Marekani. Rapa wa Marekani, Megan Thee Stallion ameweka wazi kuwa yuko tayari kuvishwa pete na kuolewa na mpenzi wake nyota wa mpira wa kikapu wa NBA, Klay Thompson.
Kwenye video aliyoichapisha kwenye ukurasa wake wa YouTube akiwa na nyota wa wanamichezo Laila Edwards, Brittany Bowe na Hilary Knight ambao walikuwa wakijadili kuhusu ndoa.
Megan aliwapongeza Bowe na Knight kwa kuchumbiana hivi karibuni
“Nimesikia mmechumbiana, hongereni napenda upendo, ni kitu kizuri sana, naamini na mimi pia nitaolewa kwa sasa niko tayari kuingia kwenye ndoa.”
Aliongeza: “Sikujua hata kama nitakuwa kwenye uhusiano, kwa kweli, lakini nilipoanza kuwa kwenye hali nzuri kuhusu maisha yangu na kufanya kazi ya kujiponya. Labda Mungu alinifungulia nafasi ya kuwa na mtu anayenipenda kwa dhati hii ni mara ya kwanza najisikia huru na mwenye amani kupita kiasi.”
Kauli hiyo imezua gumzo mtandaoni, hasa ikizingatiwa kuwa Megan na Thompson wamekuwa kwenye uhusiano muda mrefu kidogo ukiwa unakaribia mwaka sasa tangu walipotangaza kuwa wapenzi Julai mwaka jana.
Tangu kuthibitisha penzi lao, wawili hao wamekuwa wakionekana mara kwa mara pamoja katika hafla mbalimbali, huku Megan akishirikisha mashabiki wake baadhi ya nyakati zao za faragha.
Mwezi Novemba, aliachia wimbo wa kimahaba uitwao ‘Lover Girl’ ambao uliingia kwenye nyimbo bora 50 ikiingia nafasi ya 38 kwenye chati ya Billboard Hot 100, wimbo uliotafsiriwa kama ishara ya furaha yake katika uhusiano.
Hadi sasa Thompson hajatoa taarifa yoyote kuhusu kauli ya mpenzi wake na kwa sasa mashabiki wake wanasubiri kuona kama nyota huyo wa Dallas Mavericks atamvisha pete rapa huyo, ambaye kwa sasa anaonekana kuwa kwenye penzi zito.