
Unguja. Katibu Mkuu Kiongozi wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Balozi Zena Said, amesema Jukwaa la The Citizen Rising Woman ni muhimu kwa mustakabali wa taifa, hivyo amewataka wadau kuliunga mkono kwani limeonesha mwanga katika kuwainua wanawake nchini.
Balozi Zena ametoa kauli hiyo leo Februari 24, 2026 wakati akizindua jukwaa hilo la sita lililofanyika Zanzibar kwa mara ya pili na amesema hilo ni jambo la kimkakati katika kukuza uchumi wa wanawake na taifa.
“Ukimwezesha mwanamke, unatoa nafasi kubwa sana, siyo tu pekee, kwa hiyo tukio hili ni jambo la kimkakati ambalo linahitaji kutafakari kama taifa mahali tulipo na tunapoelekea kuhusiana na ushiriki wa wanawake katika masuala ya ushiriki wa wanawake kiuchumi,” amesema.
Amesema kila kona wanawake wanashiriki kwenye shughuli za kiuchumi, iwe kwenye kilimo, uwekezaji, sekta binafsi na wengine serikalini, wana vipaji na wana utashi wa kutaka kunyanyuka kuchangia maendeleo ya nchi yao, hivyo ametaka jukwaa hilo liwe ni fursa ya kutumika kuwanyanyua wanawake kupitia vipaji vyao na utashi wao.
“Nitoe wito kwa wadau wote kushirikiana kumnyanyua mwanamke. Taasisi za kifedha, msisite kutoa mikopo kwa wanawake. Taasisi za umma na binafsi, msisite kuwapa wanawake fursa katika ngazi mbalimbali, ikiwemo za uongozi,” amesema.
Amesema taifa linaweza kupata faida kubwa ikiwa jambo hilo litafanyika kwa uhakika, kwani Mungu amemjalia mwanamke uwezo wa kukuza mambo, licha ya wengine kuitumia kauli hiyo katika mtazamo hasi.
“Uwezo wa kukuza mambo ndiyo tumepewa na ndiyo nguvu yetu, na tunakuza kile tunachopewa, kwa hiyo inategemea tunakuza kitu gani. Yapo ambayo unaweza kukuza yakawa mazuri zaidi,” amesema.
Amesisitiza kuwa: “Kipaji tulichopewa na Mwenyezi Mungu tunatakiwa kukikuza vizuri, na mwanamke amepewa uwezo wa kukuza mambo, kwa hiyo muwezeshe vizuri, na atakuza mambo mazuri.”
Balozi Zena amesema mwanamke amekuwa akidogoshwa kila siku kupitia mila na desturi na dini, kwamba hawezi kuwa sehemu za mbele, lakini kiuhalisia, mwanamke ana nguvu na anatakiwa kuwa mstari wa mbele.
Amesema mwanamke amejengeka katika uvumilivu, kwani akibeba mimba anapitia maumivu mengi kwa kipindi cha miezi tisa, lakini anahakikisha anavumilia na kujifungua salama mtoto, ila kuna baadhi ya wanaume na wanawake wanauchukulia huo kama udhaifu wa mwanamke.
“Tunaposema nafasi za uamuzi zishirikishe wanawake, kuna mambo wanapofanya uamuzi huo, wasipokuwapo wanawake, inaweza kuathiri zaidi ya asilimia 50 bila wao kujua.
“Mwanamke akiwepo kwenye vyombo vya uamuzi, kuna baadhi ya vitu anataka viwe kipaumbele kwa sababu anajua matatizo yake, lakini akikosekana, inaweza kuleta athari kwa jamii nzima inayomzunguka,” amesema.
Amebainisha kuwa siyo suala la kutaka kutesa kwa zamu kwamba sasa wanawake ndiyo wawe juu, wanataka kuwa na mizania na kuzipa maono pande zote mbele ili kutoa vipaumbele na kuhakikisha jamii inapata inachostahili.
“Hii kauli mbiu ya Give to Gain, tuichukue kama mkakati na kuelewa kuwa ushiriki jumuishi wa shughuli za kiuchumi unamaanisha mfumo mzima wa kiuchumi utaendelea kuimarika kwa kuwashirikisha wanawake, ambao ni zaidi ya asilimia 50,” amesema Balozi Zena.
Ajenda ya kimkakati
Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni ya Mwananchi Communications Ltd (MCL), Rosalynn Mndolwa-Mworia, amesema kwa miaka mingi ajenda ya mwanamke imezungumzwa kama ajenda ya kijamii, lakini kwa sasa uwezeshaji wake si ajenda ya huruma, bali ni ya kimkakati.
