Bergamo, Italia. Klabu ya Atalanta imeandika historia kwa kuibwaga Borussia Dortmund na kufuzu hatua ya 16 bora ya Ligi ya Mabingwa Ulaya katika mchezo uliogubikwa na vurugu na kushuhudia kadi nyekundu tatu zikionyeshwa.
Katika dakika za mwisho jijini Bergamo, Italia, mwamuzi Jose Martinez alimtoa nje beki wa Dortmund, Ramy Bensebaini kwa kadi nyekundu baada ya kumkanyaga usoni mshambuliaji wa Atalanta, Nikola Krstovic.
Beki wa Dortmund, Ramy Bensebaini, ambaye alitolewa nje ya mchezo kwa kadi nyekundu baada ya kumkanyaga usoni mshambuliaji wa Atalanta, Nikola Krstovic, katika mechi ya mtoano ya Ligi ya Mabingwa Ulaya. Picha na Mtandao
Tukio hilo lilimuacha Krstovic akiwa ametapakaa damu na kuhitaji matibabu ya haraka, hali iliyozua taharuki uwanjani.
Penalti iliyotolewa ilipigwa kwa ustadi na Lazar Samardzic, aliyeweka mpira wavuni kwa shuti kali lililokwenda moja kwa moja kona ya juu, katika dakika za mwisho za mchezo.
Katika vurugu zilizofuata, beki wa Dortmund Nico Schlotterbeck pamoja na mchezaji wa Atalanta Giorgio Scalvini nao walioneshwa kadi nyekundu.
Nyota wa Atalanta, Lazar Samardzic, akifunga bao kwa mkwaju wa penalti katika mechi ya Ligi ya Mabingwa Ulaya dhidi ya Dortmund. Picha na Mtandao
Bao hilo liliifanya Atalanta kushinda 4-1 usiku huo na kufikisha jumla ya mabao 4-3, wakigeuza matokeo baada ya kufungwa 2-0 katika mchezo wa kwanza nchini Ujerumani.
Awali, Atalanta walianza kwa kasi baada ya mshambuliaji wa zamani wa West Ham, Gianluca Scamacca kufunga bao la mapema, kabla ya Davide Zappacosta kuongeza la pili.
Mario Pasalic aliwapa wenyeji bao la tatu, lakini Dortmund walijibu kupitia Karim Adeyemi dakika ya 75, na kufanya mechi kuwa ya presha kubwa.
Akizungumza baada ya mchezo, Zappacosta amesema:
“Watu wengi walijua tunatoka, lakini tumethibitisha tulivyo imara. Sisi hatukati tamaa.”
Katika hatua inayofuata, Atalanta wanaweza kukutana na Arsenal au Bayern Munich, katika mchezo wa hatua ya 16 bora.
Beki wa Juventus, Lloyd Kelly akioneshwa kadi nyekundu kufuatia kumgonga mshambuliaji wa Galatasaray, Baris Yilmaz. Picha na Mtandao
Juventus yatupwa nje
Katika mechi nyingine iliyokuwa ya vuta nikuvute, ilishuhudiwa vibibi kizee vya Turin, Juventus vikitupwa nje na Galatasaray.
Juventus waliingia katika mchezo wa marudiano wakiwa nyuma kwa jumla ya mabao 5-2, lakini walipata matumaini mapema baada ya Manuel Locatelli kufunga kwa mkwaju wa penalti dakika chache kabla ya mapumziko.
Beki wa Juventus, Lloyd Kelly, wakati akiteleza na kukwaruza nyuma ya mguu wa Yilmaz, hali iliyomfanya mshambuliaji huyo aanguke kwa maumivu makali. Picha na Mtandao
Hata hivyo, mambo yalibadilika mwanzoni mwa kipindi cha pili baada ya beki wa zamani wa Newcastle, Lloyd Kelly kuoneshwa kadi nyekundu kufuatia kumgonga mshambuliaji wa Galatasaray, Baris Yilmaz.
Ikiwa pungufu kwa mchezaji mmoja, Juventus walionyesha moyo wa kupambana na kufanikiwa kusawazisha katika dakika 10 za mwisho kupitia mabao ya Federico Gatti na Weston McKennie, na kuupeleka mchezo katika muda wa ziada.
Lakini nguvu ziliwaishia vibibi kizee hao na Victor Osimhen akaifungia Galatasaray bao la kwanza katika muda wa nyongeza kabla ya Yilmaz kuongeza bao la pili. Licha ya Juventus kushinda 3-2 usiku huo, Galatasaray wamesonga mbele kwa jumla ya mabao 7-5 kutokana na ushindi wa 5-2 waliopata kwenye mechi ya kwanza.
Huu ni muendelezo wa msimu mgumu kwa Juventus, ambao kwa sasa wanashika nafasi ya tano kwenye Serie A, wakiwa nyuma kwa pointi 18 dhidi ya vinara Inter.
Katika hatua ya 16 bora, Galatasaray wanaweza kuvaana na Liverpool au Tottenham.
Beki wa PSG, Marquinhos, akishangilia moja ya bao alilofunga katika mechi ya Ligi ya Mabingwa Ulaya iliyoisha kwa sare ya 2-2 dhidi ya Monaco. Picha na Mtandao
PSG yapita njia ileile tena
Mechi nyingine ilipigwa kwenye dimba la Parc des Princes, Paris, Ufaransa, ikishuhudiwa mabingwa watetezi PSG wakisonga mbele kwa ushindi wa jumla wa mabao 5-4 dhidi ya Monaco baada ya timu hizo kutoshana nguvu kwa kufungana mabao 2-2 wakati katika mchezo wa kwanza PSG ambao pia ndiyo mabingwa wa League One ya Ufaransa walishinda ugenini mabao 3-2.
PSG wanaweza kukutana na mabingwa wa dunia, Chelsea ambao waliwafunga katika mchezo wa fainali hizo zilizofanyika Marekani. Mbali na Chelsea Klabu nyingine wanayoweza kukutana nayo ni Barcelona.
Staa wa Madrid, Vinicius Jr, akishangilia kwa kucheza kwenye kibendera cha kona baada ya kufunga bao la pili katika mechi ya Ligi ya Mabingwa Ulaya dhidi ya Benfica. Picha na Mtandao
Madrid yaituliza Benfica
Licha ya kutanguliwa kwa bao moja, Real Madrid walitoka nyuma na kuandika ushindi wa 2-1 dhidi ya Benfica na Vinicius Jr ndiye aliyeifungia Madrid bao la ushindi na kuhitimisha safari ya Wareno hao.
Vangelis Pavlidis alipiga krosi ya chini ambayo iligongwa na Raul Asencio kuelekea langoni kwao. Ingawa Thibaut Courtois aliokoa, mpira ulimkuta Rafa Silva aliyefunga kwa urahisi.
Kiungo wa Madrid, Aurélien Tchouaméni, wakati akipiga shuti ambalo lilizaa bao la kusawazisha huku akifunga bao lake la kwanza katika michuano hiyo ya Ligi ya Mabingwa Ulaya. Picha na Mtandao
Hata hivyo, ndani ya dakika mbili tu Madrid walisawazisha. Nahodha Fede Valverde aliingia upande wa kulia na kumtengenezea nafasi Aurélien Tchouaméni aliyepiga shuti kali na kufunga bao lake la kwanza la Ligi ya Mabingwa.
Baada ya ushindi huo, Madrid wanaweza kukutana na vigogo wa England, Manchester City katika hatua ya 16 bora.