Madrid, Hispania. Kocha wa Benfica, José Mourinho, aliyekuwa anatumikia adhabu ya kufungiwa kusimama benchi kufuatia kadi nyekundu ya mchezo wa kwanza, taarifa zinasema alitazama mchezo huo akiwa ndani ya basi la timu.
Lakini mwisho wa siku bahati haikuwa upande wao. Na Vinicius ndiye aliyeifungia Real Madrid bao la ushindi na kuhitimisha safari ya Benfica.
Ilikuwa kama kuongeza chumvi kwenye kidonda, baada ya Mbrazili huyo kurudia shangilia yake ile ile ya kucheza karibu na kibendera cha kona tukio ambalo lilizua mjadala mkubwa wiki iliyopita kule Lisbon baada ya madai ya kutukanwa kibaguzi na Gianluca Prestianni.
Staa wa Madrid, Vinicius Jr, akishangilia kwa kucheza kwenye kibendera cha kona baada ya kufunga bao la pili katika mechi ya Ligi ya Mabingwa Ulaya dhidi ya Benfica. Picha na Mtandao
Safari hii, imekuwa tofauti na ilivyokuwa ugenini, kwani alishangiliwa kwa nderemo na vifijo kutoka kwa mashabiki wa Madrid ndani ya Santiago Bernabeu.
Madrid waliingia wakiwa na uongozi wa bao moja lakini walipata pigo baada ya mshambuliaji wao kinara, Kylian Mbappé kutolewa kikosini kutokana na majeraha ya goti. Kocha Alvaro Arbeloa, amedokeza kuwa huenda nyota huyo akakaa nje kwa siku chache.
Baadhi ya wachezaji wa Benfica, wakishangilia bao alilofunga nyota wao, Rafa Silva (ambaye yupo katikati) katika mchezo wa Ligi ya Mabingwa Ulaya dhidi ya Madrid. Picha na Mtandao
Bila Mbappe na Rodrygo, Madrid wameonekana dhaifu na wenye presha mwanzoni. Na haikushangaza Benfica walipoongoza.
Vangelis Pavlidis alipiga krosi ya chini ambayo iligongwa na Raul Asencio kuelekea langoni kwao. Ingawa Thibaut Courtois aliokoa, mpira ulimkuta Rafa Silva aliyefunga kwa urahisi.
Kiungo wa Madrid, Aurélien Tchouaméni, wakati akipiga shuti ambalo lilizaa bao la kusawazisha huku akifunga bao lake la kwanza katika michuano hiyo ya Ligi ya Mabingwa Ulaya. Picha na Mtandao
Hata hivyo, ndani ya dakika mbili tu Madrid walisawazisha. Nahodha Fede Valverde aliingia upande wa kulia na kumtengenezea nafasi Aurélien Tchouaméni aliyepiga shuti kali na kufunga bao lake la kwanza la Ligi ya Mabingwa.
Benfica waliendelea kusumbua baada ya shuti la Richard Rios kuokolewa kwa ustadi na Courtois, huku Rafa Silva akipiga mpira uliogonga nguzo ya juu na kwenda nje ya lango.
Nyota wa Real Madrid, Vinicius Jr, akishangilia kwa kuwaonesha mashabiki nembo ya Klabu hiyo baada ya kuifunga Benfica bao la pili katika ushindi wa 2-1 iliopata Madrid katika mechi ya Ligi ya Mabingwa Ulaya. Picha na Mtandao
Lakini dakika za mwisho zilikuwa za Vinicius. Ambaye alipenyezewa pasi na Valverde akimzidi kasi beki, Nicolás Otamendi na kupiga shuti la chini lililomshinda kipa, Trubin.
Baada ya ushindi huo, Madrid wanaweza kukutana na vigogo wa England, Manchester City katika hatua ya 16 bora.