MWANZA; MKAZI wa Mtaa wa National uliopo Ngudu, wilayani Kwimba mkoani Mwanza, Joyce Emmanuel, amesema kukamilika kwa jengo la watoto njiti kwenye hospitali ya kwimba ni ukombozi kwa wananchi wa wilaya hiyo.
Akizungumza nyumbani kwake wakati wa ziara ya viongozi mbalimbali, Joyce amesema alijifungua mapacha akiwa na ujauzito wa miezi sita, kila mmoja akiwa na uzito wa kilo 1.3.

Hata hivyo, kutokana na ukosefu wa vifaa vya kuhudumia watoto njiti katika zahanati ya eneo lao, walilazimika kusafiri umbali mrefu kwenda Hospitali ya Bugando Mwanza, hali iliyosababisha mtoto mmoja kupoteza maisha njiani.
Amesema hayo alipotembelewa na Mwakilishi wa Shirika la Afya Duniani (WHO) nchini Tanzania, Dk Alex Gasasira, aliyeambatana na viongozi wa taasisi ya Doris Mollel Foundation (DMF), Mkuu wa Wilaya ya Kwimba, Ng’wilabuzu Ludigija, pamoja na viongozi wengine.