KATIKA kuadhimisha Siku ya Wanawake Duniani itakayofanyika Machi 8, 2026, Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi imeandaa kliniki maalum ya ardhi kwa wanawake ijulikanayo kama ‘Samia Ardhi Kliniki’, itakayotoa msaada wa kitaalamu kuhusu masuala ya ardhi pamoja na utoaji wa hati miliki kwa wanawake waliokidhi vigezo.

Akitoa taarifa hiyo leo Februari 27, 2026 na Naibu Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Lucy Kabyemera amesema huduma hiyo itatolewa katika mikoa 26 ya Tanzania Bara na itaendeshwa na watumishi wanawake pekee. SOMA: Kampeni Mama Samia yaondoa mfumo wanawake kutomiliki ardhi Korogwe

Amesema kaulimbiu ya kliniki hiyo ni “Mwanamke; Haki Yako, Miliki Sasa,” ikilenga kuwafikia wanawake wengi zaidi na kuwawezesha kumiliki ardhi, ikizingatiwa kuwa kwa sasa ni takribani asilimia 28 tu ya wanawake wanaomiliki ardhi.

Kabyemera ameeleza kuwa utekelezaji wa kliniki hiyo ni sehemu ya maelekezo ya Rais Samia Suluhu Hassan ya kuwafikia wananchi moja kwa moja na kuwapatia huduma bora karibu na maeneo yao. Aidha amewataka wanawake kushiriki katika kliniki hiyo ili kupata elimu kuhusu haki na misingi ya umiliki wa ardhi, huku akiwahimiza wanaume kuwaunga mkono wake zao ili kunufaika na fursa hiyo.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *