Ziara ya siku saba ya Katibu wa Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Kenani Kihongosi, katika mikoa ya Tabora na Kigoma, imeibua matumaini kwa wananchi, lakini baadhi ya watendaji wa Serikali walijikuta kwenye wakati mgumu mbele ya kiongozi huyo.
Ugumu huo ulitokana namna ya Kihongosi alivyokuwa akiwabana akiwataka kutoa maelezo ya kina kuhusu utatuzi wa kero za wananchi na namna wanavyosimamia miradi ya maendeleo inayotekelezwa katika maeneo yao.
Lakini wapo watendaji wa Serikali waliomkosha mwenezi huyo, hatua iliyosababisha Kihongosi kuwamwagia sifa kwa namna wanavyotekeleza majukumu yao ya kuwahudumia wananchi.
Ziara hiyo iliyoanza Februari 15, 2026, ilikuwa na lengo la kukagua uhai wa chama, kufuatilia utekelezaji wa miradi ya maendeleo na kusikiliza kero za wananchi katika wilaya saba na majimbo 11 ya mikoa hiyo.
Ni ziara yake ya pili ndani ya muda mfupi, baada ya kukamilisha ziara ya siku tano katika wilaya na majimbo mbalimbali ya Mkoa wa Singida.
Katikati ya ziara hiyo, Kihongosi aliwaambia watendaji wa Serikali wa Tabora na Kigoma, hakwenda katika mikoa hiyo, kucheza bali kukagua na kufuatilia utekelezaji wa ilani ya chama hicho.
Hivyo, aliwataka watumishi wa umma kutekeleza maelekezo yote yaliyotolewa na chama hicho tawala kuhusu utatuzi wa kero za wananchi na usimamizi wa miradi ya maendeleo inayotekelezwa Kigoma na Tabora.
“Niwaomba watumishi wa umma, haya maagizo ninayoyatoa yakatekelezwe sijaja Kigoma kucheza kabisa. Nimekuja kufanya kazi na mimi mfuatiliaji kwelikweli, nitapiga simu kujua kinachoendelea.
“Asitokee mtu akasema hili limepita, halitafuatiliwa, tutakuja kukosana hapa. Chama kinapoagiza jambo lazima litekelezwe, wajibu ni kuona haki inatendeka, kila mtumishi atimize wajibu wake,” alisisitiza Kihongosi.
Kwa wananchi wengi, ziara ya Kihongosi ilikuwa ya neema kwao, wapo waliodiriki kuandika kero zao kupitia mabango ili kufikisha ujumbe wao kwa kiongozi huyo.
Lakini wapo wananchi walioliowasilisha kero zao moja kwa moja, baadhi zikapatiwa majibu na maelekezo ya papo kwa papo. Kero nyingine ziliahidiwa kufanyiwa kazi kwa hatua zaidi, zikihusisha mamlaka husika.
Uwepo wa Kihongosi uliamsha ari ya uwajibikaji huku akisisitiza umuhimu wa watendaji wa Serikali kuhakikisha wanaweka utaratibu wa kusikiliza kero za wananchi na kusimamia miradi kwa uadilifu na kwa kuzingatia thamani ya fedha.
Kwa ujumla, ziara ya awamu ya pili ya Kihongosi imejenga taswira ya uongozi unaoshuka chini na kusikiliza wananchi. Lakini pia ziara hiyo imeweka utaratibu wa kukagua uhai wa CCM kuanzia ngazi ya shina la chama hicho tawala.
Matumaini kwa wananchi
Ziara ya Kihongosi imerejesha matumaini na tabasamu kwa wananchi wa Tabora na Kigoma, kwa namna kero zao zilizohusu mtu mmoja mmoja au jamii zilivyotatuliwa au kupatiwa ufumbuzi papo hapo.
Moja ya tukio lilioibu hisia ni la mkazi wa Kasulu, mkoani Kigoma Joseph Wilbroad aliyeibukia mkutano wa hadhara wa Kihongosi na kueleza kuwa tangu mwaka 2023 amekuwa akipigwa danadana na halmashauri ya wilaya kuhusu fedha zake Sh620,000 zilizobaki.
Joseph alimwambia Kihongosi anazidai fedha baada ya kujenga nyumba za walimu na bweni katika sekondari za Nyumbikwampya na Nyumbigwa za Halmashauri ya Wilaya ya Kasulu.
“Toka mwaka 2023 hadi leo napigwa danadadana na halmashauri, mimi ni familia naomba unisaidie mwenezi,” alidai Wilbroad.
Baada ya maelezo hayo, Kihongosi alisema huo ni uzembe, akimtaka Wilbroad kusimama mbele ya meza kuu, huku akiwataka wakuu wa idara, chama, wabunge, madiwani na mwenyekiti wa halmashauri kuchangishana ili fedha hizo zipatikane.
“Haya ni mambo madogo sana lakini kuna mtu mmoja amekaa sehemu kazi yake kusaini anaamua tu kupuuza…sasa waipate dawa waone inavyouma,” ameeleza Kihongosi.
Kabla kuhitimisha mkutano huo, Kihongosi alimwita jukwaani Wilbroad na kumkabidhi kitita cha Sh 620,000 zilizochangwa papo hapo na watendaji wa halmashauri hiyo.
Kisa cha Wibroad kinafanana na kile cha fundi mjenzi mmoja mkazi wa Kilimanjaro aliyekuwa akiidai halmashauri ya wilaya ya Same Sh 2.8 milioni tangu mwaka 2022 na hakuwahi kulipwa jambo lililomshangaza Waziri Mkuu, Dk Mwigulu Nchemba aliyeamuru alipwe mara moja.
“Mheshimiwa Waziri Mkuu, tulipewa kazi ya kujenga vyoo sekondari ya Gonja tangu mwaka 2022, nimejenga vyoo. Nimebabaishwa kupewa malipo yangu hadi leo hii, naidai Sh 2.8 milioni, sijalipwa,” alidai fundi huyo.
Baada ya maelezo hayo na Dk Mwigulu kuwahoji viongozi wa Same akiwa mkuu wa wilaya na mkurugenzi ili kujiridhisha, aliwaagiza kuchangishana ili fedha ipatikane na haiwezi kutoka Serikalini kwa kuwa muda umeshapita.
Katibu wa Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Kenani Kihongosi amewataka viongozi wa Serikali waliopewa dhamana kuacha fitina na chuki, badala yake watimize majukumu ili kufikia malengo ya kuwahudumia Watanzania.
Aidha, ziara ya Kihongosi inaweza isisahaulike moyoni kwa mkazi wa Nzega mkoani Tabora, Zena Mohamed aliyemweleza mbunge wa Nzega Mjini, Hussein Bashe na Kihongosi kuwa hana nyumba ya kuishi na ana watoto sita.
Pamoja na maelezo hayo, Kihongosi alimtaka Zena kueleza asaidiwe nini ndipo alipojibu kuwa: “nahitaji kiwanja na chakula wewe (Kihongosi) na Bashe ndio mnisaidie maana nina watoto,” maelezo hayo yaliyosababisha kicheko kwa umati uliofurika.
Hiyo ni baadhi ya mifano ya kero zilizohusu mtu mmoja mmoja zilivyotatuliwa papo hapo, lakini kuna zile zilizohusu jamii ambazo kila eneo au wilaya alikokanyaga zilizokuwa zinajirudia.
Kero zilizotikisa
Miongoni mwa kero zilizotikisa katika maeneo aliyotembelea Kihongosi ni changamoto za elimu, maji, barabara na huduma bora za afya.
Mkazi wa Igunga, Tabora George Maige aliibua changamoto upatikanaji wa majisafi na salama katika baadhi ya kata, kero hiyo ilisemwa pia na wananchi wa Urambo na wale wa Jimbo la Kigoma Kaskazini.
Kutokana na hilo, Kihongosi aliwaambia wananchi analibeba jambo hilo kwa kwenda kuzungumza na Waziri wa Maji, Jumaa Aweso kwa ajili ya kupata utatuzi wa haraka wa changamoto hiyo.
Naye mkazi wa Kasulu, Delilah Mathias alimwezea Kihongosi kata ya Shunguliba ina kero ya uhaba wa walimu, hali inayosababisha wanafunzi kuangaika kupata huduma bora za elimu.
Baada ya maelezo hayo, Kihongosi aliwabana viongozi wa halmashauri wakiwemo wa elimu kueleza shida ipo wapi, ndipo alipata watendaji hao kukaa na halmashauri kujua shule zipi zina walimu wengi ili kuweka mgawanyo sahihi. “Kuna tabia moja, watu hawapendi kukaa maeneo ya vijijini badala yake wanapenda mijini, sasa chama hatuwezi kukubali hali hii iendelee tutakwenda kuzungumza na Utumishi,” amesema Kihongosi.
Wakati Salma Mussa mkazi wa Kijiji cha Kaburuka wilayani Kasulu, alimwambia Kihongosi awasaidia wanafunzi wa shule ya msingi Kaburuka wanakaa chini.
Katibu wa Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Kenani Kihongosi amewataka viongozi wa Serikali waliopewa dhamana kuacha fitina na chuki, badala yake watimize majukumu ili kufikia malengo ya kuwahudumia Watanzania.
Kero kama hiyo, Kihongosi alikumbana nayo mkoani Tabora alipokuwa akihutubia mkutano wa hadhara uliofanyika Jimbo la Manonga. “Tusaidie baba watoto wanakaa chini hakuna dawati hata moja. Jambo jingine barabara sio nzuri naomba utusaidie Mwenezi,” alisema Salma huku akipigiwa makofi.
Baada ya maelezo hayo, Kihongosi alimwita ofisa elimu, aliyekiri uwepo wa changamoto hiyo, na kuahidi inafanyiwa kazi wa sababu ipo kwenye mpango wa bajeti, maelezo ambayo hayakumtosheleza Mwenezi huyo.
“Kupitia baraza lako la madiwani chama kinawaomba madiwani wa Kasulu hapa madawati yapewe kipaumbele ili watoto wakae.Msipange safari nyingi nyingi za kwenda kujifunza na kutumia gharama kubwa huku wanafunzi wakiketi chini,” alieleza Kihongosi.