TRA United imeizamisha Fountain Gate kwa kuitandika mabao 4-1 katika mechi ya Ligi Kuu Bara, iliyopigwa leo Februari 26, 2026 kwenye Uwanja wa Black Rhino uliopo Karatu jijini Arusha.

Matokeo hayo yanaifanya TRA kupanda nafasi mbili kutoka ya 12 hadi 10 kwenye msimamo wa ligi ikifikisha pointi 16 baada ya kucheza 13, ikizishusha Coastal Union (pointi 15) na Singida Black Stars (pointi 15) ambayo baadaye saa 1:15 usiku itakuwa mgeni wa Namungo.

Kwa upande wa Fountain Gate, kipigo hicho kinazidi kuiweka pabaya baada ya kubaki nafasi ya pili kutoka mkiani ikiwa na pointi 12 sawa na Tanzania Prisons iliyopo nafasi ya 14, lakini zikitofautiana kwa idadi ya mabao ya kufunga na kufungwa.

TRA iliingia uwanjani kwa tahadhari lakini ikionekana wazi kuwa na njaa ya ushindi. Mabao ya mapema yaliwapa utulivu na kuifanya Fountain Gate kushindwa kurudi mchezoni.

Mabao mawili ya Enock Jiah dakika ya 30 na 56, Amy Mapaka (dakika 45) na Chanda Chewe (dakika 51), yametosha kuwapa ushindi vijana hao wa Kocha Etienne Ndayiragije, huku Fountain Gate ikiambulia moja kutoka kwa Chukunonye Abuse dakika ya 83 ambaye aliingia kutoka benchi.

Safu ya ushambuliaji ya TRA ilionekana kuwa bora ikitumia makosa ya safu ya ulinzi ya wapinzani wao ambayo ilionekana kuyumba mara kadhaa.

Kwa dakika 90, ilikuwa ni mechi ya kasi na presha, lakini umakini wa TRA ulifanya mechi kuwa ya tofauti kubwa. Fountain Gate ilijitahidi kusawazisha kipindi cha pili lakini juhudi hizo hazikuzaa matunda.

Kabla ya leo, kwenye mechi zilizokutana timu hizo, Fountain Gate ilikuwa haijawahi kupoteza mbele ya TRA United ambayo zamani ilikuwa ikiitwa Tabora United.

Februari 2025 zilitoka sare ya 0-0, Septemba 20, 2024 Fountain Gate iliibuka na ushindi wa 3-1 dhidi ya TRA, huku Februari 25, 2024 zikigawana pointi kwa sare ya 1-1 na Agosti 31, 2023 pia zikatoka 0-0.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *