
Dar es Salaam. Serikali ya Tanzania imesajili rasmi dawa ya Lenacapavir kwa ajili ya kudhibiti na kuzuia maambukizi ya Virusi vya Ukimwi (VVU), hatua inayotajwa kuleta mapinduzi katika tiba na kinga dhidi ya maambukizi hayo nchini.
Dawa hiyo ya sindano inayozuia maambukizi ya VVU, yenye uwezo wa kutumika kama mbadala wa ARV’s kwa wenye maambukizi ya VVU, ilionesha ufanisi kwa asilimia 100 katika jaribio la kwanza la utafiti Uganda mwaka 2025.
Tayari mchakato wa kuipitia dawa hiyo na kuiingiza kwenye mwongozo wa kitaifa wa matibabu kama miongoni mwa dawa zitakazotumika katika kudhibiti VVU, umekamilika.
Akizungumza leo Jumanne, Februari 24, 2026 Mfamasia Mkuu wa Serikali, Daud Msasi amesema dawa hiyo tayari imetambuliwa na kusajiliwa na Mamlaka ya Dawa na Vifaa Tiba (TMDA), huku mchakato wa kuiingiza rasmi kwenye matumizi ya kitaifa ukiendelea kupitia mapitio ya miongozo ya matibabu.
Amesema Lenacapavir si dawa ya kuzuia maambukizi ya VVU pekee, bali ni dawa ya muda mrefu inayofanya kazi mwilini kwa zaidi ya miezi sita baada ya kuchomwa chini ya ngozi.
“Hii ni dawa ya kipekee. Unachoma sindano mara mbili tu kwa mwaka. Ikiingia mwilini inashikamana kwenye seli na kuzuia virusi kuzaliana. Inabaki mwilini kwa muda mrefu kabla ya kusafishwa, na ndiyo maana inafanya kazi kwa asiye na maambukizi na kwa mwenye maambukizi kama mbadala wa ARV’s,” amesema Msasi.
Dawa hiyo ni ingizo jipya katika soko la kimataifa, ilisajiliwa mwaka 2025 na Shirika la Chakula na Dawa Marekani (FDA) na baadaye kutambuliwa katika miongozo ya matibabu ya Shirika la Afya Duniani (WHO).
Msasi amesema Tanzania tayari imeipitia dawa hiyo na kuiingiza kwenye mwongozo wa kitaifa wa matibabu kama miongoni mwa dawa zitakazotumika katika kudhibiti VVU.
“Tumeshai-adopt na kuiweka kwenye miongozo yetu. Sasa tupo katika hatua za majadiliano na wadau kuhakikisha upatikanaji wake unakuwa wa uhakika na kwa walengwa,” amesema.
Amesema tofauti na dawa nyingi za VVU zinazohitaji matumizi ya kila siku, Lenacapavir ina sifa ya kuwa dawa ya muda mrefu inayochomwa chini ya ngozi na kufanya kazi kwa miezi sita.
Hata hivyo, dawa hiyo inaweza kutumika kama kinga (kwa watu walio katika hatari ya maambukizi) na pia kama sehemu ya tiba kwa wanaoishi na VVU, kulingana na mwongozo wa kitabibu.
Msasi amesema tabia yake ya kukaa mwilini kwa muda mrefu ndiyo imevutia wadau wa afya duniani, kwa kuwa, inapunguza changamoto ya wagonjwa ikiwamo kusahau au kushindwa kutumia dawa kila siku.
Amesema mchakato wa kuingiza dawa hiyo nchini na katika mataifa mengine barani Afrika, unafanyika chini ya uratibu wa mashirika ya kimataifa na wadau wa maendeleo, wakiwamo Global Fund, PEPFAR na UNAIDS, kwa kushirikiana na WHO.
“Tanzania ni miongoni mwa nchi zinazofanya kazi kwa karibu na Global Fund katika kupambana na malaria, kifua kikuu na Ukimwi. Sasa moja ya dawa mpya tunazoingiza kwenye mkakati ni Lenacapavir,” amesema.
Amefafanua kuwa, baada ya usajili na kuingizwa kwenye mwongozo wa matibabu, hatua inayofuata ni kuhakikisha upatikanaji wa dawa hiyo kwa walengwa kupitia utaratibu wa pamoja na wadau hao wa maendeleo.
Aidha, The Global Fund imejitokeza kununua dozi milioni mbili kwa ajili ya kusambazwa katika nchi zenye viwango vya juu vya maambukizi ya VVU.
Matumaini mapya mapambano dhidi ya VVU
Wakati Tanzania ikiendelea na juhudi za kupunguza maambukizi mapya ya VVU na kuboresha huduma za tiba kwa wanaoishi na virusi hivyo, wataalamu wa afya wameeleza kuwa ujio wa Lenacapavir unaweza kuongeza utii wa matumizi ya dawa (adherence), kupunguza unyanyapaa unaohusiana na matumizi ya dawa za kila siku na kusaidia kufikia malengo ya kitaifa na kimataifa ya kutokomeza Ukimwi ifikapo mwaka 2030.
Serikali imesisitiza kuwa, dawa hiyo si mbadala wa tahadhari nyingine za kujikinga, bali ni nyongeza muhimu katika mkakati mpana wa kudhibiti maambukizi ya VVU nchini.
Walichokisema Nacopha
Ofisa Mtendaji Mkuu wa Baraza la Taifa la Watu Wanaoishi na Virusi vya Ukimwi (Nacopha), Deogratius Rutatwa amesema ujio wa dawa kinga ya VVU ya mfumo wa sindano ni maendeleo makubwa ya kisayansi yatakayosaidia kupunguza maambukizi mapya kwa kiwango kikubwa, hasa miongoni mwa makundi hatarishi.
Rutatwa amesema dawa hiyo ya muda mrefu maarufu Lenacapavir hutolewa kwa sindano mara mbili kwa mwaka, tofauti na dawa za vidonge zinazohitaji kumezwa kila siku au sindano za kila baada ya miezi miwili, hivyo itakuwa msaada pia kwa wenye VVU.
Amesema matumizi ya kila siku yamekuwa changamoto kwa baadhi ya watumiaji kutokana na kusahau, kuchoka au kuishiwa dawa, hali inayopunguza ufuasi na mafanikio ya kinga.
“Kwa anayechoma sindano, inapunguza hatari ya kusahau au kuishiwa dawa na kuongeza ufuasi mzuri wa matumizi,” amesema.
Dawa hiyo iliyosajiliwa TMDA, Rutatwa amesema ni mwanzo mzuri wa kupanua wigo wa kinga nchini.
Amesema makundi ambayo yamekuwa yakipewa kipaumbele ni pamoja na watu wanaojihusisha na biashara ya ngono na wale wanaoishi na wenza wenye maambukizi ya VVU.
Hata hivyo, amesema dawa hiyo itanufaisha pia wafanyabiashara, madereva wa masafa marefu na watu wengine walio katika mazingira ya hatari ya maambukizi.
Rutatwa amesema changamoto kubwa iliyokuwapo awali ilikuwa ni bei ya dawa hiyo kuwa juu, lakini jitihada zimefanyika kuruhusu uzalishaji wa kampuni zaidi ili kupunguza gharama.
Amesema upatikanaji wa sindano hiyo utasaidia pia kupunguza unyanyapaa, hasa kwa wanawake na wasichana ambao hulazimika kutumia dawa kwa siri.
“Sindano itawapa uhuru zaidi wa kujikinga bila woga wa kuonekana wanameza dawa kila siku,” amesisitiza.
Nacopha sasa inaishawishi Serikali kuruhusu upatikanaji mpana zaidi wa dawa hiyo, ikiwamo kuzipa ruhusa famasi na hospitali binafsi kuuza na kutoa huduma hiyo kwa utaratibu maalumu wa usimamizi.
Kwa sasa, Serikali imeanza utaratibu wa kuruhusu baadhi ya wateja waliokuwa wakipata dawa katika vituo vya umma kuzipata kupitia famasi ili kupunguza usumbufu.
“Tunatambua hofu ya Serikali kuhusu udhibiti, lakini kama ilivyo kwa dawa nyingine, inawezekana kuweka mifumo madhubuti ya usimamizi bila kuzuia upatikanaji,” amesema.
Ameshauri bima za afya kuanza kugharamia huduma za VVU na Ukimwi ili kuhakikisha uendelevu wa upatikanaji wa dawa hizo na kupunguza utegemezi wa wafadhili.
Amesisitiza kuwa, endapo sera na mifumo sahihi ya usimamizi itawekwa, sindano hiyo ya kinga inaweza kuwa nyenzo muhimu katika mapambano ya kutokomeza maambukizi mapya ya VVU nchini.
Rais wa Chama cha Madaktari Tanzania (MAT), Dk Mugisha Nkoronko amesema: “Dawa hii inaleta mageuzi makubwa sana kwenye tiba za VVU na Ukimwi. Haya ni matokeo ya elimu, sayansi na utafiti unaoleta tofauti kwenye maisha ya watu.
“Kusajiliwa ni hatua muhimu mno, ni hatua za awali kwa wanaohitaji kuanza kuzipata. Tunasisitiza usawa kwenye upatikanaji wake ili wananchi wote wanufaike na uvumbuzi huu.”