Dar es Salaam. Waziri Mkuu wa Tanzania, Dk Mwigulu Nchemba, ametoa maagizo sita kwa Wizara ya Maji akisisitiza nidhamu ya usimamizi, uwajibikaji wa watumishi na upatikanaji wa huduma bora kwa wananchi.

Akizungumza leo Jumanne Februari 24, 2026 jijini Arusha katika hafla ya ufunguzi wa Bodi za Wakurugenzi wa Mamlaka za Maji Safi, Dk Mwigulu ameagiza ukaguzi wa kina wa miundombinu ya maji nchi nzima ili kubaini na kukomesha upotevu wa maji.

Amesema bado kuna maeneo yanapoteza hadi asilimia 50 ya maji yanayozalishwa, hali aliyoiita isiyokubalika.

“Hivi ingekuwa ni biashara binafsi tungeacha iwe hivyo? Tunaacha kwa kuwa ni ya umma,” amesema.

Katika kuimarisha mapato na nidhamu, ameagiza kukomeshwa kwa miunganisho haramu inayofanywa na vishoka, akitolea mfano watu wanaojiunganishia maji kwa shughuli za viwandani au kufyatua tofali huku bili zikielekezwa kwa wananchi wa kawaida.

Waziri Mkuu Dk Mwigulu Nchemba akifungua mkutano wa bodi za Wakurugenzi za mamlaka za maji safi na usafi wa mazingira  katika hoteli ya Ngurudoto-Arusha, Februari 24, 2026

Nne, Dk Mwigulu ameagiza pia hatua zichukuliwe dhidi ya watumishi wanaofumbia macho vitendo hivyo, akisema hata kufukuzwa kwa watano kutatosha kuonesha msimamo wa Serikali.

Sambamba na hilo, ameitaka wizara kushughulikia malalamiko ya wananchi kubambikiwa bili kubwa zisizo halisi, akisema hali hiyo inawaumiza walipa kodi waaminifu na kuongeza gharama kwa watumiaji.

Kwa upande wa upatikanaji wa maji katika taasisi za umma, Dk Mwigulu amepiga marufuku wanafunzi kubeba madumu ya maji shuleni, akisema ni jambo la zamani.

Aidha, ameagiza kila shule, zahanati na kituo cha afya kiwe na kisima au mradi wa maji ndani ya mwaka mmoja.

Waziri Mkuu Dk Mwigulu Nchemba akifungua mkutano wa bodi za Wakurugenzi za mamlaka za maji safi na usafi wa mazingira  katika hoteli ya Ngurudoto-Arusha, Februari 24, 2026

“Tukijipa mwaka mmoja inatosha kumaliza hilo, mitambo tunayo, tuitumie,” amesema, akionya kuwa wanafunzi kubeba madumu ya maji ni mambo ya kizamani.

Sambamba na hayo, amesisitiza utunzaji wa vyanzo vya maji na miundombinu yake ili kulinda afya za wananchi na kuhakikisha huduma endelevu.

Akizungumza katika hafla hiyo, Waziri wa Maji, Jumaa Aweso amesema kwa kipindi cha miaka minne ya hivi karibuni, zaidi ya Sh3 trilioni zimetolewa kwa ajili ya miradi ya maji.

“Vijijini tunaendelea na miradi ya maji na tumefikia asilimia 85.2 huku mijini tukifika asilimia 92.5 na tuna miradi 28 inayoendelea,” amesema.

Waziri Aweso amesema kupitia Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (Ruwasa), katika vijiji vyote 12,333 nchini, vijiji 10,758 vimeunganishwa na huduma ya maji huku vikibaki vijiji 1575 pekee.

Amesema, Bodi za Mamlaka za Maji zilizozinduliwa leo, zimeundwa ili kusimamia mamlaka za maji zilete ufanisi na kuondoa malalamiko ya wananchi katika huduma hizo.

Waziri Mkuu Dk Mwigulu Nchemba akifungua mkutano wa bodi za Wakurugenzi za mamlaka za maji safi na usafi wa mazingira  katika hoteli ya Ngurudoto-Arusha, Februari 24, 2026.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Arusha, Thomas Sabaya, akizungumza katika hafla hiyo ameipongeza Wizara ya Maji na watendaji wake nchini akisema kuwa wanafanya kazi nzuri.

Akitolea mfano kwa Mkoa wa Arusha, amesema wakazi wa Ngorongoro walikuwa wanatembea umbali wa Kilometa 20 kuyafikia maji lakini sasa wamewekewa miundombinu ya maji wanapata maji katika maeneo yao bila shida.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *