Dar es Salaam. Kamishna Jenerali wa Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA), Aretas Lyimo, ameelezea namna wanavyopambana na matumizi ya dawa za kulevya kwa wasanii nchini.

Akizungumza na Mwananchi amesema wasanii hutumia dawa za kulevya wakihisi huongeza uwezo wa kufanya kazi, na kupelekea kuingia kwenye uraibu.

“Wasanii wanakitu kimoja ambacho ni kibaya sana. Kwamba akishatoa nyimbo zake akionekana amekuwa maarufu anadhani ule umaarufu wake lazima uchagizwe na dawa za kulevya. Ndio hapo wanapokosea sana.

“Dawa za kulevya unapoanza kutumia kwa mara ya kwanza inakuchangamsha, kama ni kuimba au kucheza unaongeza kasi na munkali. Lakini kadri unavyotumia zinakupeleka kwenye uraibu,”amesema Lymo

Amesema mtu anapotumia madawa kemikali yake inaingia kwenye ubongo na kuufanya ufanye kazi zaidi ya kiwango chake.

“Kama ni kuimba inazidisha kiwango cha kawaida. Ubongo unalala kwa kutegemea dawa za kulevya kufanya kazi na usipotumia ubongo haufanyi kazi, mpaka utumie. Ikishafikia hiyo hatua unakuwa mraibu maana yake huwezi kufanya chochote bila kutumia ile dawa ya kulevya.

“Kadri unavyotumia inashusha utendaji wako, dawa za kulevya zina tabia ya kupandisha utendaji wako alafu baadaye zinashusha. Ikifikia kipindi hicho unakuwa mwisho wako wa umaarufu wako. Ndio maana unakuta mwanamuziki anaibuka ndani ya miezi kadhaa anakuwa maarufu, ndani ya muda mfupi anapotea hiyo ndio athari ya dawa za kulevya inaua vipaji vingi sana,”amesema 

Lyimo ameongezea mamlaka iliandika barua kwa walezi wa wasanii (Basata) na kuwapa muongozo kwa msanii yeyote atakaye husika na Dawa za Kulevya au kuhamasisha matumizi yake atachukuliwa hatua za kisheria.

“Tukaandika barua kwa Basata kuwaambia hakikisheni wasanii wenu yeyote atakayetunga wimbo au atakayetoa sanaa inayohamasisha kwa namna yoyote iwe maneno, vitendo dawa za kulevya tutamkamata na kumpeleka gerezani.

“Sheria ile tukaibadilisha sasahivi kuna kifungu yeyote atakaye hamasisha dawa za kulevya kwa njia ya vitendo, sauti, au nafasi anahukumiwa pia anafungwa. Lakini pia sanaa zao lazima zihakikiwe kabla hazijaenda kwa jamii,”amesema Lyimo na kuongezea 

“Ukiangalia miaka miwili nyuma, watu walikuwa wanaimba wanavuta bangi wanaimba nyimbo za kusifia ganja. Lakini sasahivi huwezi kusikia tena kwahiyo kuanzia tulipotoa tangazo yoyote atakaye kiuka tunamkamata,”amesisitiza

Aidha hakuacha kugusia wasanii waliopoteza maisha kwa kutumia sawa za kulevya

“Kuna wasanii wamefariki kwa kutumia dawa za kulevya. Kuna wasanii wamekamatwa nje kwa tuhuma za dawa za kulevya kuna wengine waliofariki baada ya kumeza dawa za kulevya zikapasukia tumboni.

“Ndiyo maana tumewaandikia barua walezi wao Basata kwamba wahakikishe yeyote tutakae mbaini anauza, anasafirisha, anatumia dawa za kulevya tutachukua hatua bila kujali umaarufu wake kwasababu sheria haina umaarufu” amesema Lyimo.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *