ZIKIWA zimebaki takriban siku nne kabla ya kushuhudia Dabi ya Kariakoo kati ya Yanga dhidi ya Simba, katika kikosi cha Wekundu wa Msimbazi kuna mambo ya kiuongozi yamefanywa kimkakati na benchi la ufundi la timu hiyo.

Mabadiliko hayo kwa kiasi fulani yamechangia kuifanya Simba kimyakimya inarejea kwenye ubora wake ikichangiwa pia na kubadili mambo kadhaa kwenye kikosi hicho ikiwemo wachezaji wapya walioingia dirisha dogo la usajili lililofungwa Januari 30, mwaka huu.

Wakati mabadiliko hayo yakianza kuonyesha kuzaa matunda na kurejesha makali ya timu hiyo, beki wa kati Msauzi, Rushine De Reuck amepewa majukumu maalumu ili kuhakikisha wakali hao wa Msimbazi wanaendelea kuimarika.

Kama umekuwa ukiifuatilia Simba hivi karibuni, utagundua Rushine amekuwa akiambatana na Shomari Kapombe kwenye majukumu ya unahodha na alivaa usinga pale na Kapombe alikuwa nje katika mchezo husika.

Huenda ulishangaa kuona Rushine amevaa usinga juzi kwenye mechi dhidi ya Tanzania Prisons pale Dodoma ilihali Kapombe yupo ndani.

Ipo hivi; Mwanaspoti linakuletea stori kamili kwa nini licha ya kwamba mwanzo ilielezwa Kapombe ndiye nahodha mkuu baada ya Mohamed Hussein ‘Tshabalala’ kuondoka chamani hapo, lakini bado Rushine anavaa kitambaa.

Mwanaspoti imethibitisha, tangu kuondoka kwa Tshabalala, Simba haikuchagua jopo la manahodha wa kikosi hicho moja kwa moja na kilichotokea wasaidizi wa Tshabalala ndio walivaa viatu vyake.

Kapombe na Kibu ndio walikuwa wakivaa kitambaa hicho lakini uzoefu wa Kapombe ukamfanya kukaimu nafasi ya nahodha mkuu, huku Kibu aliyetimkia Libya akiwa msaidizi.

Ujio wa Kocha Steve Barker kikosini hapo ndio umebadili kila kitu na kumfanya Rushine kupewa majukumu mazito ambayo pia yapo kwa Kapombe.

Barker aliuambia uongozi wa Simba anataka nahodha ambaye watazungumza lugha moja na kuelewana moja kwa moja ambaye pia anaweza kuwaeleza wachezaji vyema kile alichoelekezwa na kocha.

Bila kupepesa macho kocha huyo akamchagua Rushine kutokana na uelewa wake wa lugha ya kiingereza vyema pia ni Msauzi mwenzake.

Inaelezwa baadhi ya viongozi wa Simba walihoji kuhusu jambo hilo huku wakitaka nahodha mkuu aendelee kuwa Kapombe kutokana na uzoefu wake katika timu na soka kwa jumla lakini kocha akashikilia msimamo wake.

Mvutano huo ulikuwa mkubwa na wa muda mrefu lakini mwishowe kocha akawa ameshikilia shilingi na viongozi kumuachia afanye uamuzi.

Hivyo basi kwa sasa Simba ina manahodha wawili, Rushine na Kapombe ambapo kila mmoja atakuwa anavaa kitambaa hicho kutokana na sababu mbili za msingi zilizoelezwa ukiachana na zile za kawaida.

Kiongozi mmoja wa Simba ambaye hakutaka jina lake litajwe, aliliambia Mwanaspoti, licha ya Rushine na kapombe kufanya kazi kwa ushirikiano, lakini watakuwa wanabadilishiwa majukumu na mwalimu kadri atakavyowiwa.

“Kuna muda Rushine atavaa kitamba wakati Kapombe akiwa ndani na wakati mwingine Kapombe atavaa usinga na Rushine akiwa ndani.

“Lengo kuu ni kuleta maelewano baina ya wachezaji na benchi la ufundi. Hapo mwalimu ndiye atakuwa anaamua kwani kuna muda wazawa wanakuwa wengi uwanjani kuliko wageni na wakati mwingine wageni wanakuwa wengi kuliko wazawa, hivyo hizo ni baadhi ya sababu,” alisema kiongozi huyo.

Katika mechi ya juzi dhidi ya Tanzania Prisons, kikosi cha Simba kilichoanza kilikuwa na wageni saba ambao ni Djibril Kassali, Libase Gueye, Inno Loemba, Clatous Chama, Anicet Oura, Ismael Toure na Rushine, huku wazawa wanne ni Yusuph Kagoma, Nickson Kibabage na Kapombe.

Mechi nyingine ambayo Rushine alikuwa nahodha wakati Kapombe ameanza kikosini ni ile ya Februari 11, 2026 dhidi ya KMC ambayo Simba ilishinda 2-0.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *