Milan, Italia. Klabu ya Norway, FK Bodø/Glimt, imeandika historia kwa kuiondoa Inter Milan katika Ligi ya Mabingwa Ulaya baada ya ushindi wa mabao 2-1 katika Uwanja wa Giuseppe Meazza, na kutinga hatua ya 16 bora kwa jumla ya mabao 5-2.
Timu hiyo iliyokuwa ikipewa nafasi ndogo kabisa imefanya moja ya maajabu makubwa katika historia ya michuano hiyo, ikiwatoa waliokuwa washindi wa pili msimu uliopita.
Bodo waliingia Uwanjani wakiwa na faida ya mabao mawili kufuatia ushindi wa 3-1 walioupata nyumbani katika mchezo wa kwanza. Hata hivyo, walilazimika kustahimili presha kubwa ya Inter mwanzoni mwa mchezo, huku mabingwa hao mara tatu wa Ulaya wakisaka bao la mapema.
Kiungo wa Bodo/Glimt, Håkon Evjen, akishangilia moja ya bao katika ushindi wa 2-1 iliopata timu yake dhidi ya Inter Milan katika Ligi ya Mabingwa Ulaya. Picha na Mtandao
Lakini wageni hao walionyesha uimara mkubwa na kutengeneza ugumu zaidi kipindi cha pili. Dakika ya 53, Jens Petter Hauge aliifungia Bodo bao la kwanza baada ya kumalizia mpira uliotemwa na kipa Yann Sommer kufuatia shuti la Ole Didrik Blomberg.
Dakika 14 baadaye, Hauge aligeuka mtoa pasi na kumtengenezea Håkon Evjen, ambaye alipachika bao la pili kwa shuti kali lililozima kabisa ndoto za Inter kurejea mchezoni.
Inter walipata bao la kufutia machozi kupitia Alessandro Bastoni dakika ya 76, lakini haikutosha kuzuia kipigo hicho cha kihistoria.
Moja ya shambulizi ambalo lilifanywa na Inter Milan katika mechi ya Ligi ya Mabingwa Ulaya dhidi ya Bodo//Glimt. Picha na Mtandao
Matokeo hayo yanaifanya Bodo kuwa klabu ya kwanza kutoka Norway kushinda hatua ya mtoano ya Ligi ya Mabingwa Ulaya.
Ushindi huo unaongeza orodha ya matokeo makubwa ya Bodo msimu huu, baada ya kuwashangaza vigogo kadhaa barani Ulaya wakiwemo Juventus, Manchester City na Atlético Madrid.
Mshambuliaji wa Bodo/Glimt, Kasper Hogh, akishangilia moja ya bao katika mechi ya mkondo wa kwanza wa mtoano Ligi ya Mabingwa Ulaya dhidi ya Inter Milan. Picha na Mtandao
Sasa, mabingwa hao wa Norway wanaweza kukutana na Man City tena au mabingwa wa Ureno, Sporting CP, katika hatua inayofuata.
Kwa Inter, ambao wanaongoza Serie A kwa tofauti ya pointi 10, huu ni mshtuko mkubwa ukizingatia walicheza fainali ya msimu uliopita dhidi ya Paris Saint-Germain (PSG), jijini Munich.
Katika michezo mingine ya mtoano iliyopigwa jana usiku, ilishuhudiwa vijana wa Diego Simeone, Atletico Madrid nao wakipenya kuingia 16 bora baada ya kuishushia kipigo cha mabao 4-1 Club Brugge.
Baadhi ya wachezaji wa Newcastle, wakishangilia moja ya bao katika ushindi wa 3-2 iliopata timu hiyo dhidi ya Qarabag katika mchezo wa mtoano wa Ligi ya Mabingwa Ulaya. Picha na Mtandao
Wengine ni Newcastle ambao wameitoa Qarabag kwa jumla ya mabao 9-3 baada ya jana kuibuka tena na ushindi wa mabao 3-2 wakati mechi ya kwanza walipokuwa ugenini walishinda mabao 6-1.
Bayer Leverkusen nao wamekata tiketi ya kutinga 16 bora baada ya kuiondoa Olympiacos kwa jumla ya mabao 2-0, ushindi ambao waliupata ugenini baada ya hapo jana kulazimishwa suluhu kwenye Uwanja wa nyumbani.
Winga wa Galatasaray, Noa Lang, akishangilia moja ya bao katika ushindi wa 5-2 iliopata timu yake dhidi ya Juventus katika mchezo wa kwanza wa mtoano Ligi ya Mabingwa Ulaya. Picha na Mtandao
Leo tena itapigwa michezo ya mtoano ambapo Atalanta watakuwa nyumbani kuikaribisha Dortmund ambao wataingia na kumbukumbu nzuri ya ushindi wa 2-0 walioupata katika mechi ya kwanza Ujerumani.
Juventus nayo itakuwa na kibarua kigumu nyumbani cha kupindua meza baada ya kuruhusu kipigo cha mabao 5-2 katika mechi ya kwanza walipokuwa ugenini dhidi ya Galatasaray.
Beki wa Paris Saint-Germain (PSG), Achraf Hakimi, ambao ni mabingwa watetezi wa Ligi ya Mabingwa Ulaya. Picha na Mtandao
PSG ambao ni mabingwa watetezi wa michuano hii, wao wataingia na faida ya bao moja baada ya kuibuka na ushindi wa 3-2 katika mchezo wa kwanza walipokuwa ugenini dhidi ya Monaco.
Real Madrid wataikaribisha Benfica pale Santiago Bernabeu katika mchezo wa marudiano baada ya kutoka kupata ushindi wa 1-0 ugenini katika mchezo ambao ulikuwa wa vuta nikuvute baada ya kuzuka kwa tuhuma za ubaguzi wa rangi.