Morogoro. Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji, Profesa Kitila Mkumbo amemwagiza Katibu mkuu wa wizara hiyo, Dk Fred Msemwa kufanya tathmini kujua kama kuna wananchi walioishi kwa muda mrefu kwenye eneo la uwekezaji wa Shamba la Mkulazi ili wanufaike au kuwa sehemu ya uwekezaji huo.

Profesa Kitila ametoa agizo hilo jana Februari 23, 2026 alipokuwa kwenye ziara ya kukagua uwekezaji kwenye mashamba ya Mkulazi yaliyopo kata za Matuli na Mkulazi, wilayani Morogoro kwa lengo la kuona kasi ya uendelezaji wa mashamba hayo inayofanywa na wawekezaji watatu kutoka India, Falme za Kiarabu na Brazil.

“Kama wananchi wapo ndani ya mashamba haya kwa muda mrefu, hatuwezi kuwapiga mateke, lazima utaratibu ufanyike, katibu mkuu, sasa mje kwa mara nyingine hapa mlifanyie kazi jambo hili, wananchi waliokuwa ndani ya mashamba haya lazima wanufaike ama wawe sehemu ya uwekezaji huu,” amesema Profesa Kitila.

Katika hatua nyingine, amemtaka Mkuu wa Wilaya na Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Mussa Kilakala kuhakikisha mashamba hayo pamoja na wawekezaji wanalindwa dhidi ya tabia ya ulishaji mifugo kwenye mashamba unaofanywa na baadhi ya wafugaji ambao wamekuwa wakitishia amani na usalama wa wawekezaji.

Pia, waziri huyo amewataka wawekezaji hao kujenga uhusiano mwema na jamii zinazowazunguka sambamba na kusaidia kwenye ujenzi wa miundombinu ya shule, zahanati na barabara.

Kuhusu uwekezaji uliofanywa, Profesa Kitila amesema unaridhisha na ni sehemu ya utekelezaji wa Dira ya Taifa ya 2050 yenye lengo la kukuza uchumi.

Akitoa taarifa ya uwekezaji huo, Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Uwekezaji na Maeneo Maalumu ya Kiuchumi (Tiseza), Gilead Teri amesema wawekezaji waliopo katika shamba hilo ni pamoja na mwekezaji kutoka Brazil anayelima hekta 10,000 na kuzalisha mazao ya mtama, mahindi na alizeti.

Zana na machine mbalimbali za kilimo zinazotumiwa na mwekezaji wa kampuni ya Eagle Agrotech Tanzania Limited anayelima miwa kwenye shamba la Mkulazi Kwa ajili ya Sukari na bidhaa nyingine za miwa. Shamba la Mkulazi lipo katika kata ya Matuli wilaya ya Morogoro. Picha Hamida Shariff

Pia, amesema yupo mwekezaji mwingine kutoka India ambaye anafanya kazi kwa shirikiano na mwekezaji kutoka Falme za Kiarabu ambaye naye atawekeza kwenye hekta 10,000 na kuzalisha miwa kwa ajili ya sukari.

Amesema shamba hilo lina ukubwa wa hekta 60,000 na uzalishaji wa miwa kwa ajili ya sukari, utakwenda sambamba na uzalishaji wa bidhaa nyingine za miwa, lakini mwekezaji huyo atazalisha umeme utakaoingizwa kwenye gridi ya Taifa endapo atakubaliana na Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco).

Meneja wa Kampuni ya Uwekezaji ya Santagro Limited kutoka Brazil, Luan Luis de Carvalho Arrua anayelima mahindi, mtama na alizeti, amesema ukubwa wa changamoto ya mifugo kulishwa kwenye shamba hilo, akisema mbali ya kusababisha hasara, pia, wafugaji wenye mifugo hiyo wamekuwa wakitishia usalama wa wafanyakazi na walinzi.

Ameeleza changamoto nyingine kuwa ni nguvu kazi akisema wafanyakazi wengi wa kwenye shamba hilo wamekuwa wakitolewa mbali kwa kuwa eneo la jirani linalozunguka shamba hilo linakaliwa na wafugaji.

Akizungumzia mipango ya kuendeleza shamba hilo, amesema kila mwaka wamekuwa wakiendeleza hekta 500 hadi 1,500 na baada ya miaka mitatu, malengo yao ni kuendeleza shamba lote.

Kilakala ambaye ni mkuu wa Wilaya ya Morogoro, ameahidi kamati yake ya ulinzi na usalama itashughulikia changamoto ya mifugo kuingizwa kwenye mashamba hayo huku akisema tayari mikakati ya kupambana na changamoto imeshawekwa.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *