
Shirika la Umoja wa Mataifa la Uhamiaji (IOM) limetangaza kuwa watu wasiopungua 7,667 walifariki au kutoweka katika njia za uhamiaji duniani kote katika mwaka uliopita wa 2025, na kuonya kwamba idadi halisi ya watu hao huenda ikawa kubwa zaidi huku likiitaja hasara hiyo ya upoteaji wa roho za watu inayoendelea kushuhudiwa kuwa “kufeli kimataifa.”
Kwa mujibu wa data za IOM, katika mwaka uliopita, kivuko cha Bahari ya Mediterania kutoka Afrika hadi Ulaya kilishuhudia kupotea kwa maisha ya watu wapatao 2,108, huku wengine 1,047 wakifariki au kutoweka wakati wakijaribu kufika Visiwa vya Canary vya Uhispania.
Aidha, katika miezi miwili ya kwanza ya mwaka huu wa 2026 tayari kumeshuhudiwa “idadi isiyo ya kawaida ya vifo vya wahamiaji”, ambapo hadi kufikia Jumanne, watu 606 wameripotiwa kufariki katika kivuko cha Mediterania.
Mkurugenzi Mkuu wa IOM Amy Pope amesema, vifo hivi haviwezi kuepukika, huku akihimiza kutumiwa njia salama za kisheria.
Amebainisha kuwa, kupunguzwa kwa ufadhili kwa makundi ya misaada, ukandamizaji dhidi ya mashirika yasiyo ya kiserikali ya kibinadamu, na ufikiaji mdogo wa data kunazuia kufanyika ufuatiliaji sahihi. Aidha, mabaki ya watu 23 yamesombwa katika pwani za kusini mwa Italia na Libya katika wiki mbili zilizopita pekee, huku mamia zaidi wakipotea baharini jambo ambalo inawiya vigumu kuthibitishwa.
Kwa mujibu wa IOM, kupungua kimataifa idadi ya vifo 9,200 vya mwaka 2024 kunaonyesha kwa kiasi fulani kufanyika majaribio machache ya njia hatari, hasa kwenye mpaka wa Marekani na Mexico na msitu wa Darien, ambapo shirika hilo la Umoja wa Mataifa limerekodi vifo vichache zaidi vya watu 409 tangu 2014…/