Dar es Salaam. Serikali ya Tanzania imeteuliwa kuwa mwenyeji wa Mpango wa Ununuzi wa Pamoja wa Dawa na vifaatiba kwa nchi za Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC), maarufu SPPS, hatua inayotarajiwa kupunguza gharama za dawa na kuimarisha upatikanaji wake katika ukanda huo.

Licha ya kwamba Tanzania imewahi kuteuliwa awali, uteuzi wa sasa unaonekana wa kwanza kwa Tanzania kuwa kitovu rasmi cha uratibu na utekelezaji wa SPPS katika ngazi ya kikanda.

Uamuzi huo umetangazwa leo Jumanne, Februari 24, 2026, katika mkutano mkuu wa mawaziri wa afya na mawaziri wenye dhamana ya masuala ya Ukimwi wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika unaofanyika Johannesburg, Afrika Kusini.

Akizungumza katika mkutano huo, Naibu Waziri wa Afya, Dk Florence Samizi, amesema uteuzi wa Tanzania ni ishara ya imani kubwa iliyowekwa kwa nchi hiyo kutokana na rekodi yake ya amani, utulivu na usimamizi madhubuti wa sekta ya afya.

Amesema kupitia mpango huo, Bohari ya Dawa (MSD) itaimarishwa zaidi kama mhimili wa ununuzi, uhifadhi na usambazaji wa dawa na vifaatiba, si tu ndani ya nchi bali pia katika ukanda wa SADC.

“Ununuzi wa pamoja utawezesha nchi wanachama kupata dawa na vifaa tiba kwa bei nafuu zaidi, kupunguza changamoto za upatikanaji na kurahisisha mnyororo wa ugavi,” amesema Dk Samizi.

Amesema mpango huo pia utaongeza matumizi ya bandari na miundombinu ya Tanzania kama lango la kusambaza bidhaa za afya kuelekea nchi za SADC, jambo litakaloongeza ajira, biashara na mapato ya Taifa.

Mbali na hilo, wazalishaji wa ndani wanatarajiwa kunufaika kwa kupata soko pana la kikanda kupitia SPPS, hatua inayoweza kuchochea ukuaji wa viwanda vya ndani vya dawa na vifaatiba na kuongeza ushindani wa bidhaa zinazozalishwa nchini.

Dk Samizi amesema Tanzania tayari imeanza maandalizi ya haraka kwa kuandaa ofisi na mifumo ya kidijitali itakayotumika kusimamia utekelezaji wa mpango huo.

Ameeleza kuwa mifumo hiyo imeandaliwa na wataalamu wa ndani ili kuhakikisha uwazi, ufanisi na usimamizi wa kisasa wa mnyororo wa ugavi.

Uteuzi huo unakuja wakati nchi za SADC zikiendelea kutafuta mbinu za pamoja za kukabiliana na changamoto za upatikanaji wa dawa, hasa katika magonjwa ya mlipuko na sugu, kwa lengo la kuhakikisha usalama wa afya kwa wananchi wa ukanda huo.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *