Moshi. Naibu Waziri wa Maji, Kundo Mathew, amesema Serikali itapunguza kwa kiasi kikubwa changamoto ya upatikanaji wa maji safi na salama kwa zaidi ya wananchi 16,000 wa Kata ya Kimochi, Wilaya ya Moshi, mkoani Kilimanjaro ndani ya siku 90.

Akizungumza jana Jumatano, Februari 25, 2026, wakati akisikiliza kero za wananchi wa eneo hilo, Kundo alisema Serikali imetenga zaidi ya Sh500 milioni kwa ajili ya kukarabati vyanzo vya maji na kuboresha miundombinu, ili kuhakikisha huduma ya maji inakuwa ya uhakika ndani ya miezi mitatu.

“Tunakwenda kuweka mifumo imara itakayohakikisha wananchi wanapata maji safi na salama kwa uhakika. Serikali ipo kwa ajili ya kutatua changamoto za wananchi na tutaendelea kuboresha huduma hii katika maeneo mbalimbali,” alisema.

Aidha, alisisitiza kuwa Serikali chini ya uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan itaendelea kuimarisha huduma za maji nchini ili kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora na endelevu.

Katika hatua nyingine, Naibu Waziri huyo aliiagiza Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira Moshi (Muwsa) kuongeza uzalishaji wa maji hadi kufikia lita 1,400 kwa siku, ili kukidhi mahitaji ya wakazi wa kata hiyo.

“Nawataka Muwsa muhakikishe mnaongeza uzalishaji wa maji kulingana na mahitaji halisi ya wananchi, kwa kujenga na kuboresha miundombinu pamoja na kuendeleza vyanzo vya maji,” alisisitiza.

Kwa upande wake, Diwani wa Kata ya Kimochi, Frankmnazareti Foy, alisema bado kuna maeneo yenye upatikanaji mdogo wa maji kutokana na miundombinu chakavu iliyoanzishwa tangu enzi za ukoloni.

Alieleza kuwa baadhi ya vijiji hupata maji kwa asilimia 30 hadi 40, vingine asilimia 75, huku maeneo ya ukanda wa chini yakikabiliwa na changamoto kubwa zaidi.

“Mradi uliopo sasa ulianzishwa mwaka 1994 baada ya wananchi kujitafutia mfadhili na kushiriki kuchimba wenyewe. Hata hivyo, bado wananchi hupata maji kwa mgao, wakati mwingine mara mbili tu kwa mwezi,” alisema.

Mmoja wa wananchi wa kata hiyo, AnaMaria Gasper, alisema tatizo la maji limekuwa likikwamisha maendeleo yao kwa kuwa hutumia muda mwingi kutafuta huduma hiyo muhimu.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *