu ni hatua muhimu katika kuimarisha utendaji kazi, kuongeza ufanisi wa uratibu na kuimarisha usalama wa Taifa kwa kuweka taasisi zote muhimu katika jengo moja lenye miundombinu ya kisasa ya kiusalama.