Dar es Salaam. Historia ya makipa kutoka Nigeria katika Ligi Kuu Tanzania Bara imeendelea kutokuwa ya kuvutia kufuatia uamuzi wa Singida Black Stars, leo Februari 27, 2026 kumsimamisha kipa Amas Obasogie kwa tuhuma za upangaji matokeo.

Obasogie anasimamishwa ikiwa ni takribani miezi 10 tangu kipa mwingine kutoka Nigeria, John Noble kuvunjiwa mkataba na Fountain Gate kwa makosa ya kucheza chini ya kiwango na kufanya makosa ya makusudi.

Taarifa ambayo imetolewa na Singida Black Stars leo imetangaza kusimamishwa kwa Obasogie kwa muda wa miezi mitatu japo haikuelezea kwa undani kosa/makosa ambayo kipa huyo ameyafanya.

Mbali na Obasogie, timu hiyo pia imemsimamisha kiungo na nahodha wa timu hiyo, Khalid Aucho kwa muda wa miezi kwa makosa ya utovu wa nidhamu.

“Uongozi kupitia Kamati ya Nidhamu umechukua hatua hizi kwa mujibu wa kanuni na taratibu za klabu,” imeeleza sehemu ya Singida Black Stars.

Singida Black Stars imemsimamisha Obasogie ikiwa ni saa chache tangu kipa huyo afanye kosa la kizembe katika mchezo wa Ligi Kuu dhidi ya Namungo FC uliochezwa jana, Februari 26, 2026 katika Uwanja wa Majaliwa, Ruangwa Lindi.

Wakati Singida Black Stars ikiongoza kwa bao moja, kipa huyo alishindwa kuukamata vizuri mkononi mpira wa faulo uliopigwa na Rodgers Gabriel ambapo baada ya kumponyoka ulimaliziwa vyema na Fabrice Ngoy aliyeipa Namungo bao la kusawazisha katika mechi hiyo iliyomalizika kwa sare ya bao 1-1.

Obasogie anasimamishwa na Singida Black Stars, mwezi mmoja na siku kadhaa tangu alipokuwemo katika kikosi cha Nigeria kilichomaliza kwenye nafasi ya tatu katika Fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) zilizofanyika Morocco.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *