
Musoma. Mamlaka ya Dawa na Vifaa Tiba (TMDA) Kanda ya Ziwa Mashariki imetoa msaada wa dawa za binadamu zenye thamani ya zaidi ya Sh32 milioni kwa Jeshi la Magereza Mkoa wa Mara, ili kusaidia utoaji wa huduma za afya kwa wafungwa na watumishi katika vituo vyao vya tiba.
Dawa hizo zinatarajiwa kusambazwa katika vituo sita vya kutolea huduma za afya vinavyomilikiwa na Magereza katika wilaya za Musoma, Bunda, Serengeti na Tarime.
Akizungumza Februari 25, 2026 mjini Musoma wakati wa kukabidhi msaada huo, Kaimu Meneja wa TMDA Kanda ya Ziwa Mashariki, Aggrey Mwabuki, amesema dawa hizo zimetokana na operesheni ya ukaguzi iliyoendeshwa katika mikoa ya Mara, Simiyu na Mwanza.
Amesema katika ukaguzi huo, TMDA ilikamata dawa zilizokuwa zikihifadhiwa au kuuzwa kinyume cha sheria katika baadhi ya maduka ya dawa, kisha kufanya uchambuzi kubaini zile ambazo bado hazijaisha muda wake wa matumizi ili ziweze kutumika kwa wagonjwa.
“Baada ya ukaguzi tulikuta baadhi ya dawa kwenye maduka kinyume cha utaratibu. Baada ya kuzichambua na kubaini hazijaisha muda wake, tumeamua kuzitoa kwa taasisi ya Magereza ili zitumike katika vituo vyao vya afya,” amesema Mwabuki.
Mwabuki amewataka wamiliki wa maduka ya dawa kufuata sheria, kanuni na taratibu zinazosimamia shughuli zao ili kuepuka adhabu ikiwemo kufikishwa mahakamani.
Kwa upande wake, mwakilishi wa Mkuu wa Magereza Mkoa wa Mara, Daimon Samson, amesema dawa hizo zitagawiwa katika vituo sita vya afya vya Magereza na zitasaidia kupunguza uhaba uliopo kutokana na ongezeko la wagonjwa wanaohitaji huduma.
“Idadi ya wagonjwa wanaohitaji huduma katika vituo vyetu ni kubwa, hivyo dawa hizi zitakuwa msaada muhimu katika kuboresha utoaji wa tiba kwa walengwa,” amesema.
Ametoa wito kwa wadau wengine kuendelea kuisaidia sekta ya afya ya Magereza mkoani humo, akisema uhitaji wa dawa na vifaa tiba bado ni mkubwa.
Naye mwakilishi wa Mganga Mkuu wa Mkoa wa Mara, Erick Mhigi, ameiomba TMDA kuendeleza ushirikiano huo kwa kuendelea kutoa msaada wa dawa salama pale zinapopatikana, ili kuboresha huduma kwa wagonjwa wanaohudumiwa katika vituo vya afya vya Magereza.