
BAADA ya sintofahamu ya baadhi ya wachezaji wa Yanga kutokana na kukosekana kwenye baadhi ya mechi, daktari wa timu hiyo, Moses Etutu amezungumzia hali za wachezaji hao huku akimtaja Prince Dube.
Yanga Jumapili iliyopita ilikuwa ugenini kucheza dhidi ya Namungo na kuibuka na ushindi wa bao 1-0 huku ikiwakosa nyota wake wanne ambao hawakusafiri kabisa na timu ambao ni Pacome Zouzoua, Clement Mzize, Aziz Andambwile na Edmund John kutokana na kuuguza majeraha.
Akizungumza na Mwanaspoti, daktari wa Yanga, Etutu alisema ni kweli nyota hao hawakuwa sehemu ya kikosi kutokana na matatizo mbalimbali yanayowakabili huku akithibitisha mshambuliaji wao Dube amepata jeraha dogo kwenye kifundo cha mguu.
“Dube ameungana na kina Pacome baada ya kupata shida kidogo ya kifundo cha mguu, ni jeraha dogo tu ambalo limetufanya tumpe mapumziko ya siku 10 ama mechi mbili ili aweze kurejea haraka uwanjani.
“Jeraha lake sio kubwa sana, halihitaji matibabu zaidi ni mapumziko ya muda ili kurudi kwenye utimamu ndiyo maana hakuonekana kwenye safari ya kuifuata Namungo,” alisema.
Etutu alisema kuhusu Pacome aliumia bega la kushoto akiwa katika harakati za kuwania mpira sambamba na kipa wa JS Kabylie, jeraha lake linachukua muda wa wiki moja kupona tangu siku amepata shida.
“Nafikiri huo muda sasa umeshatimia, ni suala la mwalimu kumtumia au kuendelea kumpa mapumziko ili hadi siku anarejea uwanjani anakuwa amepona kwa asilimia 100, hivyo tutegemee kumuona uwanjani hivi karibuni,” alibainisha.
Akizungumzia kuhusu Mzize, alisema mshambuliaji huyo alirudi uwanjani baada ya matibabu ya goti kwenda vizuri lakini akiwa katika harakati za kujiandaa na mchezo wa mwisho wa Ligi ya Mabingwa dhidi ya JS Kabylie aliumia tena, hivyo wamemfanyia vipimo na kumuandalia program maalum ya mazoezi, watatoa taarifa.
“Mzize baada ya upasuaji wa goti ambao ulienda vizuri alirejea uwanjani na kuendelea na majukumu akipata dakika chache za kucheza mechi ya ugenini dhidi ya AS FAR Rabat na baada ya hapo akiwa kwenye maandalizi ya mechi ya pili alipata shida kidogo, tatizo tayari limefanyiwa vipimo na anatarajia kuanza program ya mazoezi hivi karibuni,” alisema daktari huyo.
Wakati huohuo, alizungumzia shida ya Edmund, alisema alipata tatizo la bega la kushoto kwenye maandalizi ya mchezo wa JS Kabylie na lilitoka sehemu yake, akibainisha kwa kawaida kuumia kwa namna hiyo kunachukua wiki tatu ili kupona.
“Wiki hizo tatu zinamsaidia mchezaji kupona kabla ya kurudi kwenye migongano na kudondoka kama mchezaji kutokana na matukio hayo kuweza kumsababishia shida ya maumivu kwa ndani, kwa sasa anafanya mazoezi yake binafsi,” alisema.
Kwa upande wa Andabwile, alisema aliumia kidole gumba wakati anajaribu kupiga mpira, wamemfanyia vipimo na kujiridhisha ni maumivu madogo ambayo yatamchukua siku tano ili kurudi kwenye hali yake ya kawaida.