“Leo ni uzinduzi wa mkakati wa kiuchumi, leo hapa Zanzibar, kupitia Jukwaa la The Citizen Rising Woman, uwezeshaji wa mwanamke siyo ajenda ya huruma, ni mkakati wa kiuchumi,” amesema Rosalynn.
Amesema Taifa haliwezi kufikia uwezo wake kiuchumi bila kuwawezesha wanawake, hivyo amesema jukwaa hilo halipo kwa ajili ya sherehe, bali kwa ajili ya uzalishaji.
“Tunapenda liwe jukwaa la kupima mchango wa wanawake katika uchumi, iwe mfumo wa kufuatilia maendeleo mwaka hadi mwaka na kuhifadhi data za wajasiriamali wanawake, na iwe ripoti ya kila mwaka ya hali ya uongozi na ushiriki wa wanawake,” amesema.
Amesema haiwezekani “kubadilisha kile tusichokipima; uwezeshaji kama uzalishaji.” Kwa mujibu wa mkurugenzi huyo, wanawake wanapopewa jukwaa na fursa za kujitangaza, inaongeza uzalishaji wa Taifa.
“Kila mwanamke anayeingizwa rasmi katika mfumo wa uchumi ni ongezeko la pato la taifa, ongezeko la ajira na ustawi wa familia; hii siyo ajenda ya usawa pekee, bali ni ajenda ya ukuaji wa pato la Taifa,” amesema.
ZEEA yawabeba wanawake
Mkurugenzi wa Wakala Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi (ZEEA), Juma Burhan, amesema kuwawezesha wanawake ni muhimu, lakini ipo haja ya kuzingatia usawa katika jamii.
Amesema wanapowezesha jamii, hususan wanawake, wanasubiri kuona matokeo chanya kutokana na kile kinachofanyika kuwezesha.
Amesema wao, kama wawezeshaji, husaidia fedha, miundombinu, masoko na namna ya kufanya biashara zao katika hali ya wepesi na kufanikiwa.
Amesema ZEEA inamwezesha mwanamke, na mwanamke anakwenda kukua, kwa hiyo ipo kwa ajili ya kuwezesha wananchi kiuchumi na inaenda sambamba na jukwaa la Rising Woman katika muktadha huo.
Amesema kupitia mradi wa Inuka, kwa kushirikiana na CRDB, tayari wameshatoa mikopo yenye thamani ya Sh53 bilioni, na kati ya fedha hizo, asilimia 66 zimeenda kwa wanawake.
“Sisi, kama taasisi ya kuwezesha wananchi kiuchumi, tunakusanya taarifa nyingi kutoka kwenye wizara zote na taasisi nyingine; tunaona jinsi ambavyo kuna jitihada za makusudi, kipekee, kuwainua wanawake,” amesema.
Hata hivyo, amesema ipo haja ya kubadilisha mitazamo, zinapotolewa fedha na masoko, lengo lake ni kuleta mapinduzi ya kiuchumi kwa wananchi.
CRDB na mikopo kwa wanawake
Meneja wa CRDB tawi la Zanzibar, Fatma Nassor, amesema benki hiyo ina maeneo ambayo inasimamia, ikiwa ni pamoja na kutoa mikopo kwa wanawake, kuhakikisha wanainuka kiuchumi.
“Tunalenga wanawake wawe wazalishaji, wakue, wainuke, na kuna mikopo ambayo inataka wakue, wawekeze katika jamii inayowazunguka. Kwa hiyo, Give to Gain kwa CRDB ni kuweka kwa jamii, hususan kwa wanawake, kuhakikisha wanaendelea kukua,” amesema.
Amesema wanawake wanatakiwa kutembea pamoja kuhakikisha wanafikia wanachokitaka.
Meneja wa Cluster NMB Zanzibar, Naima Shaame, amesema Give to Gain kwa benki yao wanamaanisha ni mkakati wa kiuwekezaji kwa kuwainua wanawake katika uongozi. Amesema wanachosubiri ni kukuza katika uchumi kwa kile wanachokitoa kwa wanawake.
Naye mwakilishi wa Baraza la Wawakilishi Viti Maalumu, Dk Nasra Nassor, amesema kwa mwanamke mwenyewe, kwa sababu wapo wanaoshindwa kujikwamua kiuchumi, hivyo wanapaswa kuanza kujitambua na kujikwamua kiuchumi katika kuendeleza uchumi wa maisha yao.
“Kwa mantiki hiyo, inahamasisha wengine, lakini nawe ukiwa na mhamko wa kujihamasisha na kukua kiuchumi katika mazingira ya uwezeshwaji.
“Onesha kwamba unaweza kufanya jambo unapopewa nafasi kama mwanamke katika fursa zinazopatikana kwenye uchumi huo,” amesema Dk Nasra.