Buenos Aires, Argentina. Mshambuliaji mkongwe wa Uruguay, Edinson Cavani, ametakiwa kutundika daruga baada ya kuendelea kusuasua akiwa na klabu ya Boca Juniors, huku mashabiki wakianza kumzomea kufuatia kiwango chake kushuka.

Cavani, mwenye umri wa miaka 39, alizomewa Ijumaa wakati alipoanza kikosi cha kwanza ikiwa ni mara ya kwanza tangu Septemba mwaka jana katika sare ya bila kufungana dhidi ya Racing Club na baadaye aliachwa kwenye kikosi kilichocheza mechi dhidi ya Gimnasia Chivilcoy.

Straika huyo wa zamani wa Manchester United alijiunga na Boca Agosti 2023 lakini amekuwa na ukame wa mabao. Katika msimu wa 2025 alifunga mabao matano pekee robo ya aliyofunga mwaka 2024 huku mwaka 2026 akicheza mechi mbili tu kutokana na majeraha.

Gwiji wa soka wa zamani wa Argentina, Oscar Ruggeri, amemshauri Edinson Cavan, kuachana na soka baada ya kuonekana kushuka kiwango. Picha na Mtandao

Ni wakati wa kuacha

Shujaa wa Kombe la Dunia la mwaka 1986 akiwa na Argentina, Oscar Ruggeri, amesema wazi kuwa Cavani anapaswa kustaafu.

“Lazima aache kucheza. Ni jambo la kusikitisha kuona nyota mkubwa kama huyu anazomewa kwa namna hiyo baada ya kuwa na kazi kubwa aliyofanya,” amenukuliwa akisema.

Ruggeri ameongeza kuwa kucheza Argentina ukiwa unakaribia miaka 40 si rahisi, akieleza kuwa mwili wa Cavani unaonyesha dalili za kuchoka.

Mshambuliaji wa Boca Juniors, Edinson Cavan ambaye aliwahi kuichezea Man United ya England. Picha na Mtandao

Majeraha yamsumbua

Katika miaka ya hivi karibuni, Cavani amekuwa akisumbuliwa na majeraha ya mara kwa mara. Tangu Februari 2023, ameripotiwa kupata majeraha 13 yaliyomfanya kukosa michezo 36 ambazo ni sawa na msimu mmoja.

Hivi karibuni amekuwa akisumbuliwa na maumivu chini ya mgongo, ingawa alirejea uwanjani akitokea benchi katika mechi dhidi ya Platense mwezi huu.

Mshambuliaji wa zamani wa PSG na sasa Boca Juniors, Edinson Cavan, ameshauriwa kuachana na soka baada ya kuzomewa na mashabiki kutokana na kushuka kwa kiwango. Picha na Mtandao

Cavani aliwahi kutangaza kustaafu soka la kimataifa Desemba mwaka jana, akihitimisha safari ya zaidi ya miaka 20 iliyomshuhudia akifunga mabao 458 kwa klabu na taifa. Katika ngazi ya klabu, alitwaa mataji 24, mengi akiwa na Paris Saint-Germain (PSG).

Hata hivyo, pamoja na mafanikio hayo, mshambuliaji huyo bado anaonekana kuwa na hamu ya kuendelea kucheza.

Nyota wa zamani wa Napol, Edinson Cavan, na sasa Boca Juniors, anapitia wakati mgumu baada ya kuzomewa na mashabiki huko Argentina kutokana na kiwango chake kushuka. Picha na Mtandao

Ruggeri amesisitiza kuwa uamuzi wa mwisho upo mikononi mwa Cavani mwenyewe, akidai dalili za mwili wake ni ishara kuwa wakati umefika wa kufanya uamuzi mgumu ambao wachezaji wengi hukumbana nao mwishoni mwa taaluma zao.

Wakati Cavani akifikisha miaka 39, baadhi ya mastaa kama Zlatan Ibrahimovic waliendelea kucheza hadi miaka 41, jambo linaloonyesha kuwa umri si kikwazo kikubwa iwapo mwili unaruhusu.

Hata hivyo, presha kutoka kwa mashabiki na wadau wa soka Argentina inaonekana kuongezeka, huku wengi wakisubiri kuona kama straika huyo ataendelea kupambana au atachagua kutundika daruga rasmi.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *