Vigogo viwili vya soka Tanzania, Yanga na Simba hazitokutana katika raundi ya 32 bora na 16 bora ya Kombe la Shirikisho la CRDB msimu huu baada ya droo ya hatua hizo iliyochezeshwa leo kuzipa timu hizo wapinzani tofauti.

Yanga ambayo ni bingwa wa kihistoria wa mashindano hayo tangu yaliporejeshwa msimu wa 2015/2016 ikitwaa taji mara tano, katika raundi ya 32 itakutana na Polisi Tanzania na ikipenya, katika hatua ya 16 itakutana na mshindi baina ya Tanzania Prisons na TMA Stars.

Simba ambayo imetwaa ubingwa wa mashindano hayo mara tatu, itakutana na B19 FC na timu itakayosonga mbele, kwenye hatua ya 16 bora itaumana na mshindi kati ya Dodoma Jiji na African Sports.

Azam FC imepangwa kuumana na Mbeya Kwanza na iwapo itapita, itakabiliana na mshindi wa mchezo baina ya Fountain Gate na Gunners FC.

Mabingwa wa mwaka 2018 wa mashindano hayo, Mtibwa Sugar, watakabiliana na Mbuni FC na mshindi wa mechi hiyo atakutana na atakayevuka baina ya JKT Tanania na Hausung FC.

Kwa mujibu wa Ofisa Mashindano wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Baraka Kizuguto, raundi ya 32 bora itachezwa kati ya Machi 6 hadi 8 mwaka huu na kuanzia Aprili 9 hadi 11, kutachezwa mechi za hatua ya 16 bora.

Tangu mashindano hayo yaliporejeshwa rasmi msimu wa 2015/2016, ni timu nne tu ambazo zimewahi kuonja ladha yakunyakua taji la mashindano hayo.

Timu hizo ni Yanga iiyotwaa mara tano, Simba mara tatu na Azam FC na Mtibwa Sugar ambazo kila moja imeibuka bingwa mara moja.

DROO YA HATUA YA 32 BORA KOMBE LA SHIRIKISHO LA CRDB

1. Mbeya City vs Bandari Tanzania

2. Fountain Gate vs Gunners FC

3. TRA United vs Kijiwe Nongwa

4. Tanzania Prisons vs TMA Stars

5. Dodoma Jiji vs African Sports

6. Pamba Jiji FC vs Transit Camp

7. Mtibwa Sugar vs Mbuni FC

8. Mashujaa FC vs Kengold

9. Azam FC vs Mbeya Kwanza

10. Singida Black Stars vs Songea United

11. Geita Gold vs Nyika FC

12. JKT Tanzania vs Hausung FC

13. Coastal vs Stand United

14. Yanga vs Polisi Tanzania

15. Simba vs B19

16. Namungo vs Kagera Sugar

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *