
Dar es Salaam. Hatimaye, Msajili wa Vyama vya Siasa, Jaji Francis Mutungi, amevunja ukimya na kuzungumzia uongozi mpya wa Chama cha Wananchi (CUF) unaoongozwa na mwenyekiti, Mirambo Yusuf, huku akitaka wenye manung’uniko kufuata taratibu.
Chama hicho kilifanya uchaguzi mkuu wa dharura kuanzia Februari 20, 2026, ili kupata uongozi mpya. Hata hivyo, matokeo ya uchaguzi huo yameibua mgawanyiko miongoni mwa wanachama, ambapo baadhi wanatambua uongozi huo na wengine wanaupinga.
Uchaguzi huo ulifanyika kutokana na maelekezo ya Msajili wa Vyama vya Siasa, baada ya kutengua uchaguzi uliofanyika Desemba 18 na 19, 2024, uliomweka madarakani Profesa Ibarahim Lipumba na wenzake watano.
Kwa mujibu wa Msajili, sababu ya kutengua uchaguzi huo ni kwamba Profesa Lipumba na wenzake hawakupata zaidi ya nusu ya kura halali zilizopigwa na wajumbe, kinyume na matakwa ya Katiba ya chama ya mwaka 1992; hivyo, mchakato ulipaswa kurudiwa.
Uamuzi huo uliibua mgawanyiko ndani ya chama. Upande mmoja, ukiwemo wa Profesa Lipumba, ulipinga uamuzi wa Msajili kwa madai haukuzingatia haki ya msingi ya kusikilizwa kabla ya uamuzi kufanyika.
Upande mwingine, uliowasilisha malalamiko, uliunga mkono uamuzi huo ukidai uchaguzi wa Desemba 2024 haukufuata taratibu, hivyo ulipaswa kurudiwa ili haki itendeke.
Hata hivyo, baada ya kupatikana kwa uongozi mpya, chama kiligawanyika tena. Kundi moja halitambui uongozi huo, likidai haukupatikana kihalali kwa sababu baadhi ya wajumbe waliopiga kura hawakuwa halali.
Akizungumza leo, Alhamisi, Februari 26, 2027, Jaji Francis Mutungi amesema wenye malalamiko wanapaswa kufuata taratibu za kisheria badala ya kuzungumza kupitia vyombo vya habari.
“Wenye malalamiko na manung’uniko ni muhimu wafuate utaratibu wa kudai haki zao badala ya kuzungumza na vyombo vya habari,” amesema Jaji Mutungi.
Kauli hiyo imekuja wakati aliyekuwa mgombea wa nafasi ya uenyekiti, Othman Dunga, aliyepata kura 177, kutangaza nia ya kwenda ofisi ya Msajili kupinga ushindi wa Mirambo.
“Nimefuatilia na kujiridhisha kuwa wajumbe wengi waliopiga kura hawakuwa halali. Nimefanya rejea kwenye daftari la wajumbe wa mkutano mkuu na kubaini kuwa wengi wao si halali. Nipo katika hatua za mwisho kuwasilisha pingamizi kwa Msajili,” amesema Dunga.
Kwa upande wake, aliyekuwa Naibu Katibu Mkuu Tanzania Bara, Magdalena Sakaya, amesema licha ya kufungua kesi kupinga uamuzi wa Msajili, bado hawautambui uongozi mpya uliopo madarakani.
Naye Mjumbe wa Baraza Kuu la chama hicho, Dauda Hassani, ambaye ni miongoni mwa waandaaji wa mkutano huo, amesema wajumbe walioshiriki walikuwa halali, isipokuwa baadhi ya mikoa hawakushiriki.
“Kwa mfano, wajumbe kutoka mikoa ya Mara, Mwanza na Pwani hawakushiriki. Inaonekana kuna wanaolalamika wakidai nafasi zao zilichukuliwa na wengine, hivyo wanaendeleza mgogoro. Wengine bado wanaheshimu uongozi uliotenguliwa na wanatumia fursa hiyo kuendeleza mvutano,” amesema.
Amesema mkutano huo ulikuwa wa ghafla, hivyo ilikuwa ngumu taarifa kuwafikia wote na kujitokeza kwenye mkutano huo, ingawa idadi kubwa walishiriki na reja yao wanayo na namba zao.
“Wale wenye hoja waulize kama wana ushahidi, nimeona wengine wanalalamika lakini si wajumbe halali wa chama chetu, ila wanataka kukuza jambo tu,” amesema.
Dauda ameongeza kuwa baadhi ya malalamiko yanadai kuwa baadhi ya wajumbe walivaa mavazi ya rangi ya kijani, lakini Katiba ya chama haikatazi mavazi hayo.
“Kuvaa mavazi ya aina fulani hakuondoi uhalali wa mtu kuwa mjumbe. Huwezi kumzuia mtu kuvaa nguo alizonunua mwenyewe. Kwa kweli, madai hayo hayana hoja,” amesema.