Timu ya tathmini ikisindikizwa na Ujumbe wa Umoja wa Mataifa wa kulinda amani nchini Sudan Kusini, (UNMISS), imesafiri zaidi ya kilomita 200 kutoka Yambio, jimboni Equatoria Magharibi kupitia barabara mbovu za vumbi ili kufika kwa jamii ambazo zimesubiri haki kwa miaka mingi.
Lengo la safari hii ni kuandaa mazingira ya kuanza kwa mahakama tembezi mwezi ujao, hatua ambayo imepokelewa kwa matumaini makubwa na wahanga wa uhalifu ambao walishaanza kukata tamaa.
Mahakama tembezi zinazoungwa mkono na UNMISS zinasaidia kuleta haki kwa jamii nchini Sudan Kusini
Simulizi zinatisha na kusikitisha
Katika tathmini hiyo, simulizi za kusikitisha zimeibuka ikiwemo ya Grace Hadia, mama ambaye mtoto wake wa umri wa miaka minane amebakwa na hajui la kufanya kwa sababu maisha ya mwanaye yameshaingia doa. Akielezea uchungu wake, Grace amesema, “Mwanangu mwenye umri wa miaka 8 amebakwa, na sijui la kufanya kwani maisha yake ya baadaye tayari yameharibiwa. Sijaweza kupata usingizi tangu tukio hili litokee. Nina tumaini kuwa haki itapatikana kupitia mahakama hii tembezi.”
Hiyo ni moja kati ya simulizi nyingi za kusikitisha ambazo zimeibuliwa huku mamlaka zikikusanya kesi 35 zinazosubiri kusikilizwa, zikiwemo kesi 9 za mauaji na 15 za ukatili wa kingono na kijinsia.
Kamishna wa Kaunti ya Mundri Magharibi, Zilpha Dawa, amesisitiza hitaji la dawati la jinsia polisi akibainisha kuwa ukatili huo unazidi kukua, “Hivi karibuni, wakati wa mazishi, mwanamke alibakwa na wanaume saba. Bado tunawatafuta washukiwa ili wafikishwe mbele ya haki. Tunachokosa ni dawati la Ukatili wa Kijinsia katika kituo cha polisi kwani kesi hizi mara nyingi huchukuliwa kama uhalifu wa kawaida tu.”
Ukosefu wa majengo ya mahakama yanayofanya kazi umesababisha washukiwa wengi kukaa gerezani kwa miaka mingi bila kuhukumiwa, jambo linalochangia msongamano mkubwa katika magereza ya eneo hilo. Mahabusu mmoja ameeleza kuwa ameshatumia miaka miwili na nusu gerezani bila kupelekwa mahakamani, lakini sasa anaona mwanga kuwa mahakama hii tembezi itatofautisha kati ya wenye hatia na wasio na hatia.
UNMISS yasaidia raia wa Mundri Sudan Kusini kupata haki kupitia mahakama tembezi
Ongezeko la msongo wa mawazo
Hali hii imeleta msongo wa mawazo kwa familia nyingi ambazo zimekuwa zikihisi kuwa mfumo wa sheria umewatupa mkono na kuacha wahalifu wakitesa mitaani. Umoja wa Mataifa kupitia mpango wake nchini Sudan Kusini UNMISS umekuwa ukisaidia mchakato huu ili kuimarisha mnyororo wa haki na kujenga imani ya wananchi kwa utawala wa sheria nchini Sudan Kusini.
Mshauri wa Sheria wa UNMISS, Jean-Marie Ouedraogo, amebainisha kuwa kupelekwa kwa mahakama hii kutasogeza huduma za kisheria karibu na watu na kusaidia kuharakisha kesi ambazo zimekwama kwa muda mrefu. Amesema, “mahakama hii itasaidia kuchakata kesi, baadhi ya watu wanaweza kuachiwa huru na wengine watafuata taratibu sahihi za kisheria kulingana na ushahidi utakaotolewa.”
Kwa wakazi wa Mundri, mahakama hii inayotembea imekuwa ni zaidi ya chombo cha kisheria, bali ni sehemu ya kuponya vidonda na kuleta uwajibikaji kwa waliofanya makosa. Kwa wengi, huu ni mwanzo wa kuamini kuwa haki iliyochelewa kwa miaka mingi, hatimaye imeanza kuwafikia hata katika vijiji vya ndani kabisa.