MAMLAKA ya Mapato Tanzania (TRA) imetekeleza agizo la Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuzindua ofisi zinazotembea kwa kutumia magari ya huduma kwa walipa kodi. Waziri wa Fedha, Balozi Khamis Mussa Omar amezindua magari hayo na mengine 70 ya kawaida katika Chuo cha Kodi jijini Dar es Salaam.
Kamishina Mkuu wa TRA, Yusuph Mwenda amesema uzinduzi wa ofisi hizo ni hatua muhimu katika kusogeza huduma karibu zaidi na walipa kodi. Mwenda amesema TRA imenunua magari 10 ya aina hiyo, mawili yataanza kutoa huduma Dar es Salaam na mengine yatapelekwa katika ofisi za kanda za TRA mikoani.
Amesema ofisi hizo zitakuwa zikitoa huduma mbalimbali zikiwamo usajili wa walipa kodi wapya, utoaji wa elimu ya kodi, ushauri wa kitaalamu, na kupokea na kushughulikia malalamiko ya walipa kodi moja kwa moja katika maeneo yao ya biashara. “Ni mara ya kwanza katika historia ya TRA kumiliki magari ya aina hii. Tumewaalika mameneja wa mikoa washuhudie uzinduzi huu ili wakasimamie vizuri utekelezaji wake katika maeneo yao,” alisema Mwenda.

Ameongeza : “Serikali inalenga kujitegemea kwa mapato ya ndani. Hatuwezi kuzungumzia kushusha viwango vya kodi bila kwanza kuhakikisha tunapanua wigo wa walipa kodi”. Mwenda ameipongeza serikali kupitia Wizara ya Fedha kwa kuendelea kuwekeza katika miundombinu na vitendea kazi vya TRA ikiwamo ujenzi wa majengo ya kisasa, ununuzi wa vifaa kama kompyuta na magari hayo ya ofisi zinazotembea.
Balozi Omar amesema uzinduzi wa ofisi zinazotembea na ugawaji wa magari mapya kwa TRA utaongeza ufanisi katika kuwafikia walipa kodi maeneo mbalimbali ya nchi, kutoa elimu ya kodi na kuboresha huduma kwa wananchi. Amesema serikali inatambua na kuthamini hatua zinazochukuliwa na TRA za kujenga uhusiano chanya na walipa kodi, hususani wafanyabiashara ambao ni wadau wakuu wa mamlaka hiyo.

Balozi Omar amesema ushirikiano huo una mchango mkubwa kwa taifa kwani unarahisisha ukusanyaji wa mapato na kujenga mazingira bora ya biashara. Ameongeza kuwa mafanikio hayo yanapaswa kuendelezwa na kuimarishwa zaidi. “Kamishina Mkuu amesema mafanikio haya yametokana na sifa za utendaji wenu.
Kwa hiyo ukaribu wenu na wafanyabiashara muuimarishe zaidi, kwa sababu unaleta tija kwa taifa na si jambo la kupuuzwa,” alisema. Ametoa tahadhari kuhusu ombi la jumuiya za wafanyabiashara kupewa magari ya zamani ya TRA kwa muda wakati wakisubiri mchakato wa kupatiwa magari mapya, ili watekeleze majukumu yao kwa ufanisi. SOMA: TRA yazionya bandari kavu

Amesema ombi hilo limepokelewa na Kamishna Mkuu wa TRA, lakini akasisitiza kuwa linapaswa kuwasilishwa na kushughulikiwa kwa tahadhari ili kuepusha tafsiri potofu miongoni mwa wadau. “Ombi limepokelewa, nimemsikia Kamishina Mkuu lakini ni lazima muwasilishe kwa tahadhari kidogo. Wafanyabiashara wakiona mmeanza kutumia magari mliyopewa na TRA, inaweza kuzuka hoja nyingine tofauti. Wengine wanaweza kusema mmeanza kuonekana kama ni sehemu ya TRA, jambo ambalo linaweza kuleta mgongano wa maslahi,” alionya.