MANYARA; MGODI wa Itracom Fertilizer Limited unaojihusisha na uchimbaji na uchakataji wa madini ya phosphate uliopo katika eneo la Vilima Vitatu, Wilayani Babati mkoani Manyara, umechangia Sh bilioni 1.29 katika mapato ya serikali tangu kuanza kwa shughuli zake mwaka 2023.

Hayo yamebainishwa na Mjiolojia, Waziri Mkupe, akizungumza kwa niaba ya Ofisa Madini Mkazi wa Mkoa wa Manyara, Godfrey Nyanda, ambapo amesema mapato hayo yametokana na mrabaha na ada ya ukaguzi wa madini.

Amesema tangu kuanza kwa uzalishaji, mgodi huo umezalisha jumla ya tani 69,929 za madini ya phosphate zenye thamani ya Sh bilioni 36.99, ambazo zimeuzwa katika soko la ndani na nje ya nchi, hususan Nala mkoani Dodoma na nchini Burundi.

Kwa mujibu wa Mkupe, mchango huo umeimarisha ukusanyaji wa maduhuli ya serikali na kuchochea maendeleo ya jamii inayozunguka mgodi kupitia utekelezaji wa miradi ya Uwajibikaji kwa Jamii (CSR).

Ameeleza kuwa tangu kuanza kwa shughuli zake, mgodi huo umechangia utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo ikiwemo ujenzi wa Shule ya Msingi Vilima Vitatu, nyumba za walimu, na upo katika hatua za awali za ujenzi wa bweni la shule ya sekondari ya wasichana.

Akifafanua kuhusu mauzo ya ndani, amesema kuanzia Desemba 16, 2023 hadi Februari 24, 2026, jumla ya tani 22,686 zenye thamani ya Sh bilioni 9.07 ziliuzwa kwenda Nala, Dodoma. Katika mauzo hayo, serikali ilikusanya Sh milioni 90.74 kama mrabaha na kiasi kama hicho kama ada ya ukaguzi.

Kuhusu mauzo ya nje, amesema vibali 13 vilitolewa kwa ajili ya kusafirisha tani 47,243 za madini ya phosphate kwenda Burundi zenye thamani ya Sh bilioni 27.92. Katika kipindi cha Septemba 4, 2024 hadi Februari 24, 2026, Serikali ilikusanya Sh milioni 837.64 kama mrabaha na Sh milioni 279.21 kama ada ya ukaguzi.

“Mgodi wa Itracom Fertilizer Limited umeendelea kudhihirisha kuwa sekta ya madini ya phosphate ni kichocheo muhimu cha ukuaji wa uchumi wa Mkoa wa Manyara kwa kuongeza mapato ya Serikali, kutoa ajira na kuimarisha maendeleo ya jamii,” amesema Mkupe.

Aidha, amewahimiza Watanzania kuchangamkia fursa za uwekezaji zilizopo mkoani humo, akibainisha kuwa pamoja na madini ya phosphate, Mkoa wa Manyara una rasilimali nyingine zikiwemo dhahabu, moonstone, green tourmaline, amethyst, green aventurine, limestone, azurite, chumvi, muscovite mica, feldspar na quartz crystal.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